Mshambuliaji na nahodha wa Manchester United, Wayne Rooney ameteuliwa kuwa nahodha wa Timu ya Taifa ya England.
Rooney (28) anachukua nafasi iliyoachwa na Nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard aliyejiuzulu soka ya kimataifa baada ya Three Lions kufanya vibaya kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Rooney ameshaichezea timu hiyo ya taifa mara 95 na kufunga mabao 40, na anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuteuliwa katika timu hiyo, Februari 2003, na alifunga bao katika mwaka wake wa kwanza na Three Lions dhidi ya Macedonia.
Kocha Roy Hodgson amesema alitafakari na kujadiliana kwa kirefu na Rooney juu ya nafasi yake hiyo mpya, na kwamba yupo tayari kukabiliana na shinikizo ambalo huja na nafasi kubwa kama hiyo.
Mchezaji wa zamani wa timu hiyo na Manchester United, Rio Ferdinand amesema Rooney ndiye alikuwa chaguo sahihi, maana hata wachezaji wengine wanamheshimu, wanampenda na wanamtegemea kwa mengi wanapokuwa uwanjani.
Rooney alisema anaona fahari kuwa nahodha, lakini alipata kuambiwa na Kocha wa Manchester United, Louis van Gaaal asigangamale sana na unahodha wa Man U bali ajihisi tu kana kwamba hana chochote, akitumia maneno; ‘let it fly’.
Alisema hivyo baada ya kumwona Rooney akiwa karibu muda wote wa mchezo akitaka kutoa maelekezo kwa wenzake, wakati mwingine akionesha kukasirika pale wanapokosea au kupoteza umiliki wa mpira.
Hodgson pia amewaita kikosini mwake wachezaji wapya wanne; mlinzi wa Arsenal Calum Chambers (19), Jack Colbak wa Newcastle, Danny Rose wa Newcastle na Fabian Delph wa Aston Villa, wote wakiwa na umri wa miaka 24.
England wanacheza na Norway kwenye Uwanja wa Wembley Jumatano ijayo katika mechi ya kirafiki kabla ya mechi za kufuzu kwa fainali za Euro 2016, wakianza na Uswisi Septemba 8.