Wikiendi iliyopita tumeshuhudia washambuliaji wawili waking’ara kwa kupachika mabao ya ushindi kwa timu zao. Mbwana Samatta alikiongoza kikosi cha Fenerbahce kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya klabu ya Karagumruk.
Samata alipachika mabao hayo ikiwa ni mchezo wake wa kwanza katika Ligi Kuu Uturuki. Kocha wa klabu hiyo, Erol Bulut anaonekana kuwa na matumaini makubwa kwa Mtanzania huyo ambaye amejiunga timu hiyo akitokea Aston Villa.
Baada ya kumalizika dakika 90 za mchezo, Samatta aliviambia vyombo vya habari kuwa, ““Nina furaha kusaidia ushindi wa timu yangu kwa kufunga mabao mawili. Ninatamani mabao hayo yawe chachu ya kutwaa ubingwa kuliko kufunga mengine 100 bila kuchukua ubingwa msimu huu. Nitakuwa furaha kufunga mabao, lakini kwangu timu kufanya vizuri ni kitu muhimu zaidi,” alisema Samatta mara baada ya mchezo wao kumalizika.
Naye kocha Erol Bulut ameonekana kufurahishwa na umahiri wa Samatta hasa kutokana na kupachika mabao mawili ya ushindi katika mchezo wake wa kwanza. Hali hiyo inatajwa kuwa itamwongezea kujiamini na sasa huenda akapachika mabao mengi.
Kwa upande mwingine, mshambuliaji Ollie Watkins alikiongoza kikosi cha Aston Villa kuibuka na ushindi wa mabao 7-2 dhidi ya mabingwa watetezi Liverpool. Kwenyre mchezo huo uliofanyika Villa Park, Ollie alipachika mabao matatu na kutengeneza bao moja, Jack Grealish alitengeneza mabao matatu na kupachika mawili. McGinn alipacgika bao moja na kutengeneza moja. Hii ilikuwa taswira nzuri ya Ollie kwenye kikosi cha Aston Villa.
Wikiendi hiyo vigogo wa soka Liverpool na Manchester United vilichapwa kwa jumla ya mabao 13. Liverpool walizabwa mabao 7-2 na Aston Villa. Man United walikung’utwa mabao 6-1 na kikosi cha Jose Mourinho, Tottenham Hotspurs.
Jicho langu limewatazama washambuliaji wawili, Mtanzania Mbwana Samatta na Ollie Watkins. Samata ameanza Ligi Kuu Uturuki kwa kupachika mabao mawili wikiendi iliyopita. Wakati Ollie Watkins alipachika mabao matatu dhidi ya Liverpool. Kwenye mchezo wa huo Samatta amezidiwa goli moja kwenye mchezo mmoja tu.
Baada ya mechi nne za awali za EPL zipo rekodi za timu mbili tu hadi sasa ambazo hazijafungwa; Ni Aston Villa na Everton. Ushindi wa Aston Villa umerudisha kumbukumbu yay a Desemba mwaka 1976 ambapo kikosi cha Liverpool kilifungwa mabao 5-1 na wababe hao wa Villa Park. Baada ya kipigo hicho Liverpool ilifanikiwa kumaliza msimu ikiwa bingwa wa EPL na Ulaya.
BIASHARA YENYE FAIDA?
Mshambuliaji Ollie Watkins alijiunga na Aston Villa msimu huu kuchukua nafasi ya Mbwana Samatta aliyeuzwa kwenda kwa vigogo wa Uturuki, Fenerbahce ambao hadi anajiunga walikuwa wnashikilia nafasi ya nane katika msimamo wa Ligi hiyo.
Kufanya vizuri kwa Samatta na Ollie Watkins ni ushahidi kuwa biashara iliyofanyika ni yenye faida tu, aliyeuzwa anafanya vizuri, aliyenunuliwa kuchukua nafasi yake naye anafanya vizuri. Aliyenunuliwa anafanya vizuri. Aliyenunuliwa Aston Villa ameongeza morali kwenye timu sawa na Samatta aliyeongeza mabao Fenerbahce. Vigogo hao wa Uturuki wamesajili wachezaji takribani 8 ili kuimarisha kikosi chao akiwemo Samatta.
Dalili zinaonesha kuwa Aston Villa hawataki kurudia makosa. Kwamba huenda likawa jambo gumu sana kushuhudia Aston Villa inashuka daraja msimu huu.
Mechi nne walizocheza tangu kuanza msimu huu zimeonesha namna timu hiyo ilivyo na uchu wa kushinda kila dakika. Hasa timu hiyo inaonekana kuwa na ari zaidi na kama vile inataka kumalizana na mambo ya kunusurika kushuka daraja mapema. Kuwafunga mabingwa watetezi kunaibua ari na tiba kisaikolojia kwani inawapa wachezaji kujiamini.
Hata hivyo uzoefu unaonesha kuwa mechi za mwanzoni na mwishoni mwa msimu zinakuwa ngumu zaidi. hivyo katika mechi za awali ambapo nne zimechezwa, inawezakana ikawa ari ya mwanzo wa msimu lakini ikaleta taswira nyingine mwishoni.
Changamoto waliyonayo Aston Villa ni kulinda kiwango walichonacho sasa na mwishoni itathibitika nani ataibuka kuwa kinara kati ya Watkins na Samatta. Nje ya hapo inaonekana ni biashara nzuri kufanyika.