Menu
in , , ,

SABABU ZINAZOLINDA KIBARUA CHA VAN GAAL

Tanzania Sports

Louis van Gaal ni mmoja wa makocha ambao kwa sasa hawaungwi mkono na mashabiki wa timu wanazofundisha. Mashabiki wamekuwa wakitamani kuona mholanzi huyo anatimuliwa.

Hii inatokana na kushindwa kukata kiu ya mashabiki wa mashetani wekundu. Kutolewa kwenye Ligi ya mabingwa Ulaya kwenye hatua ya makundi na kisha kuondolewa pia kwenye Ligi ya Europa na Liverpool wiki iliyopita kumemfanya azidi kupoteza sapoti ya mashabiki.
Hata mwenendo wa timu yake katika EPL si wa kuridhisha. Timu imekuwa haina muendelezo wa matokeo mazuri.

Washabiki hawaridhishwi na van Gaal. Ni wazi pia hata wamiliki wa timu hiyo wameshakata tamaa juu ya uwezekano wa kurejesha hadhi ya United chini ya LVG. Kwa nini hatimuliwi? Sababu hizi hapa.

Sababu ya kwanza ni kuirejesha klabu kwenye nne bora za EPL kwenye msimu uliopita uliokuwa msimu wake wa kwanza ndani ya Old Trafford. Hili ndilo lilikuwa lengo lake la msimu uliopita na akalitimiza.

Hayo yalikuwa ni mafanikio yaliyowapa imani mabosi na mashabiki wa timu hiyo kwa kuwa kwenye msimu kabla ya huo klabu ilimaliza kwenye nafasi ya saba.

Hivyo wamiliki wa timu wanapata imani kuwa ingawa hawana nafasi ya kutwaa ubingwa msimu huu lakini chini ya kocha huyo wanaweza kumaliza kwenye nafasi nne za juu na kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Sababu ya pili ni kwamba Giggs bado hajakomaa kuweza kuiongoza timu. Ikiwa van Gaal anatimuliwa basi Giggs ndiye anayepaswa kuingoza timu hiyo mbaka mwisho wa msimu kwa kuwa haitakuwa busara kumleta kocha mpya kwa sasa.

Inaonekana wazi kuwa wamiliki wa timu hawana imani na Ryan Giggs kwa sasa. Kutokuwa na imani na Giggs kunawalazimisha mabosi ya United kuwa na subira na kujijengea imani na Louis van Gaal.

Malipo ya zaidi ya paundi milioni 10 kwa ajili ya kuvunja mkataba na mholanzi huyo ambaye amebakiza takribani miezi 14 kwenye mkataba wake nayo ni sababu kubwa.

Paundi milioni 10 kwa ajili ya kuachana na van Gaal zinaonekana kuwa ni pesa nyingi ambazo wamiliki wa timu hiyo hawako tayari kuzitumia kwa sasa.

Sababu nyingine ni hadhi yake pamoja na urafiki wa karibu alio nao na Edd Woodward ambaye ni makamu mwenyekiti mtendaji wa klabu hiyo.

Inasemwa kuwa familia ya Glazer wanaomiliki klabu hiyo ya Old Trfford wana imani kubwa na Ed Woodward. Wanasikiliza ushauri na maamuzi yake hivyo ni rahisi kwake kumlinda mtu wake LVG.

Sababu ya tano ni kuwa mwisho wa msimu haupo mbali. Inaripotiwa kuwa kwa vyovote vile Louis van Gaal hawezi kubaki Old Trafford msimu ujao hata kama timu itamaliza kwenye nafasi nne za juu.

Vyanzo vinaarifu kuwa wamiliki wa klabu wanatazamia kuuvunja mkataba wake baada ya msimu kumalizika kisha mikoba ichukuliwe na mwalimu mwengine.

Uwepo wa Jurgen Klopp ndani ya Liverpool, Pep Guardiola atakayejiunga na Man City na tetesi zinazomhusisha Diego Simeone na Chelsea ndivyo vinavyowafanya United wasiwe tayari kuwa na van Gaal msimu ujao.

Kwa kuwa mwisho wa msimu upo karibu basi hawana haja ya kuharakisha. Msimu utakapomalizika miezi kadhaa ijayo mholanzi huyo atafungashiwa virago. Jose Mourinho ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba ya van Gaal.

Written by Kassim

Exit mobile version