Menu
in , , , , ,

Soka ni biashara

Tanzania Sports

Manager's

Soka ni biashara ya pauni bilioni

*Kulikoni ugeugeu kuajiri makocha?

Yapo mambo mengi ya ajabu kwenye soka, yanayoacha maswali mengi kuliko majibu, licha ya ukweli kwamba hii sasa ni biashara zaidi ya burudani, tena ya mabilioni ya pauni.

Ugeugeu, kutowaamini makocha, kuwapa muda mfupi na kuwafukuza ghafla bila hata notisi huku klabu zikitaka mafanikio ya haraka ni baadhi ya tabia za wamiliki na viongozi wa klabu – hata zile kubwa kabisa za Ulaya.

Uhafidhina katika utamaduni wa biashara, kutoa muda wa kutosha kwa kocha na jopo lake kuzoeana na wachezaji na kusuka kikosi imara, kisha kutia imani kwa kocha ni mambo yanayoweza kudaidia kubadili mwenendo ‘kichaa’ wa uongozi kwenye klabu za soka.

Julian Nagelsmann ni kocha mwenye umri mdogo – miaka 32 tu lakini anafanya makubwa. Akiwa ameegama kwenye sofa katika jengo la akademia ya klabu ya Red Bull Leipzig ya Ujerumani, anaonekana kujiamini kuliko baadhi ya wakongwe.

Huyu ni kocha wa soka la kulipwa katika klabu tuliyozoea kuiita RB Leipzig wanaocheza Ligi Kuu ya Ujerumani – Bundesliga. Anakumbukia mwaka juzi – 2018, akiwa kwenye sofa hilo hilo, alipigiwa simu na Mkurugenzi Mtendaji wa Real Madrid, Jose Angel Sanchez ili achukue mikoba ya ukocha huko.

Wakati Sanchez alitaka Mjerumani huyu aingia Santiago Bernabeu kuwaongoza wachezaji kwenye mafanikio, Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa Manchester United, Ed Woodward, anakiri kwamba amekuwa akimfuatilia kocha huyo kwa makini, ikionesha kwamba ni aina ya mjuzi ambaye klabu kubwa Ulaya zingependa kuwa naye.

Akiwa kwenye ukumbi wa mikutano ambao kwa kawaida hutumiwa kwa ajili ya mijadala ya upataji na usajili wa wachezaji, Nagelsmann anazama kwenye mawazo, akishindwa kuelewa inakuwaje moja ya michakato muhimu zaidi kwenye soka huchukuliwa kiujanja na kutiwa dosari kwa kiasi kikubwa.

Kuajiri kocha ni suala zito – ni gharama kwa sababu athari yake huja kuonekana kwenye timu – matokeo na fedha zinazoingia kwenye klabu ya timu husika kutokana na kupanda chati kwa timu. Si suala rahisi rahisi kama wengine wanavyochukulia – kunyanyua sim utu na kuahidi kumwandika kazi mtu bila kuwa utafiti wa kina umefanyika na kukubaliana kwa kina vigezo na masharti ya kufuatwa.

Nagelsmann amekuwa akikataa mienendo inayomfikia ambayo kimsingi haiendani na mbinu zake. Hiyo ni moja ya sababu zilizomfanya akatae maombi ya Real Madrid. Anaamini kwamba ukaribu wa kutosha kati ya kocha na wachezaji ni jambo la muhimu, na kwake, akaona kwenda Real haingeweza kufaa kwa muda mfupi kwani wala hawezi kuzungumza Kihispaniola.

Bwana huyu anasema kwamba kuna klabu ambazo hawezi kufikiria kabisa kuchukua nafasi hiyo ya juu ya ukocha kwa sababu ya mifumo yao haipo wazi, uendeshaji ni wa shaka, na kwamba unakuta yapo mawazo tofauti mno kutoka kwa watu wengi kupita kiasi klabuni ambao pia wanalazimisha kuwa na ushawishi.

Kocha huyu anakiri kwamba wengine wanaweza kumpenda kutokana na mambo yanayoendelea kwenye eneo lake la kazi kuliko hata kutazama kwa makini na kina kazi yake. Kwa msingi huu, mabosi wa soka wajue kwamba Nagelsmann anawafanyia utafiti wa kina zao wao na klabu zao kuliko wenyewe waliokwisha kumfanyia yeye.

“Kitu muhimu zaidi kwa klabu ni kuwa na utambulisho wao, falsafa yao na aina ya uchezaji na wakishajitambua ndipo wateue kocha anayeendana na kile wanachotaka na si wanavyofanya sasa, kumchukua tu mtu kwa sababu ya jina lake,” anasema Nagelsmann.

