Menu
in

Soka Afrika Mashariki limerudi gizani

Taifa Stars

Taifa Stars

Wachezaji wengi wa Afrika mashariki wameonekana kutokuwa na mwendelezo wa viwango vyao. Ni kama vile soka lenyewe linaugua homa za vipindi.

MATOKEO ya michezo ya makundi ya timu za Afrika mashariki kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zimeingia shubiri. Ukanda huo ukiwa na nchi wanachama 10 umeshindwa kufurukuta katika kandanda na kuzishuhudia timu za Afrika magharibi na kaskazini zikiendeleza ubabe wao.

Ukanda huo unawakilishwa na mataifa ya Somalia,Djibout,Burundi, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda, lakini ndoto za kuendeleza wimbi la mafanikio limeyoyoma.

Si Tanzania iliyofuzu kwa mara kwanza mwaka 2019 baada ya kukosekana kwa miaka 40 wala Uganda iliyokuwa ikitegemewa kufanya vizuri na jirani zao Kenya,Rwanda na Burundi hazijafua dafu mwaka huu.

Katika fainali za AFCON mwaka 2019 ukanda wa Afrika mashariki uliwakilishwa na Burundi,Tanzania,Uganda na Kenya. Yalikuwa mataifa manne ambayo yalionesha namna soka la Afrika mashariki linavyokua, lakini ghafla mwaka mmoja baadaye hali imekuwa tofauti.

Jambo kubwa zaidi mmoja wa wanasoka wa Afrika mashariki alikuwa miongoni mwa nyota waliokuwa kwenye orodha ya wafungaji bora. Emmanuel Okwi wakati huo akichezea klabu ya Simba alikuwa miongoni mwa nyota wa Uganda waliofanya vizuri kwenye mashindano hayo yaliyofanyika nchini Misri.

Ule umahiri wa Tanzania,Burundi,Uganda na Kenya wa mwaka 2019 hautaonekana kwenye mashindano ya AFCON mwaka huu. Licha ya kumrejesha Jacob Mulee kwenye benchi la Ufundi lakini Harambee Stars haijafanikiwa kufuzu.

Tanzania nayo ilimrejesha Kim Poulsen lakini haikufanikiwa kufuzu baada ya kukubali kipigo cha bao moja kwa nunge dhidi ya Guinea Ikweta. Ushindi wa 1-0 dhidi ya Libya haukuwa na msaada wowote wa Tanzania zaidi ya kulinda heshima ya soka.

Tanzania ikiwa na mastaa wake Simon Msuva, Mbwana Samatta, Nickson Kibabage, Aishi Manula na wengineo hawakufua dafu katika kundi J ambalo limezishuhudia Guinea Ikweta na Tunisia zikifuzu kwa mashindano hayo.

Kenya ikiwa na nyota Wanyama,Michael Olunga ambaye amewahi kukipiga Ligi Kuu Hispania, La Liga,Francis Kahata,Joash Onyango wameshindwa kufanya vizuri kwa kuiwezesha Harambee Stars kufuzu mashindano hayo.

Uganda wakiwa na nyota wao Dennis Onyango na Taddeo Lwanga wameshindwa kutia fora kwenye hatua za kufuzu kwa AFCON mwaka huu na kuhitimisha wakati mgumu.

Swali kubwa la kujiuliza ni kwanini timu za taifa za ukanda wa Afrika mashariki hazina mwendelezi wa ubora wao? Mashindano ya AFCON yalifanyika mwaka 2019 ikiwa ni miezi 12 pekee imepita nchi hizo zimeonekana kupoteza ubora. Wachezaji wameongezwa, makocha wamebadilika na kadhalika, lakini je hizo ni sababu za kushindwa kufuzu AFCON?

Tanzania ilikaa miaka 40 bila kufuzu, kwahiyo kwa vigogo wa soka Afrika kutowaona Taifa Stars sio habari. Uganda na Kenya nao wamekuwa wakihaha huko na huko wakiwa na mastaa wao mbalimbali barani ulaya lakini hawajafuzu.

Mwaka 2004, ukanda wa Afrika mashariki uliwakilishwa na timu mbili za Rwanda na Kenya kwenye mashindano yaliyofanyika nchini Tunisia.

Wachezaji wengi wa Afrika mashariki wameonekana kutokuwa na mwendelezo wa viwango vyao. Ni kama vile soka lenyewe linaugua homa za vipindi.

Ukitazama ,afanikio ya klabu ya Simba msimu huu unaweza kuyahamishia katika timu ya taifa. Kwanza Simba wanaongoza kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika na pia wamekuwa vinara ambao wametikisa soka Afrika. Halafu Taifa Stars imetoka kushiriki mashindano ya CHAN ya wachezaji wa ndani barani Afrika, licha ya kutofanya vizuri ilitegemewa kuwa wangetumia kama nyenzo ya kufanikiwa zaidi.

CHAN ni mashindano ambao yanawezesha wachezaji wa Ligi za ndani barani Afrika kuonmesha vipaji vyao, lakini kwa upande wa Afrika mashariki inaonekana bado hatujagundua njia sahihi ya kufanikiwa na kuyalinda mafanikio yenyewe.

Ikiwa chini ya miezi 12 tumeshindwa kufuzu AFCON, je ni wakati gani timu zetu zinaonesha umwamba wa soka mbele ya mataifa kama Ghana,Nigeria,Togo,Morocco, Ivory Coast na mengine?

Kila linapofika suala la mashindano timu wanachama wa CECAFA wamekuwa kama wasindikizaji. Hakuna timu iliyowahi angalau kufika robo fainali ya AFCON. Zote zinaishia hatua za awali jambo ambalo linaonesha namna gani tuna uwezo mdogo mbele ya washindani wenye maarifa ya kutosha.

Njia pekee ya kuweza kuwa na maarifa ya kutosha kwenye soka ni kuhakikisha elimu ya michezo na bajeti za serikali katika sekta hiyo zinazalisha wachezaji wakubwa kama ukanda wa Afrika maghribi na kuwa sehemu ya nyota wanaotamba Ulaya na kwingineko.

Jitihada za kuwika na kuchanua za mwaka 2019 zilitarajiwa kuwa hatua ya kwenda juu kimafanikio lakini bado safari yetu inaonekana kuwa dhaifu na sasa soka limerudi gizani.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version