Menu
in , , , ,

SAMATTA AMEBAKIZA MASAA MATATU KUWA MFALME

 

Juzi Jumapili TP Mazembe waliwafunga Al-Merrikh kutoka Sudan mabao matatu kwa sifuri kwenye mchezo wa pili wa nusu fainali za michuano ya Klabu Bingwa Afrika. Mbwana Samatta aliweka wavuni mawili huku lingine likifungwa na Roger Assale kwenye mchezo uliopigwa jijini Lubumbashi.

Ushindi huo umekuja baada ya TP Mazembe kupoteza mchezo wa kwanza wa nusu fainali uliopigwa jijini Omdurman nchini Sudan Septemba 26 kwa matokeo ya 2-1. Hivyo matokeo ya ushindi wa 3-0 wa Jumapili unawapeleka fainali TP Mazembe kwa matokeo ya jumla ya 4-2.

Kwa mara ya kwanza Samatta anakwenda kucheza fainali ya Klabu Bingwa Afrika tangu alipojiunga na Mazembe mwaka 2011. Alifanikiwa kucheza nusu fainali kwenye michuano ya 2012 na ya mwaka jana 2014 ambapo timu yake hiyo ilienguliwa mara zote mbili na kushindwa kuionja fainali.

Samata ataiongoza Mazembe kwenye michezo miwili ya fainali itakayopigwa kati ya Oktoba 30 na Novemba 8 mwaka huu dhidi ya USM Alger ya Algeria ambapo mchezo wa kwanza utapigwa jijini Algiers nchini Algeria na wa pili jijini Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mbwana Samata amekuwa akionyesha uwezo mkubwa tangu alipojiunga na timu hiyo. Baadhi ya wachambuzi na washabiki wa soka mara kadhaa wamewahi kumtaja kijana huyo kama mfalme wa TP Mazembe.

Advertisement
Advertisement

Hii inatokana na mchango anaotoa kwenye timu hiyo kiasi cha kujizolea umaarufu na kupokea upendo mkubwa kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo wa jijini Lubumbashi na nchi nzima ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa sasa Samatta ni mchezaji muhimu na maarufu zaidi wa kikosi cha TP Mazembe kama alivyokuwa Tresor Mputu miaka kadhaa iliyopita. Mputu aliyekuwa nyota tegemeo na nahodha wa TP Mazembe alitoa mchango mkubwa timu hiyo ilipotwaa taji la michuano ya Klabu Bingwa Afrika mara mbili mfululizo mwaka 2009 na 2010.

Nahitaji kumuona Samatta akiisaidia Mazembe kutwaa taji hili kama alivyofanya Tresor Mputu ili nami niungane moja kwa moja na wanaomwita mfalme wa TP Mazembe. Kwa sasa nasita kumtawaza cheo hicho licha ya kiwango kikubwa anachokionyesha kwenye timu hiyo.

Hata hivyo muda aliobakiza kuufikia huo ufalme ninaousema si mrefu. Ni muda mfupi mno wa masaa matatu pekee. Natumaini baada ya hayo masaa matatu atakuwa ameshatwaa ufalme wa TP Mazembe na jiji zima la Lubumbashi.

Masaa matatu haya ni muda utakaotumika kuchezwa michezo miwili ya fainali dhidi ya USM Alger. Mchezo wa kwanza wa dakika tisini (saa moja na nusu) jijini Algiers kule Algeria na mchezo wa pili wa dakika tisini (saa moja na nusu) jijini Lubumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Tusubiri tuone kitakachotokea baada ya masaa haya matatu. Binafsi nina imani na matarajio makubwa ya kumuona Mbwana Samatta akiwa shujaa wa timu hiyo kwenye michezo hiyo miwili ya fainali. Mbaka sasa ameshaifungia Mazembe mabao sita kwenye michuano hii.

Anahitaji mabao mawili kutoka kwenye michezo miwili ya fainali ili aivuke idadi ya mabao saba ya Bakri Al-Madina wa Al-Merrikh na kutwaa kiatu cha mfungaji bora wa michuano hii. Hata hivyo kitu cha muhimu zaidi ni kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika kama alivyofanya Mputu na nyota wengine wakati wakiichezea timu hii. Hapo ndipo atakuwa ameupata ufalme wa TP Mazembe na jiji zima la Lubumbashi.

Written by Kassim

Exit mobile version