*Zambia, Kongo hakuna mbabe
Siku ya pili ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) imemalizika kwa timu kwenda sare, wababe Tunisia wakibanwa na timu ndogo ya Visiwa vya Cape Verde huku Zambia wakienda sare na Kongo Kinshasa.
Cape Verde walifanikiwa kusawazisha bao na kuwazuia Tunisia kuondoka na pointi zote tatu kwenye mechi ya kundi B. Tunisia walifunga kupitia kwa Mohamed Ali Moncer, lakini likasawazishwa na Héldon Ramos.
Tunisia waliofuzu kwa mashindano haya kwa mara ya 12 mfululizo, walipata pigo kabla ya michuano hii kuanza, kutokana na kuumia kwa washambuliaji wao muhimu, Saber Khalifa na Fakhreddine Ben Youssef.
Hii ni sare ya tatu ya 1-1 katika mechi nne za mwanzo hivyo kwamba timu zote za kundi B zipo sawa.
Katika mechi nyingine, Given Singuluma wa Zambia aliwapa matumaini baada ya kufunga bao katika sekunde ya 62 ya mchezo dhidi ya Kongo Kinshasa, lakini mchezaji wa Crystal Palace walio Ligi Kuu ya England, Yannick Bolasie akawasawazishia Kongo baadaye.
Winga huyo wa Palace alikuwa tishio kwa Zambia karibu muda wote wa mchezo na Kongo walikosa mabao mengine kupitia kwake na kwa Dieumerci Mbokani. Mechi za Jumapili zilichezwa kwenye mji wa pembezoni wa Ebebeyin na kulikuwa na askari polisi wengi uwanjani.
Licha ya uwanja kuwa na uwezo wa kuchukua watazamani 5,000, washabiki wengi walifika wakiwa hawana tiketi na kutaka kuingia, ambapo polisi walifanya kazi ya ziada kuhakikisha hawasumbui.