Hata wadhamini ambao wanawadhamini Simba SC walipata nafasi kubwa ya kuonekana kutokana na Simba SC kuzungumziwa sana kwa kipindi cha wiki nzima.
Wiki mpya imeanza, wiki ambayo inatupa nafasi ya kuisahau wiki iliyopita. Kuna mengi yametokea wiki iliyopita lakini moja ya kitu kikubwa kilichotokea wiki iliyopita ni kuongelewa sana kwa Simba SC.
Kwa wiki iliyopita Simba SC ilijitengenezea mazingira ya kuzungumziwa sana. Tukumbuke Simba SC iliachana na aliyewahi kuwa kocha wao mkuu Sven Venderbroeck.
Sven Venderbroeck aliyewazesha Simba kufika kwenye hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika. Swali kubwa ambalo lilibaki kwenye vichwa vya watu wengi ni nani atakuja kuwa kocha mkuu wa Simba?
Simba SC walianza kutengeneza mazingira ya watu kuwa na kiu ya kutaka kujua kocha mpya wa Simba SC atakuwa nani? Kitu kizuri zaidi kwao walifanikiwa kuziba mianya ya utoaji wa habari.
Kiu hii ilizidishwa zaidi baada ya kuvuja habari ya baadhi ya makocha ambao wametuma maombi ya kuja kuifundisha Simba SC. Majina makubwa mawili yalitajwa kuwa ni moja ya makocha ambao wameomba kuifundisha Simba SC.
Louis Van Gaal kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Uholanzi, klabu ya Barcelona, Manchester United na vilabu vingine alihusishwa kwenye kuifundisha Simba SC. Ukiachana na Louis Van Gaal kocha mwingine mkubwa alihusishwa ni Sven Errickson.
Huyu aliwahi kuwa kocha wa zamani wa timu ya taifa ya England. Kuhusishwa kwa majina haya makubwa kuliipa Simba SC kuzungumziwa kwa kiasi kikubwa sana. Mitandao ya kijamii ilijaa mijadala kuhusiana na Simba SC.
Vyombo mbalimbali vya habari viliwapigia baadhi ya makocha kuhakikisha hizo taarifa. Watu wengi wakawa na matamanio makubwa ya kuona ni lini atatajwa kocha mkuu wa Simba SC na huyo kocha mkuu atakuwa nani?
Siku ya kwanza Simba kuitisha mkutano na waandishi wa habari, watu wengi walijua Simba SC inaenda kumtambulisha kocha mkuu lakini ikawa tofauti na matazamio ya watu wengi.
Simba SC ilitambulisha mashindano yao ya Simba Super Cup. Wakazidi kuweka hamu ndani ya mioyo ya watu kutaka kujua ni lini kocha mkuu atatangazwa.
Simba SC walifanikiwa kutengeneza mazingira bora ya wao kuzungumziwa kwa muda mwingi, hii ilikuwa ni faida kubwa sana kubwa sana kwao kama chapa (brand).
Hata wadhamini ambao wanawadhamini Simba SC walipata nafasi kubwa ya kuonekana kutokana na Simba SC kuzungumziwa sana kwa kipindi cha wiki nzima.
Jana walipomtangaza Didier Gomes Da Rosa kama kocha mkuu wao kiu iliisha. Iliisha wakati ambao wao wamenufaika kuzungumziwa sana, mitandao yao ya kijamii ikiwa imetembelewa sana.
Kama ambavyo Wasafi Classic Baby (WCB), lebo ya music hapa nchini inayoongozwa na Diamond Platnumz inavyoweza kuweka kiu kwa mashabiki wake na kufanya kujenga wafuasi wengi ndivo ilivyotokea kwa Simba ndani ya wiki iliyopita.