Simba SC wameendeleza moto wao wa kushindania taji la Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya leo kuwaadhibu Ndanda FC kwa mabao matatu kwa sifuri ndani ya Uwanja wa Taifa jijini Dar-es-salaam. Kiiza alifunga mawili huku lingine likiwekwa wavuni na Mwinyi Kazimoto.
Simba waliuanza mchezo wakifanya mashambulizi mfululizo kwenye lango la Ndanda FC. Hata hivyo walinzi wa Ndanda wakiongozwa na Salvatory Ntebe walisimama imara na kuhakikisha lango lao linabaki salama.
Ingawa vijana hao wa Jackson Mayanja waliweza kutengeneza nafasi kadhaa huku Majabvi, Ndemla, Kiiza na Kazimoto wakipiga mashuti kadhaa lakini Ndanda walionekana kutulia kwenye eneo la ulinzi, jambo lililowawezesha kutoruhusu bao lolote kwa zaidi ya dakika 30 za mwanzo.
Hata hivyo Ndanda hawakuweza kutengeneza nafasi za kupiga mashuti kwa kuwa Simba walitawala sehemu kubwa ya mchezo huo.
Shambulizi la kwanza la hatari la Ndanda FC lilikuja kwenye dakika ya 31 ambapo Atupele Green alipiga kichwa safi kilichokuwa kikielekea wavuni baada ya kumpita Vincent Angban lakini Justice Majabvi alifanya kazi ya ziada na kuokoa mpira ule.
Mwinyi Kazimoto akaiandikia Simba SC bao la kuongoza mnamo dakika ya 36 akipokea krosi safi ya Ibrahim Ajib na kutulia vyema kabla ya kupiga shuti zuri lililomuacha mlinda mlango Jeremia Kisubi akiutazama mpira ukiingia wavuni.
Simba walidumu na bao lao hilo mbaka mapumziko. Ndanda FC walionekana kurudi na kasi kwenye kipindi cha pili wakifanya mashambulizi kadhaa ndani ya dakika kumi za mwanzo.
Lakini mnamo dakika ya 57 Hamis Kiiza aliunganisha kwa kichwa safi kona ya Ibrahim Ajib na kuwafunga Ndanda bao la pili ambalo lilizima ari ya vijana hao kutoka Kusini.
Dakika ya 72 ya mchezo ikamshuhudia kinara wa mabao Ligi Kuu Bara Hamis Kiiza akiiandikia Simba bao la tatu baada ya kupokea pasi nzuri ya Daniel Lyanga aliyekuwa ameingia kuchukua nafasi ya Ibrahim Ajib.
Bao hilo la Kiiza ni la 18 kutoka kwa mshambuliaji huyo raia wa Uganda anayeongoza kwenye orodha ya wafungaji akifuatiwa na Amisi Tambwe mwenye mabao 17.
Matokeo hayo yanawarudisha tena vijana wa Msimbazi kileleni wakiwa na alama 51 baada ya kucheza michezo 22.
Hata hivyo huenda wamekaa kileleni hapo kwa muda kwa kuwa wapinzani wao Yanga wana mchezo mmoja mkononi wakiwa na alama 50. Pia Azam wenye alama 47 wanayo michezo miwili wanapolinganishwa na idadi ya michezo ya Simba.