KAMATI ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii imeitaka serikali iongeze bajeti kwa Chuo cha Maendeleo ya Michezo cha Malya mkoani humu ili kiweze kuboresha miundombinu yake na kutoa taaluma bora kwa walimu na makocha wa michezo nchini.
Kamati hiyo ilitoa ushauri huo mwisho wa wiki ilipofanya ziara ya siku moja katika chuo hicho kilichopo mkoani Mwanza.
Wajumbe wa kamati hiyo walikitembelea chuo hicho ili kujionea miundombinu yake na kutoa ushauri kwa serikali jinsi ya kukiboresha.
Katika majumuisho ya ziara yao, kamati hiyo chini ya kaimu mwenyekiti wake, Florence Kyendesya,
kamati hiyo ilimweleza Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera kuwa serikali inapaswa kukiangalia chuo hicho.
Wameshauri ijenge bwalo la chakula, ofisi ya
utawala, viwanja zaidi vya michezo vinavyoendana na hadhi ya chuo hicho.
Mjumbe wa kamati hiyo, Kapteni John Komba
alisema: “Serikali iangalie upya bajeti ya chuo hiki
kama kweli inataka kukiendeleza kwa kuimarisha bajeti yake kila mwaka ili kukikuza katika kiwango cha kimataifa.
Tukifanya hivyo, tutavutia watu wengi zaidi kuja
hapa na tutapata walimu wazuri watakaosaidia kuinua vipaji vya vijana wetu na wengine watakwenda nje na kuliletea taifa tija, alisema.
Aidha, wajumbe hao waliushauri uongozi wa chuo kuwa na mipango inayolenga katika kuinua vipaji vya vijana kwa kuwapatia mafunzo mazuri vijana wanaoletwa chuoni hapo.
Kwa mujibu wa wajumbe hao, chuo kinatakiwa kiandae mpango wa kuendeleza vijana kwa kuanzisha shule za msingi na sekondari zitakazochukua vijana wenye vipaji ili kuwawia rahisi kuibua vipaji kwa vya wanamichezo.
Kwa upande wake, Bendera aliwahakikishia wajumbe hao kuwa maoni yao serikali itayafanyia kazi na kuwa nia yake ni kukifanya Chuo cha Malya kuwa cha kisasa duniani katika siku zijazo.
Alisema: Nia ya serikali ni kuwa na chuo
cha kisasa hapa Malya kinachotoa mchango wa maendeleo ya michezo duniani.
Tumeanza na hivi sasa tunakamilisha ujenzi wa uwanja wa kisasa zaidi wa ndani katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati kwa gharama ya Shilingi 1,056,000,000 na kwamba tayari serikali imekamilisha ujenzi wa maktaba na kituo cha kompyuta.
Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kilichoanzishwa na serikali mwishoni mwa miaka ya 1990, ndicho chuo pekee cha michezo kusini mwa Jangwa la Sahara kinachotoa stashahada ya
ufundishaji michezo. Tangu kuanzishwa kwake kimekwishatoa wahitimu 62 katika kozi hiyo na jumla ya wahitimu 489 wa ngazi ya cheti.