*WADAU WALIA NA SARE
*STARS KAMBINI KESHO
KOCHA mkuu wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mart Nooij, amesema kwamba matokeo ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Msumbiji (Mambas) ambayo timu yake imeipata juzi siyo mabaya na anaamini wanaweza kusonga mbele na kutinga hatua ya makundi ya kuwania tiketi ya kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Akizungumza baada ya mechi hiyo, Nooij, alisema kuwa hajakata tamaa na anaamini timu yake pia itapata mabao katika mechi ya marudiano itakayofanyika Agosti 3 mwaka huu mjini Maputo.
Nooij alisema kuwa mechi iliyochezwa jana ilikuwa ni ya kwanza na mechi itakayoamua nani asonge mbele bado haijachezwa hivyo Taifa Stars ina nafasi ya kufanya vizuri pia.
Alisema kuwa timu yake haikucheza vizuri katika kipindi cha kwanza lakini baada ya kusawazisha bao la kwanza, wachezaji waliamka na kuanza kucheza kusaka ushindi.
“Refa ni refa na soka ni soka, baada ya Msumbiji kupata penalti, na kufunga, wachezaji wangu waliamka na kurejea mchezoni, sare sio mbaya kuliko kufungwa, bado tuna nafasi, tunafunga kila mechi, tulianza na ushindi wa 1-0 na tulipokwenda Harare (Zimbabwe) tulitoka 2-2”, alisema Nooij.
Kuhusiana na makosa ya mabeki wake katika mechi ya juzi, Nooij, alisema kwamba hawezi kumlaumu mchezaji yoyote katika mchezo huo na kuongeza kuwa kikosi hicho kinazidi kuimarika siku hadi siku.
“Beki kama Nyoni (Erasto) alicheza vizuri sana kipindi cha pili kuliko humo nyuma, bado tuko katika mashindano, tutapambana Maputo,” aliongeza.
Naye Kocha Mkuu wa Mambas, Joao Chissano, alisema katika mechi ya marudiano timu yake haitazubaa na itacheza kufa na kupona ili kusaka ushindi.
“Matokeo kwetu ni mazuri, hatutalala, ila bado Nooij, ana faida kwa sababu anaijua timu yetu kuliko mimi ninavyoijua Tanzania,” alisema Chissano.
Kocha huyo aliongeza kuwa Taifa Stars imewapa wakati mgumu kutokana na kuimarika tofauti na alivyokuwa anaifahamu.
WADAU WALIA NA SARE
Kocha wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa soka nchini, Kenny Mwaisabula, alisema kuwa matokeo ya sare si mazuri kwa Taifa Stars ambayo itamalizia ugenini.
Mwaisabula aliongeza kwamba wachezaji wanatakiwa kutumia nguvu ya ziada ili kupata ushindi ugenini na hatimaye waweze kusonga mbele katika mashindano hayo.
Naye Kocha na beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ alisema kuwa timu hiyo imejiweka katika nafasi finyu ya kusonga mbele.
“Katika soka lolote linaweza kutokea lakini mpaka sasa Mambas wana asilimia 99 ya kusonga mbele sisi (Tanzania) tuna asilimia moja…tuna kazi kubwa kuwaondoa tena afadhali 2-2 tungekuwa tumepata ugenini,” alisema Julio.
Aliongeza kuwa bado Tanzania tuna kiu ya mafanikio wakati kocha ni mpya na viongozi walioko madarakani ni wapya.
Alisema pia mpira unahitaji matayarisho ya vitendo na si matayarisho ya maneno.
STARS KAMBINI KESHO
Meneja wa Taifa Stars, Clemence Boniface, alisema jana kuwa wachezaji wa timu hiyo walipewa ruhusa ya kupumzika na kesho mchana watarejea kambini.
Boniface alisema kuwa baada ya kukutana kesho, ndiyo itajulikana kama wataenda kambini Tukuyu mkoani Mbeya au watabaki Dar es Salaam kuendelea na maandalizi ya mchezo huo wa marudiano.
“Tutakutana tena Jumatano, tutakula chakula cha mchana pamoja na programu inayofuata itajulikana hapo,” alisema meneja huyo.
Kiungo wa timu hiyo, Jonas Mkude, ambaye alikuwa majeruhi, amepona na kesho ataingia kambini na wenzake.