Mabao ya Lionel Messi na Luis Suarez hayakuweza kutosha kuwapatia ushindi FC Barcelona kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Hispania wa jana Jumamosi dhidi ya Celta Vigo uliopigwa katika uwanja wa nyumbani wa FC Barcelona, Nou Camp. Maximiliano Gomes na Iago Aspas nao pia waliingia wavuni kwa upande wa kikosi cha mwalimu Juan Carlos Unzue na kuufanya mchezo huo kumalizika kwa sare ya 2-2.
Sare hiyo ilitoa nafasi kwa Zinedine Zidane na Real Madrid ya kupunguza pengo la alama 8 baina yao na vinara wa ligi FC Barcelona lililokuwepo kabla ya michezo ya jana. Masaa kadhaa baadae Real Madrid wakashindwa kuitumia nafasi hii baada ya kutoa sare ya bila mabao katika uwanja wa San Mames, dhidi ya wenyeji wao Athletic Bilbao wanaokamata nafasi ya 15 kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Hispania.
Ushindi kwa Real Madrid kwenye mchezo wa hapo jana ungepunguza pengo kati ya miamba hawa wawili kutoka alama 8 mbaka 6. Hili lingewapa matumaini makubwa Real Madrid ya kuwapiku FC Barcelona baada ya kuwa walishaachwa nyuma kwa alama 10 wiki kadhaa zilizopita. Cristiano Ronaldo na wenzie walishindwa kutumia nafasi hii.
Real Madrid tayari wameshapoteza michezo miwili mbaka sasa ambayo ni ule wa nyumbani waliopoteza kwa 1-0 dhidi ya Real Betis mwezi Septemba na ule wa ugenini waliopoteza dhidi ya Girona mwezi Oktoba. Ingawa timu hizi hazikutarajiwa kupata ushindi dhidi ya Real Madrid lakini kiuhalisia ni timu zilzizo kwenye kiwango kizuri msimu huu kwa kuwa zote hizi zipo ndani ya timu 10 za juu kwenye msimamo wa La Liga mbaka sasa.
Sare nne walizo nazo mabingwa hawa watetezi wamezipata dhidi ya Valencia, Levante, Atletico Madrid na Athletic Bilbao. Ukitazama vizuri hapa unagundua kuwa Real Madrid wanashindwa kupata ushindi dhidi ya timu zinazofanya vizuri msimu huu au zilizo kubwa kihistoria ndani ya soka la Hispamia kwa namna moja ama nyingine.
Michezo minne inayofuata ya Real Madrid kuelekea kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa La Liga ni dhidi ya timu ambazo zinatosha kumuogopesha mno Zinedine Zidane. Mchezo wa unaofuata ni dhidi ya Sevilla wanaokamata nafasi ya tano katika jedwali la Ligi Kuu ya Hispania utakaopigwa Jumamosi ya Desemba 9 ndani ya dimba la Santiago Bernabéu. Ni mchezo mgumu ambao unaweza kuwashuhudia Real Madrid wakidondosha alama zaidi.
Mchezo unaofuata baada ya huo ndio unaoogopesha zaidi. Ni dhidi ya vinara FC Barcelona utakaopigwa siku mbili kabla ya pilau la Christmas. Ingawa mchezo utakuwa mgumu kwa pande zote lakini ikumbukwe Real Madrid ingawa watakuwa nyumbani, wataingia uwanjani wakiwa kwenye presha zaidi kutokana na pengo kubwa la alama kati yao na mahasimu wao na pia na uwezekano wa kujikuta wakirudishwa nyuma zaidi ya wapinzani wao hao.
Safari ya kwenda Balaidos ndiyo itakayofuata kwa Real Madrid baada ya mchezo wa El Classico. Watavaana huko na wenyeji Celta Vigo Januari 7, 2018. Ingawa Celta si kati ya timu ambazo huwasumbua Real Madrid lakini huu hauwezi kuwa mchezo rahisi kwa vijana wa Zinedine Zidane kwa kuwa watakuwa wanacheza na timu ambayo imewazidi kwa idadi ya mabao mbaka sasa na ni kati ya timu 10 za juu ya msimamo wa La Liga. Zaidi ya hapo ni timu pekee iliyofanikiwa kuondoka na alama kutoka Nou Camp kwenye msimu huu wa La Liga mbaka sasa.
Wiki moja baadae Zinedine Zidane atakuwa na kibarua dhidi ya Villarreal ambao sasa wanakamata nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Hispania. Michezo hii minne ya La Liga inayofuata kwa upande wa Real Madrid inaweza kupoteza kabisa matumaini ya Real Madrid katika mbio za La Liga msimu huu. Siku mbaya zaidi zinakuja, Zinedine Zidane.