Hakuna aliyefikiri kuwa Inter Milan wangeshinda mchezo wa ugenini dhidi ya majirani zao AC Milan. Hata hivyo Inter Milan imepita njia ngumu ikiwemo
MPIRA wa miguu una maajabu yake. Wakati maelfu ya mashabiki wakisubiri namna Nigeria ikitinga robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1998 ikaishia kutandikwa mabao 4-1 na Denmark. Hakuna aliyetarajia Denmark kuifunga Super Eagle. Hakuna aliyetarajia kuona Nigeria inashindwa kwa namna yoyote ile.
Filimbi ya mwisho pale nchini Ufaransa ilipopulizwa Nigeria ilikuwa imeloa. Tijjan Babangida alikuwa hoi, Finidi George hakutamanika. Petr Rufai alitota kabisa, si Sunday Oliseh wala Jay Jay Okocha. Wakati FC Porto ilipowatupa nje Man United kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa hakuna aliyetatajia.
Hali kadhalika hakuna aliyetarajia kama Liverpool wangechapwa kwenye fainali ya Europa League na Sevilla. Hivi ndivyo ulivyo mchezo wa soka ambapo hakuna aliyetarajia Inter Milan ya Simeone Inzaghi ingetinga fainali.
Hakuna aliyefikiri kuwa Inter Milan wangeshinda mchezo wa ugenini dhidi ya majirani zao AC Milan. Hata hivyo Inter Milan imepita njia ngumu ikiwemo mbele ya Bayern Munich na Barcelona pamoja na AC Milan. Timu hii imefika hapo ikiwa na silaha muhimu ambazo zinakwenda mbele ya Manchester City huku kukiwa na ishara zote ni kama vita ya Daudi na Goliati. Ni silaha gani hizo?
Uchu wa mabao
Inter Milan wanategemea washambuliaji wawili pacha mvuta sigara maarufu Edin Dzeko raia wa Serbia na Lautaro Martinez raia wa Argetina pamoja na Romelu Lukaku akiwa mshambuliaji wa tatu wa nyongeza kikosini mwenye uzoefu mkubwa. Washambuliaji hao wawili wa mwanzo wanacheza katika mfumo wa 4-42 ambao unawapa nafasi ya kugawana majukumu, mmoja kurudi nyuma kuwasaidia viungo katika eneo la katikati.
Kwa kuzingatia umahiri wao tazama mchezo wa kwanza wa nusu fainali. Ni washambuliaji wenye uzoefu na uwezo mkubwa wa kukaa na mpira miguu. Siri yao ya pili ni uwezo wa kupiga mashuti makali langoni mwa adui. Siri ya tatu ni kutumia mtindo wa purukushani kila mara na walinzi wa timu pinzani. Washambuliaji wa Inter Milan hawawapi nafasi ya kupumua mabeki wa timu pinzani, kitu ambacho kinatoa tishio zaidi. Je namna gani Man City watakabiliana na safu yenye uchu wa mabao ya Inter Milan? Hilo linasubiriwa kwa hamu.
Mchezo wa kasi na kuua mechi
Siri kubwa inayowapa ushindi Inter Milan katika michezo yao miwili dhidi ya AC Milan katika nusu fainali ni uwezo wao wa kucheza kwa kasi ndani ya dakika 15 na kuua mechi. Kwa kuzingatia lugha ya soka, kuua mechi ni hali ya timu kutafuta ushindi mapema na kuwavuruga wapinzani wao.
Inter Milan walitumia dakika za mwanzo za kipindi cha kwanza kuwachapa AC Milan mabao mawili ya haraka. Kasi iliyotumika kupata ushindi ule ilikuwa ya aina yake. Kutoka winga wa kulia na kushoto pamoja na washambuliaji wa kati, kasi yao hushangaza na kuwavuruga wapinzani. Kwa namna ambavyo uwezo wa kupiga mashuti ya mbali walionao Lautaro na Dzeko ni wazi kuwa shughuli ya kukabiliana na Man City itakuwa ya mapema sana. Kasi na kuvuruga mbinu za wapinzani kwa kuwafunga mabao mapema ni silaha ambayo inatumika zaidi na kikosi cha Inzaghi.
Kujihami na mashambulizi ya kushtukiza
Aina ya mchezo wa Inter Milan ya sasa haikunyimi nafasi ya kuatwala mchezo, lakini wanakupa wakati mgumu pale wanapojihami na kutumia mashambulizi ya kushtukiza. Lakini hayo hayawezi kukamilika bila uwezo wa washambuliaji wao walionao. Mshambuliaji wa tatu katika mbinu zao ni Romelu Lukaku ambaye anaweza kubaki mbele peke yake kwa mbinu ya washambuliaji watatu; kwamba Lautaro na Dzeko wanaweza kucheza nyuma ya Lukaku wakitokea wingi ya kushoto na kulia. Hii ina maana safu yao inao washambuliaji wenye uzoefu wa mifumo tofauti. Mbinu ya kujihami na kushambulia kwa kushtukiza mara nyingi hutumia pale wanapokuwa wameua mechi mapema zaidi.
Ukuta mgumu
Kama wajulikanavyo Wataliano wanakuwa na mnyororo mgumu katika safu ya ulinzi. Sifa yao kubwa ni mbinu chafu (dark arts) ambazo ndizo zimekuwa silaha miaka mingi iliyopita. Katika michezo yao ya nusu fainali hawajaruhusu bao lolote. Inter Milan walishinda 2-0 kisha wakaibuka na ushindi wa 1-0.
Wakati an City walitoka 1-1 na Real Madrid kisha wakaibuka na ushindi wa 4-0 sawa na 5-1 kwa ujumla. Hii ina maana safu ya ushambuliaji ya Man City inapachika mabao ya kutosha. Lakini Inter Milan si wa kubezwa hivyo lolote linawezekana kwa vile hawakuruhusu bao kugusa katika nyavu zao.
Ndio kusema Inter Milan wanaingia fainali wakiwa na ukuta mgumu. je wataweza kuizuia Man City kufunga mabao katika lango? Hilo ndilo linalosubiriwa na wengi, ikiwa Inter Milan itafanya maajabu kama ya Denmark, Porto, Sevilla na wengine katika mchezo wa soka. Bila shaka mashabiki watapata uhondo wa timu mbili zenye uchu na hasita ya kutwaa mataji.