Menu
in

Simba watakumbuka uzoefu waliopata kwa Enyimba?

Simba SC

Vincent Enyeama ni jina linalokumbukwa na mashabiki wa soka nchini. Si kwamba wanamkumbuka kwa sababu alikipiga katika klabu ya Lille ya Ufaransa na kushiriki Ligi Kuu ya nchi hiyo, bali kama mwanasoka ambaye amewahi kukanyaga ardhi ya nchi hii kupambana na klabu ya Simba. 

Enyeama ni miongoni mwa makipa bora walioibuka mwanzoni mwa miaka 2000. Ni nyanda ambaye alikuja kuwakilisha kizazi kingine nchini Nigeria, baada ya kile cha akina Peter Rufai. Nigeria haikuwa nchi hodari ya kuzalisha makipa, lakini Vincent Enyeama aliibuka kuwa mlinda mlango hodari akiwakilisha klabu yake ya Enyimba. 

Katika soka klabu ya Enyimba inakumbukwa kuwa moja ya timu zilizowahi kuwa na utajiri lakini ikayeyuka katika ramani ya soka. kupepesuka huko ni kawaida, na huzitokea timu mbalimbali. mbali ya Enyima kuna timu kama Enugu Rangers ambayo nayo ni maarufu nchini. Sababu ya kufahamika Enyimba kuliko zingine ni namna klabu hiyo ilivyoihenyesha Simba. 

Mabingwa wa soka nchini Simba wameshakutana na Enyimba jijini Dar es salaam na huko Nigeria. Enyima ilikuwa hatari uwanjani, lakini mwanzoni haikuwa ikifahamika sana miongoni mwa watanzania. Baada ya kuchezea vichapo pamoja na kudindishiana kwenye kandanda ndipo wadau wakafahamu makali ya Enyimba. 

Tanzania Sports
PLATEAU UNITED

Kwa msingi huo Nigeria imewahi kutoa uzoefu wa kisoka kwa klabu ya Simba. Hata timu ya taifa tumekutana nayo mara kadhaa, kuanzia Super Eagles au timu za taifa za vijana. Ngazi ya Klabu na timu za Taifa zote zimekuwa na mchango kwa soka la Tanzania na vilabu vyake ili kufahamu namna ya kukabiliana nazo kila wanapokutana. Simba haijaanza leo kupambana na timu za Nigeria, lakini mechi zao na Enyimba ndizo zilikuwa za kusisimua zaidi.  Simba na Taifa Stars wote wanafahamu kasheshe za soka za Nigeria.

Ratiba ya shirikisho la soka barani Afrika CAF inaonesha kuwa mabingwa wa soka nchini Tanzania Simba watamenyana na Plateua United ya Nigeria. Mchezo wa kwanza baina ya miamba hiyo itahcezwa baadaye mwezi huu yaani Novemba 27 hadi 29.  Mchezo wa marudio utapigwa Desemba 4 hadi 6. Hii ina maana Simba wamerudishwa Nigeria tena. 

Wamepelekwa kwenye nchi ya kandanda barani Afrika. Nchi iliyoshuhudia staa wake John Utaka na Julius Aghahowa wakitamba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutimkia Ulaya. Vilevile jina la Simba sio geni masikioni mwa mashabiki wa Nigeria. Wanaijua vizuri kwa historia yake imeanzia miaka 1970 kwenye kandadna barani Afrika.

SIMBA KWENDA MSUMBIJI AU ZIMBABWE?

Mchezo wa Simba dhidi ya Plateua United unaanzia Nigeria, kisha wekundu hao wa Msimba watamalizia jijini Dar es salaam. Endapo Simba watafanikiwa kupenya hatua hiyo basi watakwenda nchini Msumbiji kumenyana na Costa do Sol ya Msumbiji. Ili kukutana na timu hiyo ya Msumbiji ni lazima waitoe Platinum ya Zimbabwe. Hivyo basi Simba wakifanikiwa watakuwa na mwelekeo wa kwenda Msumbiji ama Zimbabwe. 

