Kwenye mpira timu mbalimbali hutumia mbinu tofauti tofauti kwenye kushambulia. Timu inaweza kutumia eneo la katikati ya uwanja kama sehemu ya kutengeneza mashambulizi ndani ya uwanja. Kuna wakati timu inaweza kutumia mipira mirefu kutoka nyuma mpaka mbele kama mbinu ya kutengeneza mashambulizi.
Kuna wakati timu inaweza kutumia maeneo ya pembeni kutengeneza nafasi za kufunga. Mbinu zote nilizozitaja hapo juu za namna ya kutengeneza nafasi ya kufunga ni mbinu ambazo washambuliaji wa pembeni (wingers) huwa wanakuwa na umuhimu mkubwa sana kufanikisha mpango wa timu husika.
Washambualiji wa pembeni (wingers) mara nyingi hukaa pembeni mwa uwanja kwenye mapana ya uwanja iwe kushoto au kulia. Hawa husaidia sana kwenye kushambulia na kuna wakati hutumika vizuri sana kwenye kujilinda wakati timu haina mpira.
Asilimia kubwa wachezaji hawa wanatakiwa kuwa na kasi, uwezo wa kukokota mipira, uwezo wa kutumia uwazi (space), nguvu na uwezo wa kupiga krosi ambazo huwafikia washambuliaji wa kati kwa ajili ya kufunga.
Kipindi cha kilele cha mafanikio ya Manchester United iliwahi kupata mshambuliaji wa pembeni (winger) aliyekuwa anatokea pembeni kushoto, Ryan Giggs. Mchezaji kutoka Wales. Mchezaji ambaye alicheza kwa mafanikio Manchester United ambapo alifanikiwa kuchukua vikombe 13 vya ligi kuu ya England.
Ryan Giggs alikuwa na kasi, uwezo mkubwa wa kukokota mpira , uwezo mkubwa wa kukaa sehemu zenye uwazi (spaces) na uwezo mkubwa wa kupiga krosi ambazo zilizalisha magoli ndiyo maana Ryan Giggs alifanikiwa kutengeneza nafasi za kufunga (assists) 277 kwenye ligi kuu ya England na kuweka rekodi ya mchezaji mwenye assists nyingi kwenye ligi kuu ya England mpaka sasa.
Wakati natazama mechi ya Simba SC na Coast Union jicho langu lilikuwa makini sana kila alipokuwa anachukua mpira mchezaji wa kimataifa wa Simba SC kutoka Zambia, Joshua Mutale, huyu ni moja ya wachezaji wa pembeni (wingers) wa Simba SC ambao wanategemewa kutengeneza magoli uwanjani.
Kimo cha Joshua Mutale kilinikumbusha kimo cha Garrincha, mshambuliaji wa pembeni (winger) wa Brazil ambaye kwa jina la utani alikuwa anaitwa “Little bird” yani ndege mdogo kutokana na umbo lake.
Garrincha alikuwa na umbo dogo na mfupi kama alivyo Joshua Mutale. Pamoja na kwamba Garrincha na Joshua Mutale wanafanana kwa kiasi kikubwa vimo vyao lakini hawafanani kwenye eneo la mwisho la maamuzi pindi wanapokuwa na mpira.
Garrincha alikuwa na kasi kama ambavyo Joshua Mutale alivyo na kasi. Garrincha alikuwa na “control” ya mpira kitu ambacho Joshua Mutale hana. Garrincha alikuwa na uwezo mkubwa wa kukokota mpira bila kupoteza ovyo kitu ambacho kwa Joshua Mutale hakipo, yeye ni rahisi kupoteza mpira.
Garrincha alikuwa na uwezo mkubwa wa kufunga pamoja na kutengeneza nafasi za kufunga kitu ambacho Joshua Mutale hana kwa kiasi kikubwa. Ukosefu wa vitu vingi kwa Joshua Mutale kuna mfanya awe mchezaji wa kiwango cha kawaida.
Yanga ilibahatika kuwa na mchezaji wa kimataifa kutoka Congo, Tuisila Kisinda. Alikuwa na kasi sana kipindi alipokuwa na mpira lakini maamuzi yake ya mwisho yalikuwa hayana madhara. Anaweza kukimbia na mpira lakini akaishia kufanya maamuzi ambayo hayana manufaa kwa timu.
Uwezo huo wa Tuisiala Kisinda ndiyo uwezo ambao Joshua Mutale kwa sasa anao. Hana ule uwezo mkubwa ambao mshambuliaji wa pembeni anatakiwa kuwa nao. Hana uwezo wa kuwa sehemu ya kutengeneza nafasi ya magoli au kufunga magoli kwenye timu.