Baada ya kushindwa kucheza Arsenal kwa miaka minne kutokana na tatizo la kibali cha kazi, Mbrazili Wellington Silva sasa njia ni nyeupe.
Silva (22) alisajiliwa na Arsenal kutoka Fluminense tangu 2011 lakini akashindwa kucheza kwa vile hakupewa kibali cha kazi kwa vile hakuwa na uzoefu mkubwa na anatoka nje ya Umoja wa Ulaya (EU).
Walichofanya Arsenal ni kumpeleka kwa mkopo katika klabu tano tofauti za Hispania (imo kwenye AU) na sasa baada ya miaka minne amepewa uraia na pasi ya kusafiria ya Hispania, hivyo kufuzu kucheza England.
Silva ambaye ni mshambuliaji, alieleza kufurahishwa kwake na hatua hiyo akisema mambo mazuri huenda taratibu. Anadhaniwa atakuwa kwenye mipango ya Arsene Wenger kuanzia mechi za kabla ya msimu.
Alipiga picha akionesha pasi yake ya kusafiria, ambapo kwa sasa anacheza Almeria
“Kitu kizuri huja taratibu lakini hufika huku kukiwa na kuridhika kwingi duniani,” anasema mshambuliaji huyo kupitia mtandao wa Twitter.
Huyu ataongeza idadi ya washambuliaji wa Arsenal, ambapo ataungana na akina Olivier Giroud, Danny Welbeck, Alexis Sanchez na wengineo.