Menu
in , ,

Ronaldo tumuelewe tu jamani amesoma alama za nyakati

Tanzania Sports

Moja kati ya uhamisho uliowashitua wengi katika kipindi hiki cha usajili barani Ulaya ni pamoja na usajili wa nahodha wa timu ya taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo kutoka Real Madrid kwenda Juventus kwa ada ya uhamisho wa euro milioni 100 (Zaidi ya Tsh bilioni 260) ambapo tunaambiwa itaongezeka euro milioni 12 katika kipindi cha miaka miwili baadaye, inawezekana wengi hawakuutarajia uhamisho huu au hawakuupenda kutokana na kuipenda Ligi ya Hispania LaLiga hususani ushindani wa Lionel Messi wa Barcelona na Ronaldo.

Vitu viwili vilivyokuwa vinawafanya watu wajiulize kwa nini Ronaldo kahama Real Madrid wakati angeweza kubaki Real Madrid na kufikia makubaliano ili alipwe mshahara mkubwa zaidi kama hitaji lake lilikuwa ni mshahara.

Wengine waliishi katika mawazo haya basi kama ameamua kuondoka kwani nini asingerudi Man United na kuamua kwenda Juventus? Ambapo atacheza Ligi ya Serie A ambayo kwa Afrika Mashariki hususani Tanzania kwa sasa inaaminika kuwa imepoteza mvuto ukilinganisha na miaka ya nyuma walipokuwa wanacheza Ricardo Kaka, David Beckham na hata Ronaldo De Lima akiwa na Inter Milan wakati huo.

Ronaldo amefanya maamuzi sahihi kwa wakati sahihi kwa lugha rahisi unaweza kusema amesoma alama za nyakati, mshahara anaolipwa Juventus wa euro milioni 30 kwa mwaka (Zaidi ya Tsh Bilioni 70), Real Madrid naamini wasingeshindwa kumpa kama wangekaa na kufanya makubaliano nao, ukilinganisha na umuhimu wa mchezaji huyo uwanjani na nje ya uwanja katika mauzo ya jezi.

Achilia mbali tetesi za kudaiwa kuwa hakuwa katika maelewano mazuri na Rais wa Real Madrid bwana Fiorentino Perez katika miezi ya hivi karibuni, ila Ronaldo amesoma alama za nyakati kwa kujiuliza swali rahisi sana, nabaki Real Madrid kufanya nini nikiwa nimeshinda kila kitu hapa? Ni wakati wa changamoto mpya.

Kwa wanaouliza kwa nini hakurudi Man United kama ilivyoripotiwa awali na kwenda kutafuta changamoto mpya katika Ligi ambayo imepoteza mvuto (Serie A), Man United ya sasa inafundishwa na Jose Mourinho ambaye licha ya kuwahi kufanya kazi pamoja na Ronaldo katika club ya Real Madrid (2010-2013), wareno hawa wanatajwa kutokuwa na uhusiano mzuri, hivyo ilikuwa ngumu kwa Ronaldo kwenda katika nyumba ambayo baba mwenye nyumba unajua kabisa sio rafiki na wewe, nafasi ya kucheza angepata kutokana na uwezo na jina lake lakini vipi maisha ya nje ya uwanja yangekuwaje?

Mshahara ndio unatajwa kumvuta Ronaldo katika klabu ya Juventus lakini kiukweli sio mshahara pekee unaweza kumfanya Ronaldo ajiunge na Juventus, kama ni mshahara pekee angeweza kwenda China au Marekani ambapo wanakimbilia wanasoka wengi wa ulaya kwenda kumaliza soka lao na kupata pensheni kwa malipo ya mishahara mikubwa wanayolipwa.

Ronaldo anaamini anaweza akang’aa katika klabu yoyote, Ronaldo anaamini katika miaka yake minne atakayokaa Juventus atashinda taji la Ligi ya Mabingwa kwa mara ya sita, wakati Man United ya sasa haipo katika wakati mzuri na inapitia changamoto ya kujiimarisha na kurudi katika level za enzi ya Sir Alex Ferguson.

Man United ya sasa inagombania kubakia TOP 4 wakati ya Ferguson mikakati ilikuwa ni Ubingwa, Man United ya sasa kocha analalamika kuhusu mtendaji mkuu wa klabu Ed Woord kutotimiza matakwa ya Jose Mourinho katika suala la usajili, Ronaldo anajiungaje na Man United ambayo haina uhakika wa kupambana na kufika walau nusu fainali ya Champions League kama robo fainali tu ni mtihani.

Huyu ndio Ronaldo tumuelewe tu jamani amesoma alama za nyakati miaka tisa aliyokaa Real Madrid na kutwa mataji manne ya Champions League, mataji ya mawili ya LaLiga, mataji mawili ya Copa de Rey, mataji mawili ya Spanish Super Cup, Ubingwa wa dunia wa ngazi ya club mara tatu na mataji mawili ya UEFA Super Cup, Ronaldo tumuelewe tu Man United hapakuwa mahali pake salama kurudi.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version