Yanga wana pointi 37 za Ligi Kuu Tanzania Bara. Pointi zao zinawafanya waongoze Ligi baada ya kucheza mechi 15. Katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya Mwadui, walishinda mabao 5-0. Mshambuliaji mwingine wa Yanga Yacouba Sogne alipachika mabao mawili katika ushindi huo.
Huyu ni mshambuliaji ambaye alianza taratibu kuliko Michael Sarpong. Yacouba anacheza tofauti na Sarpong, pia ana uwezo mkubwa wa kuchezesha timu hata kama yeye hafungi, ni aina ya wachezaji ambao wanaifanya timu inufaike na kitu cha ziada kutoka kwake.
Sasa kwa upande wa Sarpong amekuwa mchezaji mwenye machachari mengi dimbani. Mabeki wa timu pinzani huwa zinamuwinda kila mechi anayopangwa. Ni mshambuliaji ambaye ambaye ananikumbusha mtindo wa Joseph Kaniki maarufu kama Golota.
Kaniki alikuwa na uwezo mkubwa wa kupiga mashuti lango la adui,matumizi ya nguvu na alikuwa hawezekaniki. Hata hivyo Joseph Kaniki hakuwa na kasi kama ilivyo kwa Michael Sarpong.
Ukizungumzia washambuliaji wenye nguvu na machachari kwa sasa jina la Michael Sarpong litakuwepo. Ana nguvu, mpambanaji na zaidi ni mshambuliaji ambaye anamfanya beki awe macho wakati wote. Mabeki wanatakiwa kuwa macho si kwa kuhofia kufungwa bao bali namna Sarpong anavyocheza na kuwa tishio kwa timu zao.
Michael Sarpong ni miongoni mwa washambuliaji waliosajiliwa msimu huu 2020/2021 akichukua nafasi ya David Molinga. Sarpong ana uzoefu wa Ligi za Afrika mashariki kwa vile amewahi kicheza soka nchini Rwanda. Katika ardhi ya Tanzania hii ni mara yake ya kwanza kucheza timu za hapa.
Ukitazama orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jina la Michael Sarpong halipo kati ya watano wa juu. Orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu watano inashikiliwa na John Bocco (Simba), Adam Adam(JKT Tanzania),Prince Dube (Azam),Cletous Chama(Simba)Meshack Ibrahim (Gwambina), Meddie Kagere (Simba), Michael Sarpong na Obrey
Chirwa(Azam). Wafungaji hawa ni wale ambao wana mabao zaidi ya manne.
Hii ina maana Michael Sarpong amefikisha mabao manne licha ya Ligi Kuu kufikisha mzunguko wa 15. Yanga wamecheza mechi 15 hadi sasa. Mshambuliaji wa kigeni kuishindwa kufurukuta mbele ya wazawa ni jambo linaloleta mjadala.
Orodha ya wafungaji wanaoongoza Ligi Kuu ni wazawa. Washambuliaji wa kigeni watatu Prince Dube,Middie Kagere na Obrey Chirwa wamepanya, pamoja na kiungo Cletous Chama. Yanga licha ya kuwa na washambuliaji wa kigeni bado hawajafurukuta kupachika mabao.
Michael Sarpong ndiye mshambuliaji kiongozi wa Yanga. Nafasi anayocheza ni kuhakikisha anapachika mabao ya kutosha ili kulinda namba yake kikosi cha kwanza na kuipa mabao ya kutosha Yanga kuelekea mbio za ubingwa. Middie Kagere na Obrey Chirwa wana mabao manne kila mmoja, ambayo hajafikiwa na Sarpong.
Wafungaji wenye mabao manne ndio wa chini zaidi, akiwemo Sarpong. Hapo ndipo linakuja swali, licha ya juhudi zake kuhakikisha timu inafunga mabao na kuibuka washindi kwanini wastani wa upachikaji wa mabao hauridhishi?
Je, itatosha pekee Sarpong kubaki Yanga kwa vile anashughulika sana kuhakikisha wanapata ushindi wakati katika mechi 15 amepfunga mabao manne tu? Hayo ni baadhi ya maswali ya kujiuliza nafasi ya ushambuliaji Yanga.
Ni wazi kuwa Michael Sarpong anatakiwa kujirekebisha haraka. Wakati anaanza kucheza Yanga kulikuwa na matumaini ila makubwa lakini kadiri siku zinavyoenda ndivyo anavyozidi kupotea huku wenzake wanaiva akiwemo Yacouba Sogne na Deus Kaseke.
Ujio wa Ntabanzokiza ni tishio na ujumbe kuwa uongozi wa Yanga hauridhishwi na kasi ya upachikaji wa mabao. Sarpong amekuwa akikosa muendelezo mzuri wa kupachika mabao. Mfano Mwadui FC imeruhusu kufungwa mabao 28 msimu, hali ambayo ingekuwa rahisi kwa
mshambuliaji huyo kutumia mechi hiyo kupachika mabao ya kutosha kwa vile ni rahisi. Ushindi wa mabao 5-0 wa Yanga unamaanisha Mwadui wameruhusu nyavu zao kutikisha mara 33 katika mechi 15 msimu huu. Unashindwaje kutamba na kupachika mabao ya kutosha mbele ya timu dhaifu kama Mwadui ?
Hapo ndipo linakuja suala la kuwekwa becnhi. Mchezaji wa nje anapokaa benchi ni hasara kubwa kwa timu na yeye binafsi. Sarpong alipaswa kutumia mechi ya Mwadui FC ndio kupiga mabao mengi hata kuibuka na ‘hat trick’, lakini haikuwa hivyo. Sarpong kama sio kufunga kwenye mchezo wa Mwadui basi alipaswa kutengeneza mabao matatu kwa wengine.
Sarpong ili aweze kung’ara inabidi kocha Cedric Kaze ampunguzie majukumu ya kuzunguka kutafuta mipira. Kazi ambayo anapaswa aifanye ni kucheza katika eneo lake la ushambuliaji. Mchezaji kama Ntabazonkiza anaweza kufanya kazi ambazo alikuwa anazifanya Sarpong basi itamsaidia kung’ara.
Kiufundi Sarpong sio mchezaji mbovu bali anashindwa kujua jukumu lake la kwanza ni lipi kama mshambuliaji kiongozi. Sina uhakika kama Yanga wataharakisha kumuondoa labda kama watampata mshambuliaji mwingine mfano Meddie Kagere.
Lakini marekebisho kwa Sarpong yanatakiwa kuwa pande zote; kwa mwalimu Cedric Kaze kumuongezea maarifa na kumchorea eneo analotakiwa kubaki, pili kumpa changamoto ya kupachika mabao ya kutosha angalau 20 kwa msimu huu. Nje ya hapo haitashangaza kuona Sarpong akiyakuta mabegi yake yakiwa uwanja wa ndege tayari kwa safari ya kurudi kwao Burkinabe.