Chuck Blazer: Mtoboa siri wa FBI
Imebainika kwamba ofisa wa zamani wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Chuck Blazer alipewa dili na Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) kukusanya siri ndani ya shirikisho hilo juu ya mlungula na kuwapa FBI.
Mmarekani huyo aliyekuwa kwenye Kamati ya Utendaji ya Fifa, amewafanyia kazi FBI kwa miezi 18 baada ya mwenyewe kuwa majeruhi wa sakata hilo, ambapo anakiri kwamba kama ni mlungula alikula na wenzake kwa makubaliano.
Blazer, 70, alikubaliana na waendesha mashitaka wa Marekani kuwachotea siri hizo baada ya kukiri makosa ya rushwa, utakatishaji wa fedha pamoja na ukwepaji kodi. Taarifa za makubaliano hayo zimewekwa bayana na jaji aliyekubaliana na maombi ya kampuni tano zinazomiliki vyombo vya habari.
Waraka uliopatikana unadaiwa kuonesha kwamba Blazer alikuwa akifanya kazi hizo kwa siri tangu Desemba 2011 na amekuwa kwenye kamati ya Fifa tangu 1997 hadi 2013. Mwezi uliopita waendesha mashitaka wa Marekani waliwashitaki watu 14 kwa makosa ya wizi, udangayifu, utakatishaji fedha na ruswa, vitendo vinavyohusisha mamilioni ya dola, hujuma walizofanya katika kipindi cha miaka zaidi ya 24.
Watu saba kati ya watu hao 14 ni maofisa wa Fifa waliodakwa jijini Zurich wakati wakijiandaa kuhudhuria vikao vya utangulizi wa uchaguzi uliomrejesha Sepp Blatter kwenye kiti cha urais wa Fifa. Hata hivyo, ametangaza kwamba ataondoka kwani haungwi mkono na ulimwengu wote wa soka.
Waraka wenye kurasa 19 unaoonesha makubaliano ya ushirikiano baina ya Blazer na FBI unaonesha kwamba ulitiwa saini baada ya ofisa huyo kukiri makosa yake, ambapo tangu 2011 alikubaliana na Serikali ya Marekani kuifanya kazi hiyo.
Sehemu ya waraka huo inasema: “Mshitakiwa anakubaliana kuipa ofisi hii nyaraka zote na vitu vingine vinavyoonekana vinahitajika katika upelelezi huu … na atashiriki katika shughuli za siri kuendana na maelekezo mahsusi kutoka kwa mashirika yanayosimamia utekelezaji wa sheria.”
Hali hii inazidi kuonesha kwamba FBI watakuwa na taarifa nyingi na nyeti juu ya mlungula ulivyokuwa ukitembea ndani ya Fifa, ukihusisha pia nchi, mashirikisho mbalimbali ya soka na watu binafsi kutoka mataifa mbalimbali, na huenda makubwa zaidi yakabainika hivi karibuni.