Kocha wa Brazil, Luiz Felipe Scolari amedaiwa kuachia ngazi baada ya kutofikia matarajio ya washabiki wa soka.
Scolari (65) alikwama katika nusu fainali vibaya kwa kucharazwa na Ujerumani 7-1 na kisha kwenye kutafuta mshindi wa tatu kwa kufungwa na Uholanzi 3-0 na pia mfumo na kiwango cha timu havikuwafurahisha watu wa Brazil.
Kocha huyu anayeshutumiwa na baadhi ya watu kwamba haambiliki, ndiye aliwapatia Brazil kombe hili mwaka 2002 lakini sasa katika ardhi yao wamepata fadhaa kubwa, na kuweka rekodi mbaya kupata kuwekwa.
Mbali na kufungwa kwa mara ya kwanza mechi mbili mfululizo tangu 1940, Brazil wameweka rekodi kuwa timu ya kwanza kufungwa mabao saba kwenye nusu fainali, na pia kufungwa mabao 10 katika mechi mbili mfululizo.
Scolari alikuwa anaonekana kama vile angeendelea kuinoa timu hiyo lakini chama cha soka kinadaiwa kwamba kilishaonesha ishara kuwa hatakiwi tena. Hata hivyo, kujiuzulu kwake kulitarajiwa kungewekwa rasmi Jumatatu hii.
Alizomewa na washabiki kama walivyofanya kwa wachezaji kwenye mechi ya kutafuta mshindi wa tatu, lakini akasema kwamba hatima yake ingeamuliwa na chama cha soka na si vinginevyo.
Baada ya kuachana na Brazil 2002, alikwenda kufundisha Timu ya Taifa ya Ureno, kabla ya kuingia Chelsea, Bunyodkor ya Uzbekistan na Palmeiras ya Brazil kabla ya kurudi tena kwa Samba Boys 2012 na mwaka jana akafanikiwa kuwapa ubingwa wa Kombe la Mabara.
Tayari tetesi zimeanza kusambaa juu ya majina yanayotajwa na Brazil kwa ajili ya kuchukua nafasi hiyo, likiwamo la Kocha Mkuu wa Chelsea, Jose Mourinho, ambaye hata hivyo alipata kusema hiyo ni kazi ya wazee, kwa sababu ni ya vipindi vifupi mno katika mwaka.