*Alipinga na wa Man U kwenye mechi ile
*Wa Man U alitoa gari na mke, akaokoka
Mambo ya kupinga kwa mechi ambazo mpira unadunda na hakuna anayeweza kujua matokeo hadi dakika 90 zimalizike ni hatari.
Shabiki wa Arsenal sasa analia baada ya kupinga na mwenzake wa Manchester United katika mechi ile ya Jumapili iliyopita, kwamba The Gunners wangeshinda iwe isiwe.
Henry Dhabasani aliiweka mezani nyumba ya familia yake kwa Rashid Yiga wakati shabiki huyo wa Man U kwa upande wake alipinga kwa kuweka gari na mkewe ikiwa Manchester wangepoteza.
Washabiki hao wanatoka wilaya ya Iganga, mashariki mwa Uganda na walichukulia upingaji wao huo kiumakini hivyo kwamba walilifikisha suala kwa wazee wa kimila, ambapo washabiki walishuhudia utiaji saini huo.
Kipenga cha mwisho kilipopulizwa hapo Old Trafford, Dhabasani alizimia maana hakuamini kwamba timu yake pendwa imefunga bao 1-0 wakati ilitawala mchezo huo kwa ujumla na ilikuwa ikiongoza ligi.
Tambo zake kabla na wakati wa mechi ziligeuka kuwa simanzi tangu hapo na Jumatatu ilipofika nyumba ilichukuliwa na shabiki huyo wa Man U na kumwacha jamaa akiwa hana nyumba tena.
Mbaya zaidi ni kwamba jamaa wa Arsenal ana wake watatu na watoto watano na sasa wanalazimika kulala nje, na ndiyo matokeo ya ushabiki uliopitiliza katika Afrika ambapo kila mmoja hutaka kuonekana mbabe kana kwamba ndio viongozi wa klabu kubwa za Uingereza.
Mwaka 2009 shabiki wa Manchester United aliendesha kwa fujo basi lake na kuparamia washabiki wa Barcelona baada ya timu yake kufungwa 2-0 na Barca kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL). Aliua wanne na kujeruhi wengine 10.
Wiki kadhaa kabla, shabiki wa Arsenal nchini Kenya alijiua kwa kujinyonga baada ya kikosi hicho cha Arsene Wenger kufungwa katika hatua za UCL.
Mwaka jana, washabiki wa Liverpool mkoani Ruvuma walijichanga na kufanya sherehe kubwa kufurahia mwenendo uliokuwa unaridhisha wa timu yao katika mapinduzi mekundu, chini ya kocha Brendan Rodgers.