Menu
in

Septemba ni mwezi mgumu kwa Yanga

Dar young africans

Dar young africans

MABINGWA mara 27 wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wanakabiliwa na kibarua kigumu cha ratiba yao katika mashindano mbalimbali mwezi huu wa Septemba.

Yanga ambao wametoka kuadhimisha Wiki ya Wananchi kwa kuchezea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa kigogo cha soka cha Zambia, ZANACO. Kinachochekesha zaidi bao la ushindi lilifungwa na mchezaji ambaye ameibuka kuwa maarufu na kipenzi cha washabiki wa kandanda nchini Tanzania, Kevin Kapumbu. Kupendwa kwake ni sababu ya jina lake tu.

TANZANIASPORTS imefanya uchambuzi wa kina juu ya raiba ya Yanga kwa mwezi Septemba, ambapo inakabiliwa na mechi ngumu kwa dakika 180 ngumu katika michuano ya kimataifa, kisha dakika 90 zingine katika mchezo wa wa ndani dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba.

YANGA vs RIVERS UNITED

Vijana wa mitaa ya Jangwani na Twiga nchini Tanzania,Yanga wanatarajiwa kupepeteana na Rivers United ya nchini Nigeria katika raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Kwa mujibu wa ratiba ya shirikisho la soka barani humu CAF, imeonesha kuwa Yanga wataanza nyumbani katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam kisha wataelekea nchini Nigeria kucheza mchezo wa marudiano ambao utatoa mwelekeo wao. Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Septemba 12 mwaka huu.

Mshindi atakayepatikana katika pambano la Yanga na Rivers United ataingia raundi ya pili ambako atapambana na mshindi wa mechi ya Fasil Kenema ya Ethiopia dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

Historia ya klabu ya Rivers United inaonesha kuwa ilianzishwa mnamo mwaka 2016 kutokana na muungano wa timu mbili za nchini humo, Dolphins na nyingine Sharks ambapo inatumia uwanja wa Yakubu Gowon uliopo jijini Port Harcourt.

Jina la Yakubu Gowon ni kubwa katika historia ya siasa za Nigeria. Ni miongoni mwa wanajeshi waliopata kuingia kwenye mfumo wa utawala mwishoni mwa karne ya 20 kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mara kwa mara yaliyotokea huko.

Rivers United, wao wanashiriki Ligi ya Mabingwa kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo mwaka 2017 na kutupwa mashindano na Al Merreikh ya Sudan.

KUWAKOSA DJUMA, AUCHO, MAYELE

Wakati Yanga wakiwa anaingia uwanjani umapili hii kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa hatua ya awali, watawakosa nyota wao watatu Khalid Aucho raia wa Uganda, na Djuma Shaban na Fiston Mayele raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Sababu za nyota hao kukosekana ni kuchelewa kwa hati za uhamisho wao kutoka klabu zao za zamani El Makkasa ya Misri akiyocheza Aucho na AS Vita ya Shaban Djuma na Union Maniema ya Fiston Mayele.

Kuwakosa nyota hao ni pigo kubwa kwa Yanga, kwa sababu walisajiliwa ili watumikie klabu hiyo katika mashindano ya kimataifa. Lakini sasa wanatakiwa kukubaliana na hali halisi kwa kuangalia namna bora ya kuvuka raundi ya kwanza katika mechi zote mbili bila nyota hao.

YANGA vs SIMBA

Baada ya kuvaana na Rivers United katika Ligi ya Mabingwa, Yanga itarejea katika uwanja wa Benjamin Mkapa kukabiliana na mahasimu wake Simba. Mchezo huo utachezwa Septemba 25 mwaka huu, ikiwa ni wiki moja baada ya Simba kuadhimisha Simba Day ambapo wameikaribisha klabu ya TP Mazembe kupimana nayo ubavu.

Yanga watamenyana na Simba katika mchezo wa Ngao ya Jamii ambayo ndiyo inafungua pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania.  Yanga watakuwa kwenye uchu wa kulipa kisasi baada ya kufungwa katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho TFF kwa bao 1-0 kwenye uwanja wa Ziwa Tanganyika mkoani Kigoma.

Kwa vyovyote vile mchezo wa vigogo hivi utakuwa wa kukata na shoka huku kila timu ikitaka kuonesha kuwa mbabe wa mwingine na usajili wake ni bora zaidi ya mwenzake.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version