Menu
in , , ,

Singida United, anzeni walipokosea Mbeya City

Tanzania Sports

Mapinduzi ya kizazi kipya cha watu kujivunia na kuzipenda timu zao za
mikoani yalianzia kwa Mbeya City.

Timu ambayo wana Mbeya walijivunia kuishabikia, kuipenda na kuisaidia
kwa hali yoyote kadri ambavyo uwezo wao ulivyo waruhusu.

Mbeya City hawakuwaangusha mashabiki wao mwanzoni, waliwapa furaha
ambayo walitazamia kuipata kipindi ambacho wanaishabikia timu.

Msimu wao wa kwanza kwenye ligi kuu walionesha ushindani wa hali ya
juu, wakafanikiwa kuingia katikati ya wazee wawili wa mpira hala
Tanzania ( Simba na Yanga)

Kabla ya ligi kumalizika watu wengi waliipa nafasi Mbeya City kuchukua
kombe, na hii ni kwa sababu ya matamanio ya watu wengi.

Matamanio ambayo yalikuja kutokana na wao kuchoka kushuhudia kila siku
Simba na Yanga wakibadilishana kombe la ligi kuu.

Matamanio ambayo yaliifanya Mbeya City kupata mashabiki ambao hata
siyo wazaliwa wa Mbeya, mtu wa Mwanza akawa anajivunia kuishabikia
Mbeya City kwa sababu tu ya matokeo waliyokuwa wanayapata ndani ya
uwanja.Mbeya City ikawa na mvuto mkubwa ndani na nje ya uwanja

Hamasa hii iliwapa nguvu Mbeya City na ilifanikiwa kumaliza ligi ikiwa
nafasi ya tatu ( 3) , haya yalikuwa mafanikio makubwa sana kwao kwa
sababu ndiyo kwanza ulikuwa msimu wao wa kwanza.

Mafanikio ambayo yaliwafungua watu wengi kutoka mikoa mingi hapa
nchini na kuona kumbe kuna uwezekano wa kupata furaha kwa kutumia timu
za ndani.

Hamasa ya wana Mbeya kwa Mbeya City iliwavutia wengi, na viongozi wa
Mbeya City wakaitumia nafasi ile kwa ajili ya kupata wadhamini kwenye
timu.

Ndiyo ikawa timu ya kwanza kuwa na wadhamini wengi kwenye timu kati
ya timu zilizokuwa zinashiriki ligi kuu, kitu ambacho kilionesha
timu yao inaendeshwa katika misingi ya kisasa.

Pamoja na ugeni wao, uchanga wao walifanikiwa kufanya jambo ambalo
Simba na Yanga liliwashinda.

Sifa zikazidi kwao, kiasi kwamba zikawa kama upepo ambao ulikuja
kuwayumbisha wao na kupotea kwenye njia ambayo walikuwa wamepanga
kupitia.

Mbeya City rasmi ikaanza kupoteza mvuto, matokeo yao uwanjani yakawa
hayavutii, lile tumaini la wengi kupata timu ambayo inaendeshwa kisasa
likawa limepotea tena.

Mbeya City ikaingia rasmi kwenye siasa za Simba na Yanga, waungwana
wakaanza kujitoa taratibu na kukaa pembeni kusubiri mtu mwingine
atakayeweza kuleta timu ambayo inaendeshwa kisasa.

Miaka kadhaa imepita, Tanzania tumefanikiwa kupata timu nyingine
ambayo inaonekana inaendeshwa kisasa.

Timu ambayo haimilikiwi na wanachama ila ni ya mtu binafsi.

Timu ambayo msimu huu ndiyo msimu wake wa kwanza kwenye ligi kuu
lakini mpaka sasa ina wadhamini saba( 7).

Singida United wamefanikiwa kupata wadhamini wengi bila kuwa na hamasa
kubwa ya mashabiki nyuma yao kama ilivyokuwa kwa Mbeya City.

Viongozi wake wamekaa chini, wakatengeneza namna sahihi ya wao kupata
wadhamini ambao watakuja kuwekeza katika timu yao.

Walijua mapema kuwa hakuna mfanyabiashara ambaye asingependa kutangaza
bidhaa yake sehemu ambayo inafuatiliwa kwa ukubwa kama ligi kuu.

Walitengeneza namna sahihi ya kuwashawishi wafanyabiashara hawa na
kuwaonesha namna watakavyonufaika kama watawekeza kwenye klabu.

Ushawishi mzuri husaidia kupata nyama iliyonona, tunavyoongea kwa sasa
Singida United hawana matatizo kama vilabu vingine ambavyo vilipanda
ƙligi kuu msimu huu.

Gharama za uendeshaji wa timu kwao zimepungua kwa kiasi kikubwa.

Ni kitu kikubwa na cha kuwapongeza, lakini tunapowapongeza tusisahau
kuwakumbusha kuwa hicho walichokifanya ni kitu kidogo ndani ya vitu
vikubwa wanavyotakiwa kufanya.

Wana hatua mia za kufikia mafanikio makubwa lakini mpaka sasa wamepiga
hatua moja peke yake.

Nina tamani hatua yao ya pili kuiona, hatua ambayo itakuja na mikakati
ya kuendeleza misingi sahihi ya mpira.

Leo hii wanatumia gharama kubwa kununua wachezaji wakubwa, siyo kitu
kibaya kwa mwanzoni. Wanatakiwa kufikiria namna sahihi ya kutengeneza
njia ambayo itawawezesha kutengeneza na kulea vipaji vipya ambavyo
vitakuja kuisaidia timu yao kwa baadaye.

Maendeleo ya mchezo wowote msingi wake huanzia kwa vijana wadogo, bila
kuwekeza kwenye vituo vya kuibua, kulea na kuendeleza vipaji hutokuwa
na msingi imara wa maendeleo ya mchezo wowote kwa Taifa.

Kama Singida United wamefanikiwa kupata wadhamini zaidi ya watano
ndani ya msimu mmoja, naamini wana nafasi kubwa ya kutengeneza
miundombinu imara itakayowawezesha wao kujiendesha kisasa zaidi.

Tuna makampuni mengi ambayo Singida United wanaweza kuyatumia kupata
hostel ya timu ya vijana na uwanja kikubwa ni wao kuandaa njia ya
kibiashara ambayo itamshawishi mtu.

Mfano, mfanyabiashara yoyote hutegemea bidhaa yake kutangazwa mara kwa
mara ili iweze kuwa akilini mwa mnunuzi kwa muda mrefu.

Mfanyabiashara yupi atakataa kipindi utakapomfuata akutengenezee
kiwanja ambacho jina la kiwanja litakuwa jina la bidhaa yake?

Bidhaa yake unaipa nafasi ya kutamkwa kwa muda mrefu kwa kutumia jina
la hostel au uwanja ambao Singida United wataumiliki wao.

Hapa ndipo Mbeya City hawakupafikia, pamoja na kwamba walikuwa na
hamasa kubwa kutoka kwa mashabiki lakini hatua hii hawakufanikiwa
kuifikia, natamani Singida United kuwaona wakiifikia baada ya wao
kuipita ile hatua ya Mbeya City kufanikiwa kupata wadhamini

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version