KUMSHINDA bingwa aliyeshindikana unahitaji uwezo,mbinu,nguvu na maarifa makubwa. Vilevile mabingwa walioshindikana wanapokutana shughuli inakuwa pevu, na kinachobakizwa ni mmoja mwenye bahati kuibuka mshindi.
Fainali ya Europa League iliyochezwa huko Budapest, kwenye uwanja mzuri, mkubwa na wenye hadhi ya aina yake ulishuhudiwa mchezo maridhawa na ambao wapenzi wa soka walikuwa na shauku kubwa ya kumwona mshindi aliyeshindikana kocha wa AS Roma Jose Mourinho akinyanyua kwapa dhidi ya mabingwa walioshindikana Sevilla.
Mourinho anazo rekodi za aina yake linapofika suala la mashindano ya Ulaya. Tukirudi nyuma alikuwa Henrik Larsson aliyefunga bao mwaka 2003 kwenye mashindano ya Ulaya dhidi ya timu ya Jose Mourinho. Larsson toka Sweden alikuwa mshambuliaji wa aina yake, ambaye kwa kiasi fulani alitibua rekodi ya Jose Mourinho kwenye mashindano ya Ulaya.
Mchezo wa fainali ya Europa League uliochezwa Mei 31 mwaka huu ulizikutanisha timu mbili zenye historia tofauti. Lakini vile ulikuwa mchezo uliokutanisha timu ya Sevilla dhidi ya Jose Mourinho.
Sevilla wamchukua kombe lao
Hii ni timu kutoka La Liga ambayo imekuwa mabingwa wa kombe hilo kwa nyakati tofauti. Sevilla imewahi kuzichapa timu kama Liverpool kwenye mchezo wa fainali miaka ya nyuma, na inayo rekodi ya kutwaa mara nne mfululizo. Kwahiyo Europa League ni kama mali ya Sevilla kila inaposhiriki.
Timu zinazokutana na Sevilla kwenye fainali zinakuwa na jinamizi hili ambalo linawaandama. Kwamba Sevilla wana kombe lao Europa League. Ni sawa na Real Madrid walivyo wababe kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwa mara nyingine tena Sevilla wamechukua kombe lao mbele ya bingwa aliyeshindikana.
Mourinho ameharibiwa kazi
Katika mashindano ya Ulaya Jose Mourinho anazo rekodi za aina yake. Akiwa kocha wa FC Porto alitwaa Europa League kisha msimu uliofuata akanyakua Ligi ya Mabingwa. Kabla ya kutwaa kombe hilo katika mchezo wa fainali alikutana na kocha aliyeshindikana, Sir Alwex Ferguson, lakini bao la kusawazisha la Benny McCarthy lilimpa nafasi ya kutoka sare 1-1 hivyo ushindi wake wa mchezo wa kwanza 2-1 ulimpa nafasi ya kusonga mbele.
ose Mourinho alihamia Inter Milan ya Italia, huko alikiongoza kikosi hicho kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mourinho akiwa na Manchester United alitinga fainali za Europa nako hakuremba zaidi ya kunyanyua kwapa. Mahali ambako hakuchukua taji la Ulaya ni Real Madrid, huko aliishia nusu fainali.
Kimsingi Jose Mourinho hajawahi kufungwa katika mchezo wa fainali ya mashindano ya Ulaya kabla ya kucheza na Sevilla. Kwahiyo Sevilla ndiyo timu ya kwanza kumfunga Jose Mourinho katika mchezo wa fainali. Msimu uliopita AS Roma ilitinga fainali ya Europa Conference League na ikatwaa taji hilo. Kwahiyo Mourino amepoteza fainali ya kwanza kwenye mashindano ya ulaya kwa mikwaju ya penati.
Utatanishi wa kifundi
Mourinho anafahamika kama kocha mkali na asiyependa mzaha. Lakini vile ni kocha ambaye amekuwa gwiji kuzipanga timu zake katika ulinzi na mfumo wake mara nyingi ni wa kujihami. Ingawaje fainali hii AS Roma kuna mara chache ilifunguka kwa kuanza kukabia juu kwa mfumo 4-3-3 lakini mara walipoondoka eneo la adui walijirundika nyuma na kuwapa wakati mgumu Sevilla.
