Dunia ilishuhudia Cristiano Ronaldo akivunja rekodi ya mmoja wa watu ambao waliutumikia mpira mpaka wakaacha alama kubwa katika uso huu wa dunia, Ferenc Puskas.
Mshambuliaji ambaye alikuwa rafiki wa nyavu na adui wa magolikipa wengi.
Kwake yeye kufunga ilikuwa jadi na Mungu alimleta kwa ajili ya kazi hiyo tu.
Alifanya kile ambacho Mungu alimtaka afanye. Ikawa rahisi kwake kuweka rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga magoli mengi ngazi ya timu ya taifa kwa ulaya.
Magoli 84 ndani ya michezo 85 ya timu ya taifa yalimfanya aweke alama ambayo ilidumu kwa muda mrefu mpaka pale Cristiano Ronaldo alipofunga goli la 85 katika michuano hii ya kombe la dunia na kuwa mfungaji bora wa wakati wote wa ulaya katika ngazi ya timu ya taifa.
Hii ni alama nyingine tena anaiweka baada ya kuivunja alama ya gwiji mwenzake wa Real Madrid. Gwiji ambaye alitajwa kama mshambuliaji bora wa karne ya 20. Ferenc Puskas ambaye alipewa heshima mwaka 2009 kwa kuwepo na tunzo yenye jina lake.
Tunzo ya goli bora la mwaka. Hii ni kwa sababu alitumia muda mwingi kuweka alama ambayo itawafanya watu wengi wamkumbuke.
Kama ilivyo kwa Ferenc Puskas, dunia pia inamkumbuka Alfred Di Stefano kama mmoja wa washambuliaji hatari kutokea katika uso wa dunia.
Wawili hawa waliwahi kuwekwa kwenye kikosi bora cha muda wote cha RealMadrid kama washambuliaji bora kuwahi kukanyaga nyasi za Santiago Bernabeau.
Nyasi ambazo kila mchezaji hutamani kuzikanyaga, lakini wao walibahatika kuzikanyaga. Wakati miguu yao ikifanikiwa kukanyaga nyasi hizi lakini mikono yao haikuwahi kunyanyua kombe la dunia.
Majonzi ndiyo huanzia hapa, vipaji ambavyo viliwahi kuteka hisia za wengi lakini hazina medali ya kombe la dunia.
Kwa sasa kila nafsi inakiri kuwa dunia iliwahi kupewa zawadi ya kuwa na Paolo Maldini. Beki bora wa muda wote. Mungu alimpa kila kitu, uwezo wa kukaba, kuongoza, kushambulia lakini akamnyima kombe la dunia.
Hapa ndipo ukatili wa dunia unapoanzia ndiyo maana ilikuwa haki kwa Olivier Khan kutoa machozi kipindi Ronaldo De Lima akifunga magoli mawili siku ya mechi ya fainali na kukatisha ndoto yake ya kuchukua kombe la dunia.
Jana Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wametolewa kwenye kombe la dunia. Wanatakiwa kulia kama alivyolia Olivier Khan siku ya mechi ya fainali ya kombe la dunia la mwaka 2006?
Hapana shaka ardhi itaumia ikipokea chozi la Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, wachezaji mahiri kuwahi kutokea. Wamedumu katika kiwango bora kwa muda wa miaka kumi mfululizo bila kushuka.
Wamefanikiwa kuvunja na kuweka rekodi nyingi ambazo zitakuwa kama mlima kwa vizazi vinavyokuja.
Leo hii walie? Hapana, wanachotakiwa kukifanya ni kutabasamu kisha wajivunie kuwepo katika dunia hii kwa ajili ya kutufanya tufurahie mpira.
Macho yetu yameona mambo mengi kwenye miguu ya kina Lionel Messi na Cristiano Ronaldo, mambo ambayo yatatufanya tuwasimulie wajukuuu zetu kuwa tuliwahi kushuhudia miguu ya dhahabu kutoka Argentina na Ureno.
Nchi ambazo ziliwahi kuwa na Eusebio na Diego Maradona. Mmoja aliwahi kushinda kombe la dunia na mwingine hakufanikiwa, yani Eusebio. Mreno ambaye alifunga magoli 749 katika michezo 745 lakini leo hii dunia inamkumbuka kama mmoja wa wachezaji nyota licha ya kutochukua kombe la dunia.
Inawezekana Cristiano Ronaldo na Lionel Messi wakajihisi upweke, lakini wasisahau kuwa hawapo peke yao kwani sehemu waliyopo wapo na watu mahiri wengi kama kina Eric Cantona, Zico, Ian Rush, George Weah, Michel Platini, John Cruyff, George Best, Luis Figo na Paul Gascoigne.
Watu ambao mpaka sasa dunia haijawasaliti ila inawatukuza na kuwaheshimu kama watu muhimu ambao walikuwa na vipaji vikubwa katika uso wa dunia licha ya kutoshinda kombe la dunia.