*Kaseke Jangwani, Mwalyanzi Msimbazi
Wakati Simba wakitafuta kocha na Yanga wakisubiri mwalimu wao, Hans De Van Pluijm kurudi kutoka likizo Ghana, klabu mbili hizi kubwa nchini zimeanza usajili.
Kama kawaida, nguvu za klabu mbili hizi zinaelekezwa zaidi katika wachezaji waliochipukia na kung’ara msimu uliopita, ambapo wachezaji hupewa donge nono wakati wa kusaini na kuahidiwa mishahara mizuri.
Simba wanaosema kwamba wanazingatia maelekezo ya ripoti ya kocha wao wa msimu uliomalizika, Goran Kapunovic wamefanikiwa kupata saini ya kiungo wa Mbeya City, Peter Mwalyanzi.
Yanga nao wamewabomoa Mbeya City kwa kumsajili winga machachari Deus Kaseke ikiwa ni kwa ajili ya kuziba pengo la Mrisho Ngasa aliyetimkia Afrika Kusini kucheza huko soka baadaya mkataba wake kumalizika. Inaelezwa kwamba wachezaji wote hao wawili wameanguka saini kwa mikataba ya miaka miwili kila mmoja.
Pluijm alisema kabla ya kuondoka kwamba angehitaji wachezaji mahiri na wenye nguvu na stamina kwa ajili ya kazi nzito iliyo mbele ya Yanga – kuwakilisha taifa kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.
Msimu huu Yanga wametolewa katika Kombe la Shirikisho na Etoile Du Sahel wa Tunisia baadaya kwenda sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 1-0 nchini Tunisia. Moja ya sifa za wachezaji wa Tunisia ni stamina, kuusoma mchezo lakini pia maumbo yao makubwa yaliyowanyima fursa Yanga.
Simba wamedhamiria kumaliza ukame wa ‘kupanda ndege’ wa miaka mitatu, ambapo hawajashiriki si Kombe la Shirikisho wala Klabu Bingwa Afrika, kutokana na kushindwa kupata nafasi mbili za juu.
Licha ya kubadilisha makocha ili kujiwekea mambo yao sawa, bado Simba wanaelekea hawajapata mwarobaini wa tatizo linalowakabili, na pengine usajili kwa ajili ya msimu ujao ukasaidia. Kapunovic alichukua nafasi ya Patrick Phiri aliyeanza ligi vibaya sawa na Marcio Maximo wa Yanga ambaye pia alifukuzwa.
Wakati Simba waliwawahi Yanga kwa kumsainisha mkataba mpya Said Ndemla aliyekuwa anatakiwa na wana Jangwani, Yanga nao inadaiwa kuwawekea mazingira mazuri wachezaji wake ili wabaki klabuni kwa muda mrefu na pia kumalizana na kiungo Haruna Niyonzima na beki Mbuyu Twite kwa kuwaongezea mkataba.
Wachezaji wengine ambao Yanga walikuwa wanawasaka ni pamoja na mabeki Mwinyi Mngwali wa KMKM ya Zanzibar na Salum Mbonde wa Mtibwa Sugar ambaye ni beki wa kati. Malimi Busungu wa Mgambo JKT yeye amezikataa klabu hizi kubwa na kuamua kwenda Mtibwa. Alikuwa anawaniwa pia na Azam, klabu inayojiamini kwa uhakika wa fedha na miundombinu ya soka.