Menu
in , , ,

SINGANO, MAHUNDI KABEBA ‘JENEZA’ BEGANI MWAKE.

Tanzania Sports

Maisha ni kama hadithi unayosoma, usomacho kwenye hadithi ndicho
kilichopo kwenye maisha ya kawaida.

Furaha huwepo kwenye hadithi, hata kwenye maisha ya kawaida kila
mwanadamu kuna sekunde yake furaha ya atakayokuja kupitia.

Huzuni na machukizo huandikwa kwa ustadi mkubwa kwenye hadithi, pia
mwanadamu hupitia huzuni na machukizo katika kiwango cha kusikitisha.
Na hii yote ni kuonesha maisha hubadirika sana kama hadithi.

Leo hii hadithi ya Mrisho Ngassa imeongezewa neno Mbeya City, mara
baada ya kushindwa kuwa miongoni mwa wachezaji waliowahi kuchezea
Westham.

Tutabaki kuwahadithia wajukuu zetu Ngassa aliwahi kukabana na beki
kisiki Rio Ferninand.

Kuna wakati waweza ukawa unahisi umekaa sehemu sahihi na salama,
usahihi na usalama wa sehemu husika mara nyingi unategemea na nyakati
ambazo unaishi kwa wakati huo.

Kuna nyakati zimepita na ni ajabu sana ukionekana kuishi nyakati hizo
kipindi hiki ambacho mvua imekataa kunyesha.

Ni virahisi sana mtu kuona aliposimama ni sahihi na akashindwa kufanya
juhudi yoyote ya kujiondoa mahali aliposimama hata kama ni sehemu
mbaya.

Huitaji maji ya baridi kumfanya mtu atoke kwenye giza zito la usingizi
alilonalo, ataamka baada ya kumwangia maji ya baridi, lakini atarudi
kulala kama hutomuonesha sababu ya wewe kumwagia maji.

Unakumbuka kombe la Copa Coca cola la Mwaka 2009?, ukikumbuka vizuri
lazima uchungu ukujae kuhusu kipaji cha Ramadhani Singano.

Swali gumu ambalo nitachukua muda kulitafakari kama ukiniuliza kwanini
Singano yupo akitazama mbio za nyika wakati yeye ndiye alitakiwa kuwa
kiongozi wa mbio za hizi za Nyika?

Singano alitakiwa amkaribishe Farid ulaya, lakini sasa hivi dalili
zinaonesha Singano atakuwa anampokea mabegi Farid akiwa anatokea
ulaya.

Najua kuna nyakati ngumu sana huja kwenye maisha ya mwanadamu na
kuvuruga kila mwelekeo wake. Siku zote mwelekeo huvurugwa lakini ndoto
hubaki.

Jitihada dhabiti huitajika kutetea ndoto zako mpaka zitimie. Wakati
kama huu ndiyo unahitaji watu sahihi wa kukaa karibu na wewe na
kukushauri kuhusu maisha yako ya soka yanayoenda taratibu.

Ni wakati ambao wa kukumbuka maisha yako ya nyuma na kujiangalia
sehemu ambayo uliposimama muda huu nakujiuliza kama unatakiwa
kuendelea kuwepo pale ulipo au kuna ulazima wa nyayo za miguu yako
kuonja ardhi la sehemu nyingine?

Kuitwa Messi kulikuja na hatari pamoja na faida katika a maisha yako,
hatari yake ni kubweteka kwa jina lile, faida yake ni kupigana ufike
angalau robo ya mahali alipo Messi.

Chozi la mama Tanzania hutiririka kila wakati linapokumbuka vipaji
kama vya kina Singano vinapoonesha mwisho wake kuwa ule ule kama
mwisho wa vipaji vya kina Boban.

Ustadi wa kukimbia na mpira, kutoa pasi za mwisho, kuwapita mabeki
na kufunga magoli ndivyo vitu ambavyo vinaumiza kila jina lako
linavyopita kichwani kwangu.

Hujachelewa muda unao, uko kwenye klabu yenye mazingira mazuri tena
inayoshiriki michuano ya kimataifa ni wakati wako sasa kubadili
uwelekeo mbaya ili utembee kwenye ndoto zako.

Mwangalie Farid kwa jicho la wivu, umia kumuona alipo Ulimwengu na
ujifunze mengi kupitia Samatta. Baada ya hapo simama pigania kipaji
chako kwa hali ya juu.

Maumivu yoyote ndani ya moyo wako yasikufadhaishe, jaribu kujitafutia
furaha mwenyewe, ongeza bidii kwenye mazoezi huku ukiwa na hasira ya
wewe kuendelea kuwepo sehemu ulipo sasa hivi.

Nakutakia kila la kheri ndiyo maana nimekuja kukupa taarifa ya kwamba
nimemuona Mahundi akiwa amebeba Jeneza lako begani mwake.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version