Hatimaye kiu ya mabao kwa mshambuliaji wa kati wa Manchester United, Wayne Rooney imemalizika, pale alipofunga mabao matatu kwenye mechi ya kufuzu kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) dhidi ya Club Brugge.
Wakicheza ugenini baada ya kuwa wameshinda mechi ya kwanza nyumbani Old Trafford kwa 3-1, United wamefanikiwa kuvuka kigingi cha mechi za kufuzu, na sasa watasubiri ratiba kamili wajue watakwaana na akina nani, baada ya msimu uliopita kuyakosa mashindano hayo makubwa kwa klabu Ulaya.
Rooney alifunga mabao hayo katika dakika za 20, 49 na 57, akisaidiwa na akina Memphis Depay na Juan Mata kwa mawili ya mwisho, ambapo Herrera baadaye dakika ya 53 alifunga bao, United wakionekana wazi kwuazidi nguvu wenyeji.
Hata hivyo, Javier Hernandez ‘Chicharito’ atakuwa na huzuni kwa sababu alipewa fursa ya kupata bao kwa kupiga penati aliyoshindwa kuzamisha wavuni.
Rooney alionesha wazi kufarijika kupata bao la kwanza tangu Aprili mwaka huu alipofunga bao lake la mwisho.
Aliweka mikono usoni mwake, kabla ya kuzitazama mbingu na kusali kushukuru. Bao la mwisho alifunga dhidi ya Aston Villa, na tangu hapo amekuwa akishindwa kabisa kazi aliyokuwa ameizoea miaka iliyopita.
“Kusema ukweli kama nisingekuwa na nguvu ningeathiriwa sana na hali iliyonikuta huku watu wengi wakinichagiza. Hata hivyo sikuwa na wasiwasi kwa kukosa kufunga, nilijua mabao yatakuja tu na nilisema wazi. Fursa zimekuja na nimezitumia vizuri,” akasema Rooney baada ya hat-trick yake.
Kwa Herrera ilikuwa mechi ya kwanza msimu huu, ambapo zote zilizopita kocha Louis van Gaal alikuwa akimuacha kando na kuzua sintofahamu miongoni mwa washabiki. Kwenye mechi hii ya Jumatano, kocha aliwapumzisha Morgan Schneiderlin na Bastian Schweinsteiger.
Kiungo mchezeshaji Herrera alianza akicheza na yule mkabaji, Michael Carrick ambapo walianza pasipo kuchangamka, lakini kadiri mechi ilivyoendelea walikuwa vizuri na huenda akapata nafasi zaidi za kucheza.
Hata hivyo, Schweinsteiger na winga Ashley Young waliingia kipindi cha pili, ikionekana wazi kwamba siku zijazo kutakuwapo ushindani mkubwa kwenye eneo la kiungo katika kupata namba.
Van Gaal alisifu kikosi chake, akisema walijipanga vyema, wakacheza vyema wakiwa na mpira na pia kujipanga vilivyo wakati hawakuwa nao. Akasema kwamba kila bao linazidi kuwapa wachezaji hali ya kujiamini na kwamba kwa Rooney kufunga, amefurahishwa sana.
Kocha huyo ametangaza pia kwamba kuanzia sasa atakuwa akimchezesha Marouane Fellaini nafasi ya ushambuliaji badala ya kiungo. Uendelevu wa kuimarika kwa United utakuwa katika mtihani wikiendi hii, watakapocheza na Swansea ugenini katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu.