Tanzania ndiyo nchi pekee ambayo watu wake bado wana amini kujua kuongea lugha ya kiingereza ni ufahari na kitambulisho cha kuwa msomi.Idadi kubwa ya watanzania hawajui kuongea lugha hiyo ya Malkia na kiukweli,wanajisikia unyonge sana.Wale wanyeuwezo wa kuzungumza lugha hiyo,wanaona kama maisha tayari wameshayapatia! Jamani,tumerogwa?
Siku ya jumapili ya 11 mei,pazia la ligi kuu nchini Uingereza lilifungwa rasmi kwa michezo yote huku macho na masikio yakielekezwa pale Anfield kwenye mchezo kati ya Liverpool ambao ulimalizika kwa majogoo hao wa jiji kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 huku pale Etihad,timu ya Manchester city wakiibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kutangazwa rasmi kuwa mabingwa wapya wa EPL msimu wa 2013/2014.
Baada ya mechi hiyo,yalifanyika mahojiano ya wachezaji wawili wa timu ya Man City,Sergio Aguero raia wa Argentina na Samir Nasri kutoka Ufaransa.Sergio Aguero alionekana kutojua kabisa lugha ya kiingereza iliyokuwa inatumika na muda mwingi alipokuwa anaulizwa maswali na waandishi wa habari,alionekana kujiuma uma tu! Habari haikuwa kubwa sana pale Uingereza lakini,tukio kama hilo linapotokea kwa wachezaji wetu wa Kitanzania,balaa huwa linazuka! maneno ya kashifa na kejeli huwatoka watu kama mvua! jamani,tumerogwa?
Wataalamu wa Isimu ya lugha wanabainisha wazi kabisa kuwa,mtu anayejifunza lugha ya pili baada ya kuwa amebalehe au kuvunja ungo,hawezi kupata umahiri wa lugha hiyo ya pili unaolingana na mzawa wa lugha husika.Maana yake ni kwamba,unaweza kujifunza na kujua kabisa lugha hiyo lakini huwezi kuimudu kama mzawa anavyoweza kufanya.Wanaoweza kuimudu lugha ya pili ni wale tu walioanza kujifunga wakiwa chini ya umri wa miaka 13.
Kujua lugha zaidi ya moja kwa mwanasoka,sio jambo baya na kutojua pia,sio dhambi.Wapo wachezaji wengi amabao wanauelewa wa lugha zaidi ya moja.Watu kama Romelu Lukaku wa Chelsea na Kelvin Prience Boateng wa Shalke 04 wanauwezo wa kuzungumza lugha zaidi ya tano na wapo wengi tu lakini,uwezo wao wa kumudu lugha hizo hauna uhusiano wa moja kwa moja na kile wanachotakiwa kukifanya uwanjani.
Napata shida sana kubaini tofauti ya Sergio Kun Aguero na Kelvin Yondani kwenye suala la lugha hiyo ya Malkia.Pamoja na kuwa hata Samir Nasri alikuwa anajing’ata ng’ata akihojiwa,Aguero haweza kabisa! Carlos Tevez alipata kuzichezea klabu tatu za ligi kuu Uingereza (West Ham United,Man United na Man City) na kuishi Uingereza kwa miaka saba lakini,linapokuja suala la kuzungumza lugha ya kiingereza,huwa ni vituko vitupu,hana anachojua.Kwa nini umponde “Nadir Hourub Canavaro” kwa kiingereza chake cha kuvizia? Hapana,tunawaonea bure watu wetu.
Kocha wa timu ya Southampton ya Uingereza,Muajentina Mouricio Pochettino alifika Uingereza hajui hata neno moja la kiingereza na mara kadhaa amekuwa akitumia mkarimani pindi anapofanya mkutano na waandishi wa habari,unadhani ameishusha daraja timu yake? hapana,yeye ni moja ya makocha walifanya vizuri sana msimu huu.Ukitaka kujua ubora wake,waulize Man City na Chelsea kilichowapata msimu huu pale walipotua St.Marrys Stadium,watakupa jibu.Mara kadhaa kocha huyo amekuwa akisisitiza kuwa,lugha ya mpira ni ya kimataifa,inahusisha zaidi matendo kuliko maneno.
Mshambuliaji wa TP Mazembe,Mbwana Samatta naye kwa nyakati tofauti amewahi kumulikwa na kamera za watanzania akihojiwa kwa lugha ya kiingereza na wengi huwa wanamponda kutokana na kuunga unga maneno ya lugha hiyo iliyoletwa Tanzania kwa usafiri wa Ndege.Jamani,tumerogwa? kama Antonio Vallencia tu huwa anajikanyaga linapokuja suala la lugha hiyo,sembuse mtoto wa Mbagala?
Lugha ya kuzungumza ni kitu kidogo sana kwenye mchezo wa soka na wala haina ulazima kwa mchezaji kuwa mtaalamu wa Sarufi.Lugha ya soka haihitaji sentesi zilizonyooka,inahitaji zaidi matendo.Siku nikiamka asubuhi na kusikia TFF wametuleta kocha Mchina ambaye anajua lugha ya kichina tu,wala siwezi kuhofia mradi tu awe na utaalamu wa mchezo huo.Kuhusu lugha,najua tu kina Ramadhani Singano watamuelewa.
Hivi mtu kama Nicholous Anelka au Zlatan Ibrahimovic wangejifunza lugha ngapi? hawa ni baadhi ya wachezaji ambao wamecheza soka kwenye nchi mbalimbali ambako wanazungumza pia lugha tofauti.Ukikazania sana sarufi ya lugha,unaweza kujikuta unajua namna na kunyoosha sentensi halafu unasahamu namna ya kuutuliza mpira mguuni! Tunapowabeza wachezaji wetu kisa hawajui kuzungumza lugha ya watu,tunawaonea bure kabisa.Hata kwenye tuzo za mchezaji bora wa Dunia mwaka huu,tumeshuhudia wanasoka wengi wakiongea lugha za kwao japo baadhi wanafahamu pia lugha ya kiingereza.
Nina uhakika Aguero angepewa nafasi ya kuchagua lugha ya kujieleza,asingechangua Kiingereza ambacho hakiwezi.Angechagua lugha ya kwao ambayo anaimudu vizuri.Kuna lugha ziliiteka dunia na sasa,hazipo tena.Lugha ya Kigiriki na Kilatini,zilikuwa na nguvu sana siku za nyuma na sasa hazipo tena.Ni vizuri kwa mchezaji kujua lugha nyingi hasa kiingereza kwa sasa lakini,usipojua pia sio dhambi.