Msimu wa ligi kuu Tanzania bara mwaka 2023/2024 umeisha katika siku za hivi karibuni na klabu ya soka ya Yanga iliibuka kuwa bingwa wa ligi hiyo. klabu mashuhuri ya Mtibwa sugar inayotoka kitongoji cha Turiani mkoani Morogoro imeshuka daraja na kurudi katika Championship league ambayo zamani ilikuwa inafahamika kama ligi kuu daraja la kwanza. Klabu kadhaa zimeshaagana na wachezaji wao na baadhi zimeagana na makocha pamoja na benchi zima la ufundi. Katika maandalizi ya msimu mpya wa ligi kuu vilabu vipo kimya vinajipanga katika maandalizi. Kila klabu inajipanga kuhakikisha kwamba msimu ujao wanafanya vizuri katika maandalizi hayo. Vilabu vya Championship na first league kama vilivyo vya ligi kuu navyo vyatakiwa viwe na mabenchi ya ufundi ya nguvu kwa ajili ya kuleta ushindani kwenye ligi zao pamoja na kombe la Federation. Kwa muono wangu vilabu hivyo vinatakiwa viajiri makocha na benchi la ufundi lenye vigezo vifuatavyo:
Kuibua vipaji vipya vya wachezaji. Kocha ambaye anayeajiriwa na klabu anatakiwa awe na maono na jicho la kuona vipaji vipya miongoni mwa wachezaji wachanga. Kocha anatakiwa awe na sera ya kuinuawachezaji wachanga kwa sababu kibiashara kocha ambaye anainua wachezaji wapya wa ndani huwa katika kipindi cha mda mrefu hutengeneza faida kwa klabu kwani klabu inapojenga kikosi chake kwa kutumia wachezaji wa ndani basi huwa inapungiza gharama kubwa za usajili na pili hujiweka katika mazingira magumu siku za usoni wakija kuwauza hao wachezaji hususuani kama vipaji vilivyoibuliwa vikicheza vizuri.
Kocha Alex Ferguson hujisifia kwamba sehemu kubwa katika mafanikio yake kisoka na kuibua kundi la wachezaji ambalo liliitwa CLASS OF 92 katika klabu ya Manchester United kwani baada ya kufanya hivyo kundi lile lilicheza mda mrefu katika klabu hiyo na kuipa mafanikio makubwa klabu hiyo. CLASS OF 92 ilijumuisha wachezaji kama vile David Beckham, Garry Neville, Phil Neville, Nick Butt, Paul Scholes na Ryan Giggs. Kocha mwenye muono huo anaweza kujenga misingi ya maendeleo ya klabu kwa mda mrefu ujao.
Kusimamia mastaa wakacheza pamoja. Kocha Jose Mourinho huwa ana kawaida ya kujisifia sana na katika mojawapo ya mambo ambayo huwa anajisifia nayo ni pamoja na uwezo wake wa kufundisha wachezaji wenye daraja la kidunia (world class players). Huwa anasema kama kocha huwezi kufundisha wachezaji wa aina hiyo basi huyo sio kocha mkubwa. Kwa hali ya kawaida vilabu vya sasa hujitahidi katika kununua wachezaji wenye majina na historia kubwa ili viweze kujitanua kisoko na pia viweze kupata mafanikio. Tukiangalia kwa sasa ligi kuu ya soka Tanzania kila klabuinapambana kusajili wachezaji wakubwa na wenye uzoefu mkubwa. Kama kocha atapewa klabu halafu atakuwa hawezi kufundisha wachezaji wenye majina basi kocha huyo hafai kuwa anafundisha ligi kuu ya soka Tanzania bara kwani katika vilabu vyote kwa sasa vina wachezaji wa haiba ya ustaa. Katika usajili wa sasa hakuna klabu ambayo utasema kwamba haijasajili wachezaji wenye uzoefu vilabu vyote vina wachezaji wazoefu.
Kutibu wachezaji ambao wana matatizo ya kinidhamu. Kocha mahiri atakuwa anajua namna bora ya kushughulika na wachezaji wenye matatizo ya kinidhamu na kama hatakuwa na uwezo huo basi huyo sio kocha mahiri. Kikawaida inafahamika kwamba wanamichezo wengi wenye vipaji huwa wana kawaida ya kuwa na matatizo yakinidhamu hususani ujeuri na hiyo huwa inasababishwa mara nyingi na uzoefu wa awali wa maisha ambayo huwa wanapitia. Kocha anatakiwa awe na uwezo wa kuyatambua matatizo ya wachezaji na aweze kutambua mbinu nzuri ya kisaikolojia ya kuayapatia ufumbuzi. Wachezaji kwa ujumla huwa wanatokea katika mazingira ya namna tofauti ambayo huhitaji uyaweze kuyaelewa hayo mazingira ili uweze kupata ufumbuzi wa matatizo ambayo huweza kuwakumba hao wachezaji.
Mfano wachezaji wanaotokea katika mazingira magumu ya kimaisha huwa yanatofautiana na wachezaji ambao wanaotokea katika mazingira mepesi ya kimaisha. Alex Ferguson huwa katika mambo ambayo hayasahau kama kocha ni kwamba aliweza kumsajili mchezaji ambaye huko nyuma alipewa wasifu kwamba mchezaji huyo ni mtukutu na ameshindikana na akamsajili na kisha kupambana na kumtafutia tiba ya utukutu huo mchezaji huyo mpaka akakaa sawa na kuwa mchezaji mwenye kuleta faida kwa klabu. Mchezaji huyo ni Eric Cantona.
Ferguson huwa anasema kwamba kwa kila aliyemuulizia kuhusu wasifu wa Cantona alimpa sifa ambazo hazikuwa nzuri lakini yeye akaamua kuchukua maamuzi ya kumsajili kwa kujua kwamba kwa uwezo wa kucheza soka ambao aliokuwa nao Cantona alimuhitaji sana na alipomsajili alitumia mbinu kadhaa za kisaikolojia kumweka sawa ili aweze kucheza kwa kujituma kwa hali ya juu na alifanikiwa katika hilo.
Kuweza kuwabadilisha wachezaji kutoka kucheza nafasi moja na kucheza nafasi nyingine. Kocha yoyote mahiri anatakiwa awe na uwezo wa kumfanya mchezaji ajiamini na kucheza nafasi ambayo hajaizoea na kisha kufanya vizuri. Gareth Bale alipokuwa anacheza nafasi ya beki lakini aliposajiliwa klabu ya Tottenham Hotspur alibadilishwa na kuanza kuchezeshwa nafasi ya winga na akafanya vizuri. Kolo Toure aliposajiliwa kutoka Afrika na kwenda kucheza Arsenal alikuwa mshambuliaji lakini alipoenda klabu hiyo akabadilishwa na kupelekwa kuwa beki. Samuel Et’oo alipohamia klabu ya Inter Milan kutoka Barcelona alihamishwa nafasi aliyoizoea na kupelekwa nafasi nyingine na akacheza vizuri tu.