Menu
in , , ,

SCHWENSTEIGER NA SCHNEIDERLIN SI SULUHISHO KAMILI

Klabu ya Manchester United imepiga hatua kubwa mno kwenye maandalizi yake kwa ajili ya msimu ujao. Hiyo ni baada ya kupata saini ya Bastian Schwensteiger kutoka Bayern Munich na ile ya Morgan Schneiderlin kutoka Southampton. Bastian, nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani mwenye umri wa miaka 30 ni kiungo mahiri aliyeisaidia klabu ya Bayern Munich kutwaa mataji mengi yakiwemo nane ya ligi ya Ujerumani na lile la klabu bingwa Ulaya 2012/13.

Pia alitoa mchango mkubwa Ujerumani ilipotwaa kombe la dunia 2014. Morgan Schneiderlin, mfaransa mwenye umri wa miaka 25 pia ni mchezaji wa kiwango cha juu kuweza kuwemo kwenye ‘first eleven’ ya kikosi cha Manchester United na kuwasugulisha benchi wakina Fellaini, Michael Carrick na viungo wengine wa United.

Hivyo naweza kusema Schweinsteiger na Scheirderlin ni suluhisho la matatizo Old Trafford. Hata hivyo hawatoshi. Manchester United ina kila sababu ya kufungua pochi zaidi kusajili mlinzi mmoja mahiri wa kati na mshambuliaji mmoja wa kiwango cha juu. Hii inatokana na ukweli kwamba kunahitajika ukuta wa kuaminika kuimarisha ulinzi ili kupunguza idadi ya mabao ya kufungwa. Pia safu kali ya ushambuliaji ili kuiongezea United mabao ya kutosha.

Katika msimu wa mwisho wa Sir Alex, 2012/13, United iliruhusu mabao 43 katika michezo 38 ya ligi kuu ya Uingereza. Hii ilikuwa ni ishara ya kuanza kulegalega kwa safu ya ulinzi ya United iliyoundwa na Rio Ferdinand na Nemanja Vidic kwani kwenye msimu wa nyuma yake, 2011/12 United iliruhusu mabao 33 tu kwenye ligi hiyo.

Msimu wa 2013/14 United chini ya David Moyes ikaruhusu tena idadi ya mabao 43 kwenye ligi kuu ya Uingereza. Hiyo si tu kwamba ilikuwa dalili ya kufeli kwa mbinu za Moyes aliyekuwa mrithi wa Sir Alex ila pia ilichangiwa na kushuka kwa kiwango kwa walinzi wa kati Vidic na Ferdinand. Ferdinand na Vidic wakaondoka.

Van Gaal akaichukua timu na akasajili wachezaji kadhaa akiwemo mlinzi Marcos Rojo akitokea Sporting Lisbon ya Ureno. Akabakia pia na walinzi wa kati kama Smalling, John Evans na Phil Jones. Katika msimu wake wa kwanza Van Gaal ameiwezesha United kupunguza idadi ya mabao ya kufungwa. Ikaruhusu mabao 37 tu katika msimu huo wa 2014/15 na kufanikiwa kurudi katika nne bora kwenye msimamo wa ligi ya Uingereza.

Hata hivyo ukuta wa United bado unalegalega. Bado hakujakuwa na walinzi wa kati wawili wa uhakika Old Trafford kama walivyokuwa Ferdinand na Vidic katika ubora wao. Si Smalling, Evans wala Phil Jones alionyesha kiwango cha kutosha katika nafasi hiyo ya mlinzi wa kati.

Marcos Rojo aliyesajiliwa na Van Gaal anayeweza kuwafanya wapenzi wa United iwasahau wakina Vidic. Hivyo huyu jamaa anahitaji pacha wake. Matts Hummels angefaa kuwa pacha wa Rojo. Ila mbio za United kumshusha mlinzi huyo Old Trafford zilishagonga ukuta baada ya mlinzi huyo kuongeza mkataba na klabu yake ya Dortmund. United kwa sasa inawania saini ya mlinzi wa kati wa Valencia Nicholas Otamendi.

Atakuwa pacha sahihi wa muargentina mwenzie Marcos Rojo kama United watafanikiwa kumsajii mchezaji huyo. Hapo ndipo idadi ya mabao ya kufungwa itapungua na hata kuwafikia na kuwapita Chelsea walioruhusu mabao 32 tu msimu uliopita wakitwaa ubingwa wa ligi hiyo ya England.

Kwenye safu ya ushambuliaji, Wayne Rooney pia anahitaji pacha wake. Anahitajika mshambuliaji anayelijua goli hasa ambapo atasimama mbele ya Wayne Rooney na kuhakikisha idadi ya mabao ya kufunga pia inaongezwa kwa kiasi kikubwa.

Katika msimu wa mwisho wa Sir Alex United ikitwaa ubingwa wa ligi ilifunga mabao 86 katika ligi kuu ya Uingereza huku Van Persie aliyetimkia Fenerbahce akifunga 26 kati ya hayo. Msimu uliofuata, 2013/14 mabao yakapungua na kufikia 64 kitu kilichopelekea United kushika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi.

Msimu uliopita, 2014/15 yalipungua tena na kufikia 62. Hiyo ni dalili kuwa safu ya ushambuliaji inahitaji mabadiliko. Sina shaka na Wayne Rooney kwani katika misimu ya karibuni amekuwa akichezeshwa kama kiungo zaidi na si katika nafasi ya mshambuliaji.

Nauona umuhimu wa mtu kama Edinson Cavani kusimama mbele ya nahodha Wayne Rooney. Hivyo United inatakiwa kutoa pia kiasi cha pesa kumpata mshambuliaji huyo wa PSG. Schneiderlin na Schweinsteiger bado si suluhisho kamili. Cavani na Otamendi pia wanahitajika Old Trafford.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version