Simba SC wamefanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuwaadhibu
Singida United kwa ushindi wa 2-0 ndani ya dimba la Namfua jijini Singida kupitia mabao ya
Meddie Kagere na John Rafael Bocco.
Bao la kuongoza la Meddie Kagere lilifungwa na kinara huyo wa mabao kwenye dakika ya 10 ya
mchezo baada ya mlinzi wa Singida United, Salum Kipaga kufanya makosa alipojaribu kutuliza
krosi dhaifu iliyopigwa na Mohamed Hussein 'Tshabalala' na kujikuta akitoa nafasi kwa MK14
kuuweka mpira wavuni akiwa karibu kabisa na lango.
John Bocco alifunga bao lake la kichwa rahisi kabisa akibaki yeye na nyavu katika dakika ya 64
ya mchezo. Alipata nafasi hiyo ya wazi baada ya golikipa wa Singinda, Said Lubawa kuumia na
kutoka nje ya uwanja na hivyo krosi ya Emmanuel Okwi kumkuta mshambuliaji huyo akiwa
ndani ya eneo la hatari huku lango likiwa bila golikipa.
Ushindi huu wa leo umewafanya Wekundu hao wa Msimbazi kukamilisha jumla ya alama 91
ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote. Ni alama 8 zinazowatofautisha na Yanga walio
kwenye nafasi ya pili wakiwa na alama 83 huku timu zote mbili zikiwa zimebakisha michezo
miwili tu ili kufunga pazia la msimu huu wa VPL.
Simba wanatwaa ubingwa kwenye mchezo ambao hawakuweza kuonesha mpira mzuri
kutokana na ubovu wa eneo la kuchezea kitu kilichosababisha wachezaji kushindwa kupiga pasi
sahihi mara nyingi walipojaribu kisambaza mipira.
Kikosi cha Simba chini ya mwalimu Patrick Aussems kiliundwa na golikipa; Deogratius Munishi,
walinzi; Nicholas Gyan, Mohamme Hussein, Yusuph Mlipili, na Erasto Nyoni, viungo; James
Kotei, Haruna Niyonzima na Mzamiru Yassin pamoja na safu hatari ya ushambuliaji ya John
Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi.
Wenyeji Singida United kwenye safu yao walikuwa na Said Lubawa (golikipa), Frank Zakari,
Gilbert Mwale, Salum Kipaga, Kenned Wilson, Rajab Zahir, Boniface Maganga, Issa Makamba,
Jonathan Daka, Habib Kiyombo na Geoffrey Mwashiuya.
Michezo miwili ya Simba iliyosalia ni dhidi ya Biashara United utakaopigwa Mei 25 na ule dhidi
ya Mtibwa Sugar watakaocheza ugenini Mei 28.
Ni msimu wa mafanikio kwa kiwango gani kwa Simba na nyota wao?
Hakika ni msimu wa mafanikio makubwa mno Wekundu wa Msimbazi. Kwa mara ya kwanza
ndani ya miaka 15 Simba wamefanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Mara ya
mwisho vijana hao wa Msimbazi kutetea ubingwa wa michuano hiyo ilikuwa mwaka 2004
walipotwaa taji hilo la wakiwa na nyota kama Ulimboka Mwakingwe, Haruna Moshi na
wengine.
Katika kipindi chote hicho tangu 2004 wapinzani wao wa jadi Yanga wameweza kutetea taji hilo
la Ligi Kuu mara nne ikiwa ni pamoja na kulitwaa mara tatu mfululizo kwenye misimu 2014/15,
2015/16 na 2016,17.
Pengine ubingwa wa msimu huu kwa Simba unatoa ishara kuwa sasa wamezima rasmi zama za
utawala wa vijana wa Jangwani kwenye michuano hiyo kwenye misimu ya karibuni. Pia taji lao
hili la 20 linawafanya kuwa nyuma kwa mataji 7 pekee dhidi ya watani wao wa jadi kwenye
mataji ya jumla ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ukiwatazama kwenye michuano ya nje pia waliweza kuweka rekodi ya kufika kwenye robo
fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu walipofanya hivyo zaidi ya miaka 40 iliyopita. Uimara
waliouonesha kwenye michezo yao ya nyumbani kwenye michuano hiyo ya Klabu Bingwa Afrika
ulionesha kuwa kikosi chao cha msimu huu ni moto wa kuotea mbali. Baadhi ya watu wanadai
kuwa hiki ni kikosi bora zaidi kwenye historia ya Simba ya muda wote.
Makali zaidi yameoneshwa na safu yao hatari ya ushambuliaji ambayo inaundwa na Meddie
Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi. Safu hiyo imefunga mabao 54 mbaka sasa kwenye
msimu huu wa VPL ambayo ni mengi kuliko mabao ya timu nyingine yoyote ya VPL msimu huu
ukiwatoa Yanga ambao hata hivyo wameuzidi utatu huo wa Simba kwa bao moja pekee wakiwa
na mabao 55 mbaka sasa.
Pia wachezaji wao Haruna Niyonzima na John Bocco wameendelea kuongeza idadi ya mataji
wakiwa pia walishashinda taji hilo la Ligi Kuu wakiwa kwenye timu nyingine kabla ya kuhamia
Msimbazi. Kwa Haruna Niyonzima ni taji lake la tano ambapo alishinda matatu akiwa na Yanga
na hili ni la pili akiwa na Simba baada ya kutwaa la kwanza msimu uliopita. Kwa nahodha John
Bocco ni taji la tatu akiwa pia ameshinda moja akiwa na Azam FC msimu wa 2013/14.
Kinachoutia doa msimu huu wa Simba ni kuondolewa mapema kwenye michuano ya Kombe la
TFF. Kipigo cha 3 – 2 walichokipata dhidi ya Mashujaa inayoshiriki kwenye Ligi Daraja la kwanza
mwezi Disemba mwaka jana kinaweza kuitwa kipigo cha aibu unapolinganisha hadhi ya
mabingwa hawa wa Ligi Kuu na wababe wao hao kutoka Kigoma.
Swali linalosalia sasa kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Bara ni timu zipi zitaungana na African
Lyon kwenye kushuka daraja.