Shangwe Arsenal kufuzu Ulaya
Furaha ya mashabiki wa Arsenal imetimia, baada ya timu yao kufuzu kwenye hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Arsenal wamefuzu wakiwa na mchezo mmoja mkononi, baada ya kuwachapa mabingwa wa Ufaransa, Montpellier mabao 2-0.
Kicheko kikubwa zaidi Emirates kilitokana na kiungo wao mahiri aliyekuwa majeruhi kwa miezi 15, Jack Wilshere kupachika bao safi.
Kana kwamba hiyo haitoshi, mshambuliaji wa kushoto, Lucas Podolski aliendelea kuchanua, baada ya kufunga zuri kwa mkwaju mzito.
Podolski alikuwa amegongeana na mchezaji mwenzake aliyetua Emirates msimu huu, Olivier Giroud anayeanza kuizoea timu yake mpya.
Arsene Wenger anasema pamoja na kufuzu, wanataka kumaliza wakiwa nafasi ya kwanza kwenye kundi lao, inayoshikwa na Schalke wa Ujerumani, wakiwazidi Washika Bunduki wa London kwa pointi moja tu.
Ushindi wa Arsenal haukupatikana kirahisi, na katika kipindi chote cha kwanza walikuwa wakihaha kumiliki mpira na kujaribu kupanga mashambulizi.
Hawakufanikiwa kupata mabao hadi kipindi cha pili, na kusababisha washabiki waliojazana Emirates kulipuka kwa furaha, walipokuwa wakielekea kufuzu.
Licha ya Podolski akizoea kuzifumania nyavu, Wilshere anazoea misukosuko ya uwanjani huku Giroud akiachana na kigugumizi cha miguu alichoanza nacho.
Arsenal inaelekea kujengeka vizuri kadiri siku zinavyokwenda, ambapo ukuta wao ulikuwa imara chini ya nahodha Thomas Vermaelen, aliyeonekana kuwa fiti.
Ushindi wa Schalke dhidi ya Olympiacos uliwahakikishia Arsenal kuvuka, ambapo katika mechi ya mwisho na ya kutafuta heshima tu, Arsenal watawafuata Olympiacos nchini Ugiriki.
Timu nyingine ya England, Manchester United wameshasonga mbele tangu walipokuwa na mechi mbili mkononi, ambapo wiki hii wamepoteza mchezo kwa bao 1-0 mkononi mwa Galatasaray.
Mabingwa watetezi wa Ulaya, Chelsea wamebaki roho mkononi, kwani huenda wakaweka historia ya kuwa bingwa wa kwanza kutolewa katika hatua hizi.
Chelsea waliomtimua kocha wao, Roberto Di Matteo baada ya kuchakazwa mabao 3-0 na Juventus nchini Italia,wanatakiwa washinde mechi yao ya mwisho.
Pamoja na kutakiwa kuwafunga FC Nordsjaelland katika uwanja wa Stamford Bridge, wataomba Shakhtar Donetsk wawafunge Juventus ili kuwaepusha na fedheha.
Sare kati ya miamba hao wawili itakuwa imewaharibia mambo Chelsea walio chini ya kocha mpya, Rafael Benitez.
Mabingwa wa England, Manchester City wameshahitimisha safari yao kwenye mashindano haya makubwa.
City wanaofundishwa na Roberto Mancini, walitoka rasmi baada ya kwenda sare ya bao 1-1 na Real Madrid Jumatano hii.
Kocha Mancini anasema bado City hawajafikia kiwango cha kuwa washindani katika bara la Ulaya, kwani ndio kwanza wanaijenga timu yao.