Shamrashamra zililipuka kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar Salaam kwa mashabiki wa Simba huku wachezaji wa timu hiyo wakimbeba kocha wao Milovan Cirkovic wakidhani kwamba tayari wametwaa ubingwa kufuatia ushindi wa 3-0 dhidi ya Moro United huku wakiamini taarifa zilizosambazwa kuwa Azam wameshikiliwa katika sare ya 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi.
Hata hivyo, furaha hiyo ya Simba iliondoka kufuatia taarifa sahihi zilizofuata kwamba mechi ya Azam haikumalizika bali ilivunjika katika dakika ya 88 kutokana na vurugu za wachezaji wa Mtibwa Sugar kupinga penalti iliyotolewa kwa wenyeji na refa Rashid Msangi wa kutoka Dodoma.
Azam, ambao kisheria ndio wanaotarajiwa kupewa pointi tatu za mechi ya jana, watakuwa na pointi 53 na wanaweza kufikisha pointi 59, kama walizizonazo Simba sasa, kama watashinda mechi zao mbili zilizobaki dhidi ya Toto African na Kagera Sugar.
Simba sasa watahitaji kupata angalau pointi moja katika mechi yao ya mwisho dhidi ya wapinzani wao wa jadi Yanga katika mechi ya kufunga msimu Mei 5 ili kuwa mabingwa kama Azam haitadondosha hata pointi moja katika mechi zake mbili zijazo.
Vurugu za jana, zilikuwa ni tukio la tatu katika siku za karibuni kutokea katika mechi zinazoihusisha timu tajiri ya Azam kutokana na timu pinzani kupinga maamuzi ya refa.
Machi 10, beki wa Yanga, Stephano Mwasika alimpiga ngumi refa Israel Nkongo wakati akipinga kutolewa kwa kadi nyekundu kwa kiungo wa timu hiyo ya ambayo imetema ubingwa wake msimu huu, Haruna Niyonzima, na Wanajangwani wakalala 3-1.
Yanga walitaka mechi hiyo, ambayo beki wao mwingine Nadir Haroub Cannavaro alitolewa kwa kadi nyekundu, irudiwe lakini rufaa yao ilidunda.
Katika mechi iliyopita ya Azam dhidi ya Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma iliyomalizika kwa wageni kushinda 1-0, refa Martin Saanya alipigwa na kujeruhiwa na mashabiki akituhumiwa kuwapendelea Azam. Aliokolewa na polisi.
Beki wa Polisi Dom, Bakari Omari alitolewa kwa kadi ya pili ya njano katika dakika ya 57 kabla ya Azam kupata bao pekee lililofungwa na beki Aggrey Morris dakika saba kabla ya mechi kumalizika.
Hata hivyo, video ya goli hilo la kona lililodaiwa kuwa ni kati ya vyanzo vya kushambuliwa kwa refa huyo, ilionyesha lilikuwa sahihi kwani kipa wa Polisi hakuchezewa madhambi bali aliteleza kabla ya Morris kufunga kwa kichwa.
Kwenye Uwanja wa Taifa jana, Simba walipata goli la kuongoza mapema katika dakika ya 11 kwa njia ya penalti iliyotolewa na refa Nathan Lazaro wa Kilimanjaro baada ya beki Hilal Bingwa wa Moro United kuunawa mpira wakati akijaribu kuokoa na Patrick Mafisango kufunga ‘tuta’ hilo.
Haruna Moshi ‘Boban’ alipatia Simba goli la pili katika dakika ya 34 akimalizia pasi safi ya Uhuru Selemani na Felix Sunzu akapachika la tatu katika dakika ya 74 akitumia pasi ya Emmanuel Okwi.
Wakati huo huo, Simba ilishindwa kumtambulisha kiungo Nizar Khalfan waliyetangaza kumsajili kutokana na sababu iliyotajwa kwamba nyota huyo wa aliyetemwa na klabu yake ya Philadelphia Union ya Marekani, anauguliwa.