WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho walifungwa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza wa robo fainali dhidi ya Al Masr ya Misri. Si rahisi kuelezea mchezo huu ulivyokuwa na jinsi Simba walivyouweka mikononi mwao, lakini wakaruhusu mabao mawili ambayo hata hayaelezeki yaliinfiaje.
Hata hivyo mchezo wa soka una matokeo ya kikatili mno, na kwamba imba hawakupaswa kuondoka uwanjani wakiwa wamefungwa kutokana na kiwango chao walichokionesha uwanjani. Lilikuwa pambano ambalo unaweza kusema la upande mmoja, kwa sababuAl Masr walikuwa na mpango mmoja tu, kushambulia kwa kushtukiza na kujihami. TANZANIASPORTS inakuletea uchambuzi wa masuala muhimu katika mchezo huo ambao tathmini yake inaonesha Simba wana kila sababu ya kutwaa Kombe la Shirikisho msimu huu kutokana na uwezo wao wa kiuchezaji na ufundi.
Ufundi ndani ya boksi
Simba wana kila sababu ya kujiulaumu kwa kuchelewa kuipelekea moto Al Masr. Kipindi cha pili walicheza mpira mkubwa ambao ulikuwa na sababu zote za kuwapatia mabao. Katika mchezo w marudiano Simba wanatakiwa kuachana na tamaa ya kuingia kwenye boksi la Al Masr ndipo wafanikiwe kuwafunga. Katika mpangilio wa kimbinu Al Masr ni timu inayocheza mchezo wa kujihami. Wachezaji watano wa Al Masr walikuwa wanacheza kwenye mstari wao wa 18.
Katika kuzuia walianza na mabeki watano, kisha viungo wattu mbele yao, mshambuliaji mmoja mbele ya viungo na mwingine akicheza katikati ya mstari wa kiwanja (5-3-1-1). Katika mfumo huo wanapunguza ukubwa wa uhuru wa washambuliaji wa Simba kulisogelea lango lao. Ni sababu hii kila washambuliaji wa Simba walipoletewa pasi kwenye boksi walijikuta wanashindwa kufunga mabao sababu mabeki wa Al Masr walikuwa kama nyuki. Suluhisho la mfumo huo ni kuwaambia wachezaji wa Simba eneo la ushambuliaji kuhakikisha wnaapiga mashuti makali nje ya 18, bila kusubiri kusogelea ndani ya boksi.
Krosi wanazitegemea, wamejiandaa kuzuia
Al Masr wanategemea kuwa Simba wanashambuliaji hata kwa krosi. Katika ufundi wao kuna mabeki warefu kwenye eneo lao la ulinzi. Urefu huo unawapa nafasi ya kuondosha hatari zote za wapinzani wao. Ni mara chache krosi za Simba zilikuwa hatari, kwa sababu nyingi ziliondolewa na mabeki. Ili kukabiliana na rundo la mabeki kwenye boksi lao ni kuhakikisha benchi la ufundi linapanga wachezaji ambao watakuwa na kazi ya kuipanbgua safu ya ulinzi. Kwa mfano Elie Mpanzu anaweza kutumika kama mchezaji wa kupangua safu ya ulinzi ya Al Masr au Joshu Mutale na Kibu Dennis.
Mabadiliko ni kwamba Kibu Dennis kuanzia upande wa kushoto kisha Elie Mpanzu na Jean Ahoua wanakwenda kucheza nyuma ya mshambuliaji ikiwa na maana Elie Mpanzu anaweza kutokea kulia kuingia eneo la hatari na kusababisha madhara kwa wapinzani kwa sababu anao uwezo mzuri wa kutumia mguu wa kushoto. Hivyo basi Kibu Dennis mwenye matumizi makubw aya mguu wa kulia anakwenda kuichachafya ngome ya Al Masr kutokea kushoto huku Jean Ahoua akiwa kwenye eneo la nje kidogo ya 18 ili kupokea mapnde. Mbinu ilitumika mara kadhaa lakini haikuleta matokeo mazuri kwa sababu ya makosa madogo ya wachezaji wenyewe.
