Afisa Habari wa mabingwa wa ligi kuu Tanzania Bara Simba SC Haji Manara, ameweka wazi kuwa msimu ujao watasajili wachezaji wanne katika kujiweka sawa na mashindano mbalimbali.
Manara ameongea hayo leo (Jumatano) baada ya kukabidhiwa ubingwa wa ligi mkoani Lindi wakati timu hiyo ilipocheza dhidi ya Namungo FC.
“Sisi tutasajili kufuata weledi tunataka kurekebisha kikosi chetu sio kama wengine, msimu ujao tutatangalia nafasi nne tu,”alisema.
Kitaalamu Manara amelenga kuangalia nafasi ambazo hazifanya vizuri wakati wanaelekea katika michuano ya kimataifa ya klabu bingwa Afrika itakayoanza mapema mwaka huu.
Manara hakusahau kurudia kauli yake kuwa Simba itachukua ubingwa mara 10 hivyo tayari wamechukua mara tatu zikisalia awamu saba.
“Tumechukua mara tatu katika zile kumi hivyo bado mara saba, tutawapa nafasi wengine mwaka 2027, ’ alisema.
Alipoulizwa juu ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya watani wa jadi Yanga wa nusu fainali ya michuano ya ‘Azam Sports Federation Cup’ (ASFC), alisema baada ya kurejea Dar es Salaam ndio wataanza kujiandaa na mchezo huo ambao upo kawaida kama michezo mingine.
“Niulize habari za ‘utopo’ baada ya kurejea Dar es Salaam, kwa sasa nashangilia ubingwa ambao tumekabidhiwa,”aliongeza
Simba ndio timu pekee kwa misimu ya hivi karibuni kuingia katika hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika ikiwa na kikosi kilichokuwa bora kabisa.
Endapo watafanya usajili kwa kulenga nafasi zilizoachwa wazi timu hiyo itakuwa bora na itafanya vizuri katika michuano ijayo.