Mechi ya marudiano ya watani jadi, Yanga na Simba, itafanyika Aprili 11 jijini Dar es Salaam badala ya Machi 14 kama ilivyokuwa awali, kwa mujibu wa ratiba mpya ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara iliyotolewa jana.
Katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyofanyika Oktoba 31 kwenye uwanja wa Taifa ambapo Simba ilikuwa mwenyeji, Yanga ililala 1-0 wakati Wekundi wa Msimbazi waliposhinda mechi yao ya 10 mfululizo katika ya 11 zote walizoshinda za mzunguko wa kwanza.
Hata hivyo, furaha ya Simba ilipotea Desemba 24 baada ya mahasimu wao Yanga kushinda 2-1 katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Tusker, hali ambayo imedaiwa kuwafanya wana Msimbazi kuchezesha timu ya vijana katika michuano ya Kombe la Mapinduzi ambayo inaendelea katika vituo viwili vya Zanzibar na Dar es Salaam.
Akitangaza ratiba mpya, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela, alisema kwamba mabadiliko yamezingatia ratiba ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika, Kombe la Shirikisho, mashindano ya kimataifa ambayo timu ya taifa, Taifa Stars na ya wanawake, Twiga Stars zitashiriki.
Mwakalebela alisema pia mabadiliko hayo yamezingatia maamuzi ya timu mbili za Zanzibar, Mafunzo na Miembeni kuchagua Uwanja wa Uhuru kama uwanja wake wa nyumbani katika mechi zake za kimataifa.
Hata hivyo, Mwakalebela alisema kuwa mzunguko wa pili wa ligi hiyo utaanza kufanyika Januari 16 kama ilivyotangazwa awali na kuzitaka timu zote kuendelea na maandalizi ya hatua hiyo ya lala-salama.
Mwakalebela alisema pia kutokana na mabadiliko hayo, sasa pazia la ligi kuu msimu wa mwaka 2009/ 2010 litafungwa Aprili 17 kwa timu zote 12 kuwa katika viwanja sita kukamilisha ratiba.
Aliongeza kuwa Januari 16 kwenye uwanja wa Uhuru Dar es Salaam, African Lyon inayoshika mkia katika msimamo wa ligi, itawakaribisha mabingwa watetezi, Yanga huku vinara wa ligi hiyo, Simba, wakiwakaribisha Majimaji kutoka mjini Songea katika siku inayofuata.
Simba ilifanikiwa kumaliza mzunguko wa kwanza kwa kujikusanyia jumla ya pointi 33 na kufanikiwa kuweka rekodi ya kushinda mechi zote 11 za mzunguko huo ikiwa chini ya kocha wake Mzambia, Patrick Phiri wakati Azam FC ilishika nafasi ya pili na Yanga ni ya tatu.