Jose Mourinho alimchagua Mancini kuwa miongoni mwa wapigaji wa penati. Beki huyo alishajifunga bao ambalo liliwapa nafasi Sevilla kurudi mchezoni. Wataalamu wa saikolojia wanabainisha Mancini licha ya kuonesha kujiamini hakupaswa kuwa mchezaji wa kupiga penati.
Kati ya wachezaji waliokosa penati Mancini alikuwa miongoni mwao, huku akiwa amevalisha kitambaa cha unahodha badala ya Pellegrini aliyefanyiwa mabadiliko. Kiufundi Jose Mourinho alifanya utatanishi.
Mourinho analipenda soka la ‘undava’
Katika mchezo wa soka Real Madrid wanafahamika kwa mtindo wao mambo meusi, ambapo kwa lugha ya kiingereza tunaweza kusema ‘Dark arts’. Hizi ni mbinu za kihuni kuwadhibiti wapinzani, ambayo hata wapiga pasi na soka la burudani kama Manchester City hawakuwa nayo huko nyuma kabla ya msimu huu nao kuachana na “uungwana kupita kiasi”.
Mbinu hii hufanywa kwa kumshawishi mwamuzi kutoa upendeleo kwa timu yao. Kinachofanyika ni uhuni, uchokozi,kutafuta faulo,kujiangusha,vurugu za kimchezo,kumtia presha mwamuzi,kuzua ugomvi na hila mbalimbali.
Katika fainali ya Europa League kulijaa matukio ya namna hiyo, AS Roma walikuwa wakicheza kwa kila aina ya mbinu nyeusi na kuwavuruga Sevilla pamoja na kuwapotezea mwelekeo. Mbali ya hilo Jose Mourinho amebaki na mbinu zake za kujihami licha ya kuboresha wakati wa kukaba.
Namba 10
Ajabu zaidi Mourinho bado anatumia mbinu ya nambari kumi katika safu ya ushambuliaji. Paulo Dyabala ambaye alipachika bao la kuongoza la AS Roma ni kiungo nambari kumi, ambaye katika soka la kisasa wanazidi kupotea. Lakini Mourinho angali anatumia mbinu hii na amefika fainali kwa mchango wa Dyabala.
Sevilla wana DNA na Kombe
Wanajiamini kwenye fainali ya Europa League kuwa wao ndiyo watemi, wababe,wataalamu,mabingwa na kila aina ya neno lenye kuashiria mafanikio. Sevilla walimiliki mpira kwa ufasaha, lakini tatizo lao lilikuwa mbinu chafu na undava wa AS Roma ulichangia wavurugane au kushikana jezi mara kwa mara kwa nia ya kugombana au kushawishi mwamuzi awapendelee.
Katika fainali hiyo Sevilla walicheza mpira wao kama kawaida huku mshambuliaji wao toka Morocco, El Neysri akifanya majaribio kadhaa ya kupachika mabao. Katika Europa League, Sevilla wana DNA huko. Timu zitakuwa zinaihofia Sevilla kwa sababu ya historia yao, jambo ambalo litazivuruga nyingi. Njia pekee ya kuwanyima Sevilla kombe la Europa ni kuhakikisha hawafuzu hatua ya fainali.
Bono amerudia ya Kombe la dunia
Kwenye fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika mwaka 2022 huko nchini Qatar, mlinda mlango wa Morocco alitia fora. Morocco ilitinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022 kabla ya kutolewa na Ufaransa.
Huyu si mwingine ni Bounou (Bono) golikipa wa Sevilla. Katika hatua ya matuta, golikipa huyo anajulikana kwa umahiri kuokoa michomo. Bono amekuwa mwarabu anayetisha wapigaji wa penati na kumfanya awe miongoni mwa makipa kivutio. Hana papara, mcheshi na daima huonesha maelekezo kwa mpinzani wake anayetaka kupiga penati. Anasimama langoni, ananyosha mkono upande mmoja kama mbinu ya kumvuruga mpinzani. Ni golikipa ambaye hahitaji maelekezo mengi kwa sababu ana kipaji kikubwa cha kudaka.