Menu
in , , ,

SIMBA WAPENI RAHA MASHABIKI WENU.

Wekundu wa msimbazi timu ya Simba yeye maskani yake katikati ya jiji la Dar es salaam,kwa mara nyingine tena wamejikuta wakiwa na msimu mbaya kwenye ligi kuu ya Tanzania bara baada ya kumaliza msimu wakiwa na alama 38 na kuambulia nafasi ya nne huku waliendelea kukosa tena nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.

Klabu ya Simba ilianza msimu kwa kutumia Falsafa ya kutumia vijana zaidi ambapo kwa soka la kisasa walikuwa na nia njema tu.Walichokosea ni kutaka vijana hao kuwapa mafanikio ya haraka badala ya kuwapa muda.Moja kati ya viungo bora washambuliaji kwasasa Tanzania,huwezi kuliacha jina la Ramadhani Singano “Messi” na huyu ni matunda ya mfumo wa kuibua vijana ulioanzishwa na timu ya Simba.Simba ni lazima waendelee kuwekeza kwa vijana na kukiongezea nguvu kikosi chao cha kwanza.

Mgogoro wa viongozi nao umechangia kufanya vibaya kwa timu hiyo.Siku zote kukiwa na makundi kwenye timu,hamuwezi kusonga mbele.Nyumba inayogawanyika yenyewe,kamwe haiwezi kusimama.Ugomvi wa baba na mama siku zote anayeumia huwa ni mtoto na hapa ndipo unapokuja kugundua kuwa,waathirika wa ugomvi wa viongozi wa Simba ni mashabiki na wanachama.Hakuna kitu chochote shabiki wa soka anachonufaika na timu isipokuwa matokeo mazuri uwanjani.

Baada ya kumaliza mkataba wake wa muda mfupi,kipa Yaw Berko raia wa Ghana huenda akatimka klabuni hapo na tayari kuna majina matatu yametajwa kuziba nafasi yake.Hussein Sharif wa Mtibwa Sugar,Shaban Kado wa Coastal Union na Ally Mustafa wa Yanga huenda mmoja kati yao atajiunga na wekundu hao wa msimbazi.

Klabu ya simba nayo kama ilivyo kwa watani wao wa jadi timu ya Yanga,wanakabiliwa na zoezi la uchaguzi mkuu.Hapa ndipo mara kadhaa wanachama wamekuwa wakivurunda na kumchagua mtu kishabiki badala ya ueledi.Simba imeyumba sana na sasa ni muda wa kumpata mtu mwenye mawazo chanya na mtazamo wa mbali ili kuweza kuleta mabadiliko.

Mwenyekiti anayemaliza muda wake Ismail Aden Rage huenda ikaonekana kama hajafanya kubwa lolote lakini,wanasimba ni lazima wakafahamu kuwa hata kama angekuja Florentino Perez asingeweza kufanya kubwa lolote endapo angetumia mfumo huo wa msimbazi ambapo kila mtu anasajili mchezaji wake na anapopenda anauwezo wa kumuuza! Unaweza kumsema Rage kadiri ya uwezo wako na unahaki ya kufanya hivyo lakini,mfumo ni lazima ubadilishwe.

Kwa timu kubwa kama Simba yenye mashabiki lukuki ndani na nje ya mipaka ya nchi kukosa mashindano ya kimataifa mfululizo,ni kutowatendea haki wapenzi wenu.Ni muda wa kila mtu kutimiza wajibu wake ili Simba yenye ubora iweze kurejea.TanzaniaSports inawatakia mafanikio kuelekea zoezi kubwa la kupata viongozi wapya wa klabu.

51.556772-0.117842

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version