PLATEUA UNITED WANA SIFA GANI?

Taarifa mbalimbali zinaeleza kuwa klabu hiyo ilitangazwa kuwa mabingwa wa soka Nigeria kwa sababu ya ugonjwa corona. Iliamuliwa kuwa timu inayoongoza Ligi ndiyo ikabidhiwe ubingwa wa Ligi Kuu Nigeria. 

Kwa sasa wanafundishwa na kocha Abdul Maikaba, ambaye bila shaka atataka kutumia uzoefu wa Enyimba kuitetemisha Simba miaka ya nyuma. Uzoefu wa Nigeria kuwa wababe mbele ya klabu na timu za taifa za Tanzania. sifa kubwa ya timu za Nigeria ni kutawala mchezo na kucheza kwa kasi. Hili lilikuwepo wakati wa Enyimba, na hata Plateua United watapita mulemule.

HISTORIA YA PLATEUA UNITED

Klabu ya Plateua United ilianzishwa mwaka 1975 ambapo kwa sasa inatumia uwanjanwa New Jos wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 40,000.  Timu hiyo imepata nafasi ya kuwakilisha Nigeria kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kukabidhiwa ubingwa mapema kutokana na mlipuko wa ugonjwa corona. Hii ina maana kama sio ugonjwa huo huenda habari ingekuwa nyingine kwa Plateua United.

WACHEZAJI TEGEMEO WA PLATEUA UNITED

Kila timu inakuwa na nyota wake anaotegemewa na ambao hutumika kuamua matokeo. Klabu hiyo inawategemea nyota wake kama vile Amoa Gyang,Tosin Omoyele, Bernard Ovoke, Chukwuweike Ibe, Benjamin Turban. Hao ndio wachezaji wanaotajwa kuwa hatari zaidi katika kikosi hicho. Kwa mfano mshambuliaji wao Tosin Omoyele aliwahi kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Atletico Madrid ya Hispania mwaka 2018. Pia wachezaji wengi waliopo katika kikosi cha Super Eagles wanacheza Ligi za ndani akiwemo Omoyele.

JE SIMBA WAMEJIFUNZA LOLOTE NIGERIA?

Mwaka 2005 Simba ilikutana kwa mara ya kwanza na timu ya Nigeria. Historia inaonesha kuwa Simba ilikutana na Enyimba kwa mara ya kwanza na ikaambulia vipigo katika michezo mitatu. Kwanza walikutana katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa ambapo Simba ilipata kipigo cha jumla ya mabao 5-1. Katika mchezo uliofanyikwa jijini Dar es salaam, Simba na Enyimba zilitoka sare 1-1 kabla ya kushishiwa kipigo kizito cha mabao 4-0 huko Nigeria. 

Mwaka 2003 Simba ilipambana na Enyimba katika makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Katika mchezo w a kwanza Simba ilichapwa mabao 3-0 huko Nigeria, kabla ya kushinda mabao 2-1 jijini Dar es salaam dhidi ya timu hiyo.

Mwaka 2008 timu hizo zilikutana katika hatua ya kwanza ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa ambapo ikiwa nchini Nigeria, Simba ilifungwa mabao 4-0. Katika mchezo wa marudiano Simba ilishuhudia ikizabwa tena mabao 3-1, hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 7-1.

Kimsingi Simba wanatakiwa kuwa waangalifu katika mechi zote mbili dhidi ya Plateau United. Tumeona mara kadhaa Simba ikipoteza mechi za ugenini kwa vipigo vikubwa, hivyo iwe ugeni wa Plateua au vinginevyo sio suala la kuipuuza. Kwenye mechi zao dhidi ya Enyimba pia ilikuwa timu ngeni lakini ikaleta madhara. Simba wanacheza mchezo mzuri sana na wanaweza kumaliza mchezo dhidi ya wapinzani wao mapema sana. Hata hivyo dhidi ya timu za Nigeria hawana rekodi nzuri. Ni wakati wa kujiandaa haswa.  

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version