Eli Mpanzu acheze kwa ajili ya timu
Kila timu inakuwa na wachezaji ambao wanaibeba kutokana na uwezo wao mkubwa. Elie Mpanzu ni miongoni mwa silaha muhimu katika kikosi cha Simba lakini aambiwe uchezaji wake uwe unaihusisha timu nzima. Upo wakati alikuwa anaipasua vyema Al Masr lakini alichelewa kuwachezesha wachezaji wenzake na kujikuta akiporwa mipira ama mabeki kuondoa hatari. Ni mchezaji ambaye anatakiwa kukumbushwa ili mipango na mikimbio yake ifanikiwe lazima ahusishe timu.
Kwa mfano, anapokea pasi na kelekea eneo la hatari pembeni na kujikuta anakabiliwa na mabeki wawili au watatu wanaotaka kumzuia, lakini badala ya kubadilisha mbinu yeye anakwenda hivyo hivyo akitarajiwa kuwapita, hayo ni makosa yake binafsi si ya mwalimu. Timu inapomhitaji mchezaji kwenye matukio ya kuwapa ushindi, ni lazima atumie akili ya haraka kuona kama anawez akuwapta mabeki watatu kwa wakati mmoja ambao wanamlenga yeye.
Kulazimisha kuwapita kutokea pembeni kulisababisha mara kadhaa asiwe ‘effective’ kwenye kukamilisha shambulizi. Unachukua mpira unawakimbiza, kisha muono wako uwe unaangalia ikiwa nafasi ipo ama mbinu nyingine itumike. Kuzingirwa na mabeki watatu ambao wanafahamu hatari yako ni lazima winga au mshambuliaji ubadili mbinu kuelekea nje kidogo ya 18 ukitokea pembeni ama kushirikiana na viungo wako, namba 10 na nane ili watoe usaidizi wa maarifa kuwapita wapinzani. Elie Mpanzu aambiwe si jambo sahihi kulazimisha kila mipango kuamuliwa na yeye wakati anaweza kusaidiwa ni sawa na kucheza timu kwa ushirikiano.
Wapishane au waanze wote?
Hili ni swali kwa benchi la Ufundi la Simba. Je washambuliaji wao waanze wote kwenye mchezo mmoja au wapishane kwa dakika kadhaa? Leonel Ateba ni mshambuliaji mzuri na anao uwezo wa kutunza mali mguuni, kupiga mashuti na kufunga mabao. Katika mchezo dhidi ya Al Masr alizingirwa na mabeki wa timu hiyo kama nyuki. Kila alipojaribu kugeuka hatua moja alikuwa amebanwa na wachezaji wa Al Masr. Hii ilimfanya shindwe kufurukuta. Je katika mazingira hayo, Leonel Ateba na Steven Mukwala waanze kwenye mchezo mmoja au waendelea kupishana, mmoja anaanza na mwingine anaingia? Nadhani makocha wana kibarua cha kuamua hapa kwani ni wao wanaishi nao kila siku mazoezini.
Simba hawana kisingizo
Ingawaje wamepoteza mchezo wa kwanza, lakini Simba wana kila sababu ya kutwaa kombe hili. Sababu hakuna timu ambayo inaonekana kuitisha Simba kiuchezaji, kimbinu na maarifa ya wachezaji. Al Masr hawakuwa tishio kwa Simba, na mabao yao yamejieleza wazi kutokana na yalivyofungwa kwa makosa madogo hasa la bao la pili. Bao la kwanza ni suala la uwanja weneywe (pitch) ambapo hesabu za kipa zilikwenda vibaya hivyo ukadunda na kuingia wavuni. Narudia tena Simba hawana sababu yoyote ya kuwaambia Watanzania watashindwa kutwaa kombe hili. Uwezo wanao, nguvu wanazo, ufundi wanao, maarifa wanayo. Kombe la Shirikisho ni lao, washindwe wenyewe tu. Wanao uwezo wa kufunga mabao hadi matano (5) kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo wa marudiano.