• Boniface Wambura abaki afisa habari
KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imempitisha Selestin Mwesigwa kuwa katibu mkuu wake.
Mwesigwa alizaliwa 1970 na ana digrii ya Masuala ya Kimataifa toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, diploma ya mafunzo ya sheria na pia amepata kuhudhuria kozi mbalimbali za utawala zilizotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Dunia (FIFA).
Wasifu wake pia unaonyesha kwamba aliwahi kufanya kazi Plan International na kimichezo, mara ya mwisho alikuwa katibu mkuu wa klabu ya Yanga.
Taarifa iliyotolewa leo kufuatia kikao cha Desemba 22 na kusainiwa na Rais wa TFF, Jamal Malinzi pia imemtaja Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura kubakia kwenye nafasi yake.
Evodius Mtawala ni mkurugenzi wa vyama wanachama na masuala ya kisheria, Wakili Melchesedeck Lutema ni mwenyekiti wa uchaguzi, Wakili Julius Lugaziya ni mwenyekiti wa rufaa ya uchaguzi na Ahmed Mgoyi ataongoza kamati ndogo ya mpira wa ufukweni.
Idd Mshangama ameteuliwa kukaimu nafasi ya ukurugenzi wa mashindano kwani waliokuwa wameomba nafasi hiyo hadi Desemba 15 hawakuwa wamekidhi vigezo hivyo maombi mapya yanakaribishwa.
Nafasi ya ukurugenzi wa ufundi itakaimiwa na Salum Madadi wakati ukurugenzi wa fedha na utawala utakaimiwa na Danny Msangi.