Menu
in , , ,

SAKATA LA MLUNGULA FIFA

Urusi, Qatar kupoteza uenyeji Kombe la Dunia?

*Jack Warner alikwapua $mil 10

Sakata la mlungula ndani ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limeingia sura mpya huku ukijitokeza uwezekano wa Urusi na Qatar kupoteza uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2018 na 2022 kwa mtiririko huo.

Vielelezo kadhaa vinaendelea kutolewa siku baada ya siku na sasa ofisa mwandamizi wa Fifa, Dominico Scala kutoa mwanga zaidi juu ya hatima ya suala hilo.

Scala ambaye ni mkuu wa kitengo cha Fifa cha ukaguzi na uratibu wa manunuzi anasema kwamba ikithibitika nchi yoyote kati ya hizo zilinunua kura kitakachofuata ni kufutwa kwa tuzo za uenyeji huo.

Hali hiyo inatokeza wakati aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Fifa, Jack Warner kutoka Shirikisho la Soka la Amerika Kaskazini, Kati na Caribbean (Concacaf) akiahidi kumwaga ukweli wote.

Ushahidi mwingine uliowasilishwa Marekani na mmoja wa washitakiwa 14 wanaosubiri hatima yao ni kwamba maofisa wa juu wa Fifa walikubaliana kupokea rushwa ili kutoa upendeleo kwa nchi, ikiwamo Afrika Kusini 2014.

Akizungumza na gazeti la Uswisi liitwalo ‘Sonntagszeitung’, Scalla alisema wanachosubiri ni ushahidi husika ili hatua stahiki zichukuliwe.

Anasema hayo huku Rais wa Fifa, Sepp Blatter akiwa ameamua kuachia ngazi muda mfupi ujao.

Maofisa hao saba wa Fifa walikamatwa kabla ya kuanza mkutano wa uchaguzi jijini Zurich, Uswisi ambapo pamoja na wengine saba nje ya Fifa, wanahusishwa na wizi, rushwa na utakatishaji fedha kwa kiwango kinachofikia pauni milioni 100.

Mamlaka za Marekani ndizo zinaendesha kesi ya awali wakati za Uswisi nazo zimefungua upya majuzi kuchunguza mchakato wa uenyeji wa fainali za 2018 na 2022 na zipo katika nafasi nzuri zaidi ya kupata ushahidi.

Blatter amekuwa madarakani tangu 1998 na alichaguliwa tena majuzi kwa kipindi kingine cha miaka minne lakini siku nne baada ya kuchaguliwa alitangaza atajiuzulu kwani haungwi mkono na wote kwenye ulimwengu wa soka.

Mwanasheria wa Marekani, Michael Garcia aliyeajiriwa na Fifa kuchunguza mchakato huo wa uenyeji wa 2018 na 2022 alitoa ripoti ambayo Fifa wanadaiwa kuichakachua kisha kudai hapakuwa na tatizo, hivyo Garcia akajiuzulu na huenda akaiweka hadharani ripoti yake.

Garcia alifanya kazi kwa miaka miwili na ripoti yake ina kurasa 430 lakini Fifa waliamua kutoa kwa ufupi wakijisafisha, ndipo Garcia akaeleza kwamba walichosema hakikuwa sahihi.

Katika tuko jingine, zipo habari kwamba dola milioni 10 zilizotolewa na Afrika Kusini kwenye akaunti za Fifa zilikuja kuishia mikononi mwa Warner au watu wake wa karibu.

Wakati Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) likiona kwamba ilikuwa rushwa kutoka Afrika Kusini kwenda Fifa kwa ajili ya kuisaidia ipate uenyeji wa fainali za 2010, Afrika Kusini inadai zilikuwa fedha za kusaidia kukuza soka kwa Waafrika walioko Caribbean.

Hata hivyo, ufuatizi wa fedha hizo unaonesha kwamba Warner aliyekuwa akidhibiti akaunti hizo alitoa fedha hizo taslimu, mikopo binafsi na kutakatisha fedha.

Warner (72) alijiuzulu uongozi Fifa kwa tuhuma za rushwa na baadaye nchini mwake aliachia ngazi kama waziri wa usalama na sasa anatakiwa nchini Marekani.

Ushahidi unaodaiwa kuonwa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) unaonesha kwamba Januari 4, Februari mosi na Machi 10, 2008 jumla ya pauni milioni 6.5 zilipokewa Concacaf.

Nyaraka zinaonesha kwamba mtandao wa maduka makubwa – JTA Supermarkets wa nchini Trinidad & Tobago ulipokea $4,860,000 kutoka kwenye akaunti hizo.
Fedha hizo zililipwa kwa awamu kati ya Januari 2008 na Machi 2009, kiwango kikubwa zaidi kikiwa ni $1,350,000 Februari 2008.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version