Menu
in , , , ,

Rooney aumia, kukosa mechi

Mshambuliaji tegemeo wa Manchester United, Wayne Rooney ameumia hivyo atakuwa nje kwenye mechi ya Jumamosi hii dhidi ya Newcastle huku ikiwa haijulikani kama atacheza kwenye marudiano na Bayern Munich wiki ijayo nchini Ujerumani.

Kocha wa United, Dabid Moyes anasema kwamba mchezaji huyo wa Timu ya Taifa ya England – Three Lions – aliumia kidole kwenye mechi ya robo fainali ya kwanza dhidi ya Bayern kwenye dimba la Old Trafford na ana wasiwasi kama atakuwa fiti kwa mechi ya marudiano.

“Wayne alipata mkwaruzo mbaya kwenye kidole chake usiku ule (walipocheza na Bayern). Jeraha ni kubwa na si kwamba litakuwa tatizo kwa mchezo huu tu, si ajabu hata kule Munich Jumatano hataweza kucheza kwa hiyo tunafuatilia akipata matibabu wikiendi yote hii tuone kama atapona haraka,” akasema Moyes.

Hilo ni pigo la pili kwa timu iliyo nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi, huku mpachika mabao bora wa misimu miwili iliyopita, Robin van Persie naye akiwa anauguza majeraha makubwa ya goti yanayoweza kumweka nje hadi mwisho wa msimu. Aliumia kwenye mechi dhidi ya Olympiakos ambamo alifunga mabao yote matatu yaliyowavusha United.

Moyes anasema kwa waliofuatilia vyema pambano dhidi ya Bayern, wangemwona Rooney akichechemea mwishoni mwa mchezo huo, akaongeza kwamba huwa maumivu ya vidole ni mabaya ambapo kuna wakati hulazimika kuchomwa sindano ili ucheze.

Katika mechi ya leo, United wanaweza kuwa na majeruhi walioanza mazoezi, Chris Smalling na Jonny Evans. Kuna wasiwasi juu ya uwezekano wa Rafael na Ryan Giggs kucheza lakini Alex Buttner yupo safi sawa na akina Juan Mata na Patrice Evra.

Newcastle bado wanasumbuliwa na majeruhi, ambapo Moussa Sissoko anaungana na wengine waliokuwa nje kwa muda mrefu baada ya kupata maumivu ya nyama za paja. Wengine walio nje ni kipa namba moja Tim Krul, mlinzi Mathieu Debuchy na mshambuliaji matata Loic Remy.
 

51.556688-0.117643

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version