“Kuna wakati napata katika klabu nyingi za Ulaya kwamba katika msimu mmoja wanataka kuwashambulia wapinzani wao mapema sana na pia kutumia mashambulizi ya kushitukiza dimbani. Mara wanamfukuza kocha na kuanza mfumo tofauti wa kumiliki mpira muda mrefu hata kama ni kwenyeeneo lao. Uendelevu unakosekana kwa kufanya hivyo.

“Unatakiwa kuwa makini kwenye kazi na kama unataka kubadili mambo inachukua muda. Sasa unakuta mambo yanafanyika hovyo hivyo tu, unabadilisha wachezaji, unabadilisha uskauti, unabadilisha kila kitu katika muda mfupi; sasa hiyo haina mantiki. Bila mwelekeo sahihi, unaishia kwenye matatizo,” anasema kocha huyu mdogo.

Utafiti uliofanywa na ‘Optimal Football’ kwa kufuatilia ligi kuu tano kubwa za Ulaya katika kipindi cha miaka mitano unaunga mkono uchambuzi wa Nageelsmann. Uchambuzi huo ulihitimisha kwamba asilimia 75 ya timu zilimtumia kocha mkuu wao kama mtu anayefanya uamuzi mwingi kama si wote kuhusiana na masuala ya kiufundi na mikakati ya kisoka.

Sasa unapombadilisha kocha mkuu, inamaanisha kwamba moja kwa moja klabu inatakiwa kubadili mikakati pia kwa sababu hii ina msingi wake moja wa moja chini ya kocha mkuu. Ukitazama kiasi cha fedha kinachotumika kwenye kubadili wachezaji kwa kuwasajili kutoka klabu moja kwenda nyingine – kima cha pauni bilioni 5.3 (kwa kiangazi kilichopita tu) huku taassisi za soka zikielekea kuwa kubwa sana kibiashara, inawezekanaje kubadili kocha ghafla ghafla tu? Ni kuharibu fedha na mwelekeo wa soka.

Mads Davidsen, mwasisi wa Optima Football anayeshauri klabu katika mabara matatu tofauti, anaamini kwamba tabia hiyo ya wenye klabu na viongozi wao dhidi ya makocha inatokana a utamaduni wa kihafidhina wa kutotaka kuondokana na kile ambacho tayari kimefanywa.

Kadhalika kuna utamaduni unaoibuka wa kila timu kutaka kujiendesha kama wengine au kufuata mkumbo tu. Tazama mifano ya mafanikio ya sasa ya Liverpool, Manchester City, Leicester na Wolves. Hebu pia rejea alichofanya Nagelsmann na wachezaji wake dhidi ya Tottemhan Hotspur katika Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL).

Spurs walishitukiza wakamwondoa Mauricio Pochettino ambaye kiangazi kabla hakuwa amepewa hata senti ya kufanya usajili, na mara moja wakachukua jina kubwa – Jose Mourinho aliyetoka kukaa ndani baada ya kufukuzwa Manchester United.

Huko nako alikuwa ameshindwa kwenda na Man United wanayotaka washabiki. Ndiyo maana hata huko awali walisita kumchukua, maana si kocha anayeendana na mfumo wa Manchester United inayojulikana na wengi tangu zama za Sir Ale Ferguson.

RB Leipzig waliwapiga Spurs nyumbani kwao Ujerumani na hapa hapa London, Mourinho akiwa hana jipya la kufanya na wachezaji aliorithi na ambao hajawazoea wala hawajaweka mfumo rasmi wa kucheza wenye ufanisi na uendelevu.

Ndiyo maana mwanasoka wa zamani wa Manchester United ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka, Garry Neville, alisema Mourinho na Spurs ni sawa na ndoa ya kirahisi rahisi tu au urafiki wa shaka usiolenga mafanikio ya klabu. Bali, ni kwamba Mourinho alihitaji kazi huku Daniel Levy (Mwneyekiti wa Spurs) akihitaji kupaisha jina kwa kuchukua jina kubwa.

Mwaka 2014 Pochettino alilipiwa pauni milioni mbili tu na Spurs kutoka Southampton. Huu utabaki kwenye majalada kama uamuzi mzuri na mafanikio kwao, ikizingatiwa utajiri uliojengeka katika ushiriki wao kwenye UCL kwa miaka minne, ikiwa ni pamoja nakufika fainali yake mwaka jana na kutolewa na Liverpool.

Wakaja wakamfukuza nlakini wakashindwa kuweka mbadala sahihi. Hii inaonesha ukosefu wa intelijensia na jitihada sahihi za kuteua kocha mpya. Klabu zinaweza ‘kuvunja benki’ kwa ajili ya kusajili wachezaji lakini hawataki kujielekeza vyema kwenye kukubali kupata kocha ghali na sahihi kwa wachezaji wale. Hawataki kocha atakayekuja kuwapa mafanikio ya muda mrefu – wanataka kufumba na kufumbua wawe na makombe yote ndani na nje ya nchi. Wanashindwa kuelewa dhana ya ukocha.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version