MABINGWA wa soka Tanzania wametupwa nje kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa katika ubora wa aina yake kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika kusini. Ushindi wa mabao 3-0 ulishindwa kuikoa Simba kutinga hatua ya nusu fainali ua Ligi ya Mabingwa kutokana na kupoteza mchezo wa kwanza kwa mabao 4-0.
Vijana wa kocha Didier Gomes wakicheza kwa kujiamini, pasi fupi na kutawala mchezo kama wal9vyo kawaida yao waliliandama lango la Kaizer Chiefs tangu dakika ya kwanza ya mchezo huo na kutoa ishara kuwa walikuwa wamepania kutinga hatua ya nusu fainali na kuandika rekodi ya aina yake katika mchezo huo kwa Tanzania.
Hata hivyo Simba walilazimika kuchukua uamuzi mgumu wakati mchezo unaendelea baada ya kocha wa timu hiyo kufanya mabadiliko ya kumtoa kiungo wa ulinzi Muzamiru Yassing na nafasi yake kuchukuliwa na Bernard Morrison, huku ikikumbana na majeraha waliyopata nyota wake wawili wa kimataifa Taddeo Lwanga na Joash Onyango ambao waliumia kutokana na kugongana vichwa wakati wanawania mpira wa juu dhidi mshambuliaji wa Kaizer Chiefs Samir Nukovic. Nafasi za nyota hao zilichukuliwa na Erasto Nyoni na Kennedy Juma.
Iliwachukua dakika 22 za mchezo huo Simba kuandika bao la kuongoza kupitia kwa nahodha wake John Bocco kufuatia kazi nzuri ya kitimu kutengeneza shambulizi ambalo Kaizer Chiefs hawakuwa na uwezo wa kuzuia.
Bocco alipachika bao la pili kunako kipindi cha pili cha mchezo huo baada ya kazi nzuri ya Mohammed Hussein na Luis Miquissone upande wa winga wa kushoto. Kiungo mshambuliaji Cletous Chama alipachika bao la tatu katika dakika za lala salama na kuzidisha shinikizo kwa Kaizer Chiefs ambao walionekana kuzidiwa maarifa na uwezo wa Simba kutawala mchezo.
TanzaniaSports inamtathmini kocha wa Simba , Didie Gomes alipanga kikosi ambacho moja kwa moja alijipua kutaka kuishambulia Kaizer Chiefs kuanzia dakika ya kwanza hadi mwisho wa mchezo. Langoni alikuwepo Aishi Manula kama ilivyo kawaida kwa mabeki wa pembeni Shmari Kapombe na Mohammed Hussien kulia na kushoto. Katikati ya safu ulinzi ilinza na Joash Onyango na Pascal Wawa, wakati safu ya kiungo ilikuwa na majemedari Taddeo Lwanga na Muzamiru Yassin.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Gomes kumtoa Muzamiru Yassin yalikuwa ya kiufundi kwa sababu Kaizer Chiefs hawakuwa hatari langoni mwa Simba badala yake walicheza kwa kujihami muda wote wa mchezo.
Je Simba waliimarisha wapi?
Uamuzi wa benchi la ufundi unastahili pongezi kwenye mchezo wa leo dhidi ya Kaizer Chiefs. John Bocco alirejea kikosi cha kwanza kuongoza safu ya ushambuliaji akisaidiwa na Chris Mugalu hali ambayo ilionesha wazi Kaizer Chiefs walishindwa kumdhibiti nyota huyo kutokana na kupachika mabao mawili.
Hili ni eneo ambalo Simba walifanikiwa kuwadhibiti Kaizer Chiefs kwa sababu walitakiwa kumchungua nahodha huyo pamoja na Chris Mugalu. Kocha Gmes alibadili mbinu zake baada ya kumweka benchi kiungo mshambuliaji Larry Bwalya na nafasi hiyo ikaenda kwa Bocco.
Silaha za pembeni
Simba bado wanatakiwa kujivunia mabeki wao wa pembeni Shomari Kapombe na Mohammed Hussein, ambao kwa namna moja au nyingi wanaifanya timu ishambulie zaidi kupitia nafasi zao kuliko katikati ya dimba. Luis Miquissone alionesha kuwa bado wamo na atatesa vigogo wa soka barani Afrika baada ya kupiga krosi maridadi iliyotua miguuni mwa John Bocco na kuzaa bao la pili la Simba. Ile kasi aliyokwenda nayo, anamna alivyomgeuza beki wa kulia wa kulia wa Kaizer Chiefs, Frosler alitumia maarifa ya hali ya juu.
Simba wametoa onyo
Kwa mujibu wa takwimu za Shirikisho la soka barani Afrika CAF, limesema Simba ndiyo timu pekee yenye rekodi ya kupindua matokeo ya kufungwa mchezo wa kwanza na kusonga mbele. Mwaka 1979 Simba walikubali kipigo cha mabao 4-0 jijini Dar es salaam kutoka kwa Mufurila Wanderers ya Zambia. Lakini katika mchezo wa marudiano Simba waliichapa Mufurila mabao 5-0 huko Zambia.
Mashabiki wa Kaizer Chiefs waliamini timu yao ingeweza kulinda ushindi kirahisi na isingeweza kufungwa mabao idadi kubwa ya mabao katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam. Lakini habari imekuwa tofauti kwamba Simba wameibuka na ushindi wa mabao 3-0 licha ya kutosonga mbele wametoa onyo kuwa wanaweza kuifunga tiu yoyote barani Afrika.
Hakuna timu iliyotoa salama kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa. Mabingwa watetezi Al Ahly walikung’ukutwa 1-0, AS Vita ilizabwa mabao 4-1, El Merreikh ilitandikwa mabao 3-0 na ikiwa na maana kuwa ni uwanja mgumu kwa vigogo wa soka barani Afrika.
Licha ya ushindi wa mabao 4-0 kocha Gavin Hunt hakutemea kuiona tishio kutoka kwa Simba, lakini baada ya kupiga bao la pili kocha huyo alilazimika kusimama na kuanza kutoa maelekezo kwa wachezaji wake.
Kicheko chake alichokionesha kwenye mchezo wa kwanza jijini Johannesburg kiliyeyuka kwenye dimbala Benjamin Mkapa Dar es salaam. Wakati akianza kuhofia mchezo huo akajukuta timu yake ikipigwa bao la tatu, ambalo lilimtoa jasho na kuzunguka zunguka kwa kiwewe kama kuku aliyekoswa koswa na rungu la kumuua ili awe kitoweo wakati wa Sikukuu.
Kocha Hunt alielekeza huku na huko kama mhubiri ambaye alitaka waumini wake wamwelewe, lakini ubao wa ulionesha hali mbaya ilikuwa inaendelea kwa vijana wake.
Hunt alilazimika kubadilisha wachezaji wa mbele na kuwaingia mabeki wapya watatu ili kuwazuia Simba. Bao la tatu lilipatikana huku hao mabeki wapya watatu wa Kaizer Chiefs wakiwa wameingia uwanjani kuilinda timu hiyo.
Na tuseme Kazier Chiefs licha ya ushindi wa mchezo wa kwanza nyumbani kwao wameonywa kuwa Dar es salaam ni uwanja mgumu ambao huwezi kutoa ukiwa umekenua meno.
Simba wamejitangazia himaya
Ni kweli wametupwa nje ya mashindano katika hatua ya robo fainali, lakini tayari vigogo wa soka barani Afrika wanafahamu msimu ujao 2021/2022 Simba watarudi tena kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa. Timu mbalimbali zimekuwa zikiitazama Simba kwa jicho la tatu miaka ya karibuni na bila shaka imeshabdilisha mawazo ya wengi kuwa labda ilikuwa inajaribisha.
Kandanda safi. Pasi fupi fupi na kutawala mchezo. Uchu wa ushindi na ushirikiano wao. Kasi na nidhamu yao kuepuka adhabu za waamuzi. Kwamba hawaogopi presha.
Hawaogopi ukubwa wa timu yoyote. Wapo tayari kubadilika kocha wao Gomes akiagiza mabadiliko ya kimbinu, Mugalu anaweza kushuka chini zaidi kuchukua mipira na kwenda mbele akibadilishana nafasi na John Bocco au Bocco anaweza kurudi hadi kwenye himaya ya viungo wao na kupokonya mpira na kuipa uhai timu yao.
Simba wapo tayari kurekebisha makosa yao, hicho ndicho walichokifanya kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Kaizer Chiefs na kutoa onyo kuwa uwanja wa Dar es salaam si sehemu salama kwa kigogo yeyote wa kandanda.
Hayo ni miongoni mwa mambo ambayo yanaiweka Simba katika daraja lingine na bila shaka wametangaza soka lao barani Afrika.