Hii ndiyo mechi ambayo huwa inatazamwa kwa kiasi kikubwa tena kuzidi mechi yoyote duniani. Ndiyo mechi ambayo hubeba hisia za wengi.
Ndiyo mechi ambayo hutazamwa kwa kutumia moyo na siyo macho kama mechi nyingine ambazo tunazijua.
Mioyo ya watu wengi husimama kwa dakika tisini kwa ajili ya kutazama mechi hii tu. Na hii ni kwa sababu moja tu mechi hii ni kubwa sana.
Ndiyo maana ikaitwa El Clásico Ni mechi ya daraja la juu sana. Ni mechi ambayo imebeba timu kubwa mbili duniani.
Timu mbili ambazo wachezaji wengi kwa asilimia kubwa huwa na ndoto ya kuja kuvaa jezi moja wapo kati ya hizi timu mbili.
Yani kwa mchezaji ambaye huchipukia, asilimia kubwa huwaza Real Madrid na Barcelona, huwaza namna ya kuzikanyaga nyasi za Santiago Bernabeau au Nou Camp.
Hapa ndipo Hijja ya mpira wa miguu inapopatikana. Huwezi kusema umekamilisha ibada ya mpira wa miguu kama hujaenda kusajili hapa.
Hii ni picha tosha kuwa timu hizi ni kubwa sana duniani, na zina mvuto mkubwa sana duniani. Ndiyo maana mechi kati yao hushika hisia za watu wengi sana.
Na kwa hivi karibuni umaarufu na mvuto wa El Clásico ulikuwa mkubwa sana. Watu wengi walikuwa wanavutiwa kuitazama mechi hii.
Mpaka ikafikia wakati iwe inachezwa kipindi ambacho kitawapa nafasi mpaka watu wa China kuitazama mechi hii katika muda mzuri.
Unajua hii ni kwa sababu gani?, walitaka kupanua soko la mechi hii kubwa, ili waweze kupenyeza mpaka sehemu ambayo mpira hauna nafasi kubwa.
Ila waliamini kupitia nembo mbili tu ambazo zingewasaidia kupitishia hii mechi mpaka sehemu ambazo zinaonekana hazipendi sana mpira.
Nembo hizo ni Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Hawa wachezaji walitumika kama kitu ambacho kinaweza kusaidia kujipenyeza kwenye nchi kama hizi.
Uwepo wa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi ulikuwa na maana kubwa mbili , maana ambazo zilikuwa zinaibeba kwa kiasi kikubwa hii mechi.
Maana ya kwanza hawa wachezaji wawili walikuwa wana vipaji vikubwa zaidi ukilinganisha na wachezaji wengine waliobaki.
Ukubwa wa vipaji vyao ulikuwa unatazamika kwa maana hii moja kubwa sana, maana ya kuzibeba timu zao kwenye mechi hii.
Mashabiki wengi walikuwa wanaitazama hii mechi ili kuona namna gani ambavyo Cristiