Fenemeno au kwa lugha nyepesi ya wenzetu ni Phenomenoh ndiyo njia
pekee ambayo unaweza ukamtambulisha mbele ya watu na wakakuelewa
vizuri.
Ni mtu wa ajabu ambaye aliwahi kutokea katika ulimwengu wa soka.
Alikuwepo namba tisa, tulimshuhudia namba tisa bora duniani na
aliondoka namba tisa bora duniani na hatujafanikiwa kupata tena namba
tisa bora duniani tangia Ronaldo De Lima atutoke katika ulimwengu wa
soka la ushindani.
Uwezo wake wa kukimbia na mpira, kasi na nguvu za mguuni ndivyo vitu
ambavyo vilikuwa vinamtambulisha kiurahisi kabla hata ya mabao yake.
Utamchukia kwa lipi Ronaldo ? na utaanzaje kumchukia wakati miguu yake
ilikuwa silaha tosha ya kutengeneza tabasamu la mpenda soka yoyote
duniani ?
Beki gani alikuwa anatamani kukutana na Ronaldo ? Beki gani ambaye
anaweza kupata usingizi wakati anajua kesho baada ya jua kupita
utosini atakutana na shughuli ya kumkaba Ronaldo ?
Haikuwa kazi nyepesi kumkaba Ronaldo na haikuwa kazi ya kufurahia
kumkaba Ronaldo, ni jambo zuri kucheza mechi moja na Ronaldo lakini
lilikuwa jambo la kuhuzunisha kupambana na Ronaldo.
Alikuwa mwiba wa mabeki na sindano ya makipa wengi, hakuna kipa ambaye
angekaa kihasara siku ambayo anacheza na Ronaldo. Kipa atajiandaa,
umakini atauweka zaidi golini ila mwisho wa siku atafungwa.
Huyu ndiye Ronaldo De Lima mshindi mara tatu ya tuzo ya FIFA World
player of the year na mshindi mara mbili wa Ballon D’or. Mtu pekee
ambaye amehusika kulitoa chozi la kipa katili Olivier Khan.
Unaona nini kila unapotazama uso wa Khan ? Uimara, ukakamavu, uanaume
hasa, tena uanaume ambao siyo wa kulia lia.
Ni ngumu kuliona chozi la Khan hadharani, lakini Ronaldo De Lima
alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kumtoa chozi kipa huyu katili.
Mashindano ya kombe la dunia ya mwaka 2002 ndiyo mashindano ambayo
hayatakuwa mepesi kutoka katika ubongo wa Khan.
Magoli mawili ya Ronaldo De Lima ndiyo magoli machungu sana aliyofungwa Khan.
Ilikuwa jambo gumu sana kumfunga Khan , kipa ambaye aliaminika na watu
wengi ana mikono 100. Kipa ambaye alikuwa anajaa golini mpaka unakosa
sehemu sahihi ya kupitishia mpira. Lakini kwa Ronaldo lilikuwa jambo
lililowezekana.
Aliuvaa ujerumani na akachanganya ufundi wa kibrazili kuhakikisha
anavunja ukuta wa Berlin kuipatia nchi yake ushindi.
Kiduku chake kilitosha kuelezea kazi aliyokuwa anaifanya ndiyo maana
taswira ya kiduku chake haijawahi kunitoka kila nikikumbuka mashindano
hayo.
Kuna Ronaldo mmoja tu Duniani, ambaye kwa bahati mbaya hajawahi
kushinda UEFA champions league.Na leo hii tunakumbuka tukio la kigaidi
alilowafanyia Wajerumani