Serikali imeziruhusu klabu za Simba na Yanga kuutumia Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi zao za Ligi Kuu ya Tanzania Bara, alimradi klabu hizo zitimize sharti la kutuma maombi yao mapema.
Chanzo kutoka katika kikao kilichofanyika jana baina ya Yanga, Simba, TFF na Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, kimesema kuwa klabu hizo na nyingine, zinaweza kuutumia uwanja huo kuanzia sasa ambapo Uwanja wa Uhuru waliozoea kuutumia kwa ajili ya mechi zao za Ligi Kuu umefungwa kwa muda ili ufanyiwe ukarabati.
Taarifa zaidi kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam jana, kuanzia saa 9:00 alasiri, zimedai vilevile kuwa suala tata la makato ya uwanjani hapo litapatiwa ufumbuzi katika kikao chao kingine kitakachofanyika keshokutwa Jumatatu.
Imeelezwa kuwa katika kikao hicho, Serikali imekuwa ikiwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Setti Kamuhanda.
“Kikao kilienda vizuri na inaelekea pande zote zitakubaliana na kumaliza tofauti zote zilizoibuka hivi karibuni,” chanzo hicho kilisema.
Wiki hii yote, klabu za Simba na Yanga zilikuwa zikilalamikia makato makubwa wanayokumbana nayo kila mara wanapocheza kwenye Uwanja wa Taifa na zilitishia kuachana nao na pia kutopokea mapato ya Sh. Milioni 33 pekee kwa kila moja, kutokana na Sh. Milioni 222 zilizopatikana katika mechi yao ya kuwania Ngao ya Jamii iliyopigwa Agosti 18 ambapo pesa nyingine nyingi zilidaiwa kulipia uwanja huo, kukatwa kodi na TRA na pia kutwaliwa na taasisi za BMT, TFF na IDFA.
Katika hatua nyingine, ilidaiwa awali kuwa, baada ya Serikali kuufunga Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya matengenezo, Simba walikuwa mbioni kuhamishia mechi zao kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na Yanga walitarajiwa kuutumia Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Klabu nyingine za Ligi Kuu zilizokuwa zikitumia Uwanja wa Uhuru, pia zilitangaza kuhamia viwanja vya mikoani, ikiwemo Azam FC iliyoripotiwa kwenda kuutumia Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.