Hakuna ubishi kuwa mashabiki wa soka la Tanzania wanao mchango wake kuwavutia vigogo wa CAF kuyafanya mashindano ya AFL kuzinduliwa jijini Dar es salaam.
KWA mara nyingine tena klabu ya soka ya Simba inadhihirisha kuwa wao ni vinara linapofika suala la mashindano ya Kimataifa. Simba wanaingia uwanjani wikiendi hii kupepetana na miamba ya soka Afrika, klabu ya Al Ahly ya Misri. Takwimu zipo wazi kuwa umahiri wake katika mashindano ya CAF kuwa Simba ni klabu yenye hehima kubwa na kivutio cha soka katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Simba wanaingia uwanjani katika hatua ya robo fainali ya mashindano mapya ya African Football League (AFL). Katika mashindano hayo zipo timu 8 zinazoshiriki, huku Simba ikijiwinda kuweka rekodi nyingine. TANZANIASPORTS katika tathmini yake, inafahamu kuwa baadhi ya nyota wa Kimataifa barani Afrika wanatamani kuichezea klabu ya Simba kutokana na ushiriki wake kwenye mashindano ya CAF.
Nyota mmoja aliyesajiliwa na timu ya Ligi Kuu Tanzania akitokea klabu ya Raja Casablanca ya Morocco ameiambia TANZANIASPORTS kuwa tangu akiwa nchini humo alikuwa akifuatilia Simba, na baadhi ya wachezaji wa kigeni katika klabu Raja walikuwa wakizungumzia wababe hao wa Tanzania.
Sifa kubwa aliyotaja nyota huyo wa kigeni ni ushiriki na mafanikio ya Simba kwenye mashindano ya CAF ambako ni jukwaa ambalo wachezaji wenye shauku ya kufanikiwa wanatamani kuichezea klabu hiyo. Akizungumzia mashindano mapya ya African Football League amesema ni muhimu kusubiri hadi mwisho kisha tathmini ya msingi wake kufanyika.
MILIONI 10 KILA BAO
Wakati Simba ikiwa tayari kupepetana na Al Ahly, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yupo tayari kununua kila bao litakalofungwa. Rais Samia amekuwa akitoa ahadi na kutekeleza ya kununua kila bao kwa dau lake, ambapo kuelekea mchezo wa AFL, Rais Samia ameweka dau la shilingi Milioni 10 kwa kila bao litakalofungwa na wachezaji wa Simba. Kama alivyofanya kwenye mashindano mengine, Rais Samia ameonesha hatanii na hivyo ameweka dau ambalo nyota wa Simba wanatarajiwa kuhamasika na kusaka mabao kwa udi na uvumba dhidi ya timu kali kutoka Misri.
NANI KUPACHIKA BAO LA KWANZA?
Wachezaji wa Simba wana nafasi kubwa ya kuandika rekodi ya kufunga bao la kwanza kwenye mashindano mapya ya AFL. Safu ya ushambuliaji ikiwa na nahodha John Boco, Moses Phiri, Jean Baleke, Onana na Kibu Dennis wanaingia katika mchuano wa kupachika bao la kwanza la mashindano na kuiweka Simba kuwa na rekodi ya aina yake barani Afrika.
VIPAJI MBELE YA WENGER
Nani asiyemfahamu Arsene Wenger au maarufu kama Profesa Wenger kocha wa zamani wa Arsenal na bingwa wa EPL? Mashabiki wana mkumbuka Arsene Wenger kama miongoni mwa makocha gwiji waliofanikiwa kuibua vipaji mbalimbali vya wanasoka. Lakini katika mchezo kati ya Simba na Al Ahly utawapa nafasi nyota wa Kitanzania kutandaza kandanda mbele ya gwiji wa kufundisha mpira wa miguu duniani.
CAF WANOGEWA NA MZUKA WA BONGO
Hakuna ubishi kuwa mashabiki wa soka la Tanzania wanao mchango wake kuwavutia vigogo wa CAF kuyafanya mashindano ya AFL kuzinduliwa jijini Dar es salaam. Ni dhahiri CAF wanatamani mzuka wa mashabiki wa Tanzania na namna wanavyojazana viwanjani kuziunga mkono timu zao. Si Simba wala Yanga, bali hata timu ya Taifa nayo inawavutia mashabiki wengi pamoja na zile za kigeni zinazoomba kutumia viwanja vya Tanzania vimevuna mashabiki mara kadhaa.
CAF wameiona Simba inavyotetemesha vigogo, kisha wakashuhudia mabingwa wa Tanzania Yanga walivyoshiriki msimu uliopita na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho mbele ya Rais wa CAF, Motsepe. Ule mzuka walionao mashabiki unawafanya viongozi na wachezaji wa kigeni kuona Tanzania kama sehemu ambayo ina ‘kichaa cha soka’ kama ilivyo Brazil. Pengine ufunguzi ungeweza kufanyika katika mataifa makubwa kisoka kama vile Afrika kusini, Morocco, Misri au Algeria na Tunisia lakini mzuka wa Bongo umewavutia wengi. Na Zaidi mzuka huo unamaanisha pesa. Soka la Tanzania linawapa pesa CAF, kamwe hawataliacha.
UHONDO WA TP MAZEMBE
Katika hatua nyingine ya kudhihirisha kuwa mzuka wa mashabiki wa Tanzania katika soka unawavutia wengi, klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nayo itatumia uwanja wa Benjamini Mkapa Jumapili itakapopepetana na Esparance ya Tunisia.
TP Mazembe wamechagua kutumia uwanja wa Benjamin Mkapa badala ya Lubumbashi kutokana na serikali ya huko kutoafikiana na uingizaji wa vifaa vya kampuni ya kigeni kurusha mashindano hayo moja kwa moja. Kwa maana hiyo mashabiki wa soka nchini Tanzania watakuwa na nafasi ya kuburudishwa na soka la vigogo toka Tunisia, Esperance.