Menu
in , , , , ,

SAKATA LA KASHFA YA FIFA

England wahofia uchunguzi FBI

Chama cha Soka cha England (FA) kinaelekea kukwazwa na mwenendo wa uchunguzi unaofanywa dhidi ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwamba unaweza kuiweka nchi pabaya.

Moja ya maeneo wanayohofia ni juu ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Fifa, Jack Warner aliyepata kuwa na safari za Uingereza, ikiwa ni pamoja na kufika nyumbani kwa Prince Charles.

Msiri ndani ya FA anasema kwamba FBI wanaelekea kujielekeza kuchunguza dili hilo, kutokana na ukweli kwamba Warner amekuwa na uhusiano wa karibu sana na FA.

Warner ni mtuhumiwa mmojawapo kati ya 14 wa wizi wa fedha, rushwa na utakatishaji fedha na ameshafunguliwa mashitaka nchini Marekani, ambapo sasa anasubiriwa kusafirishwa kutoka Trinidad & Tobago.

Aprili 2000 Warner aliwasili England kuonana na rafiki zake katika FA na pia akapata ukarimu wa unaodaiwa kuhusishwa na uwezekano wa England kupewa nafasi ya kuandaa fainali za Kombe la Dunia 2006.

Huyu alikuwa na uwezo wa kushawishi wajumbe kutoka Amerika na Caribbean (Concacaf) kutoa kura tatu muhimu. Alipewa fadhila pia ya usafiri maalumu wa ndege hadi Manchester ambako United walikuwa wakicheza na Chelsea.

Baada ya mechi hiyo Old Trafford, Warner alipata ndege tena kurudi kusini mwa nchi ambapo alifanyiwa dhifa maalumu na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Utamaduni Habari na Michezo, Chris Smith.

Ni baada ya hapo FA walisema kwamba wangeandaa mpango wa kuendeleza soka huko Caribbean lakini haikuwekwa wazi mpango huo ungegharimu kiasi gani cha fedha.

Fadhila za FA ziliendelea, kwa chama hicho kuwafutia madeni rafiki wa Warner katika Chama cha Soka cha Jamaica waliokuwa wakidaiwa pauni 135,000.

Wakati FA ya England wakijiandaa kutafuta uenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2018 ilikuwa kawaida ya kumwandalia Warner chakula cha jioni na viburudisho vya zaidi ya pauni 55,000.

Ofisa mmoja wa FA amesema kwamba ana wasiwasi kwamba England wataumbuka kwani kwa hali ilivyo FBI watatua pia England.

Warner aliahidi kuweka wazi kila jambo linalohusu rushwa, hata kumhusu Rais wa Fifa anayeachia ngazi, Sepp Blatter, akisisitiza kwamba yeye si mla rushwa.

Hata hivyo, aliachia ngazi Fifa baada ya kutuhumiwa kujihusisha na rushwa na pia baadaye alijiuzulu uwaziri nchini mwake kutokana na mazingira ya rushwa kumzunguka.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version