Simba jana ilitolewa kwa mara ya pili katika Ligi ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kufungwa mabao 3-0 na Wydad Casablanca ya Morocco nchini Misri, lakini habari njema ni kuwa kipigo hicho kimewawezesha Wekundu wa Msimbazi kupata nafasi ya kuikabili DC Motema Pembe ya JK Kongo katika pambano la Kombe la Shirikisho, CAF, la klabu za Afrika.
Mchezo dhidi ya Casablanca ulikuwa maalum kwa ajili ya kupata timu itakayochukua nafasi ya TP Mazembe kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo. TP Mazembe ilizotoa timu zote mbili lakini ikaenguliwa na CAF baada ya kukatiwa rufaa na Simba.
Kwa mujibu wa habari kutoka Cairo, Misri, Wydad ilipata goli la kwanza katika dakika ya 87 kabla ya kuongeza mawili ya haraka haraka ndani ya dakika tano za majeruhi.
Kwa matokeo hayo Wydad inasonga mbele na kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Klabu Bingwa ambayo Simba ilikuwa ikiwania kufuzu kwa mara ya pili baada ya kutinga mwaka 2003.
Simba itaanza nyumbani katika mchezo wa hatua ya timu 16 bora dhidi ya Motema Pembe. Mechi nyingine za hatua hiyo zimeanza wiki-endi hii na marudiano ni wiki mbili zijazo.
Mshindi wa mechi kati ya Simba na Motema Pembe ataingia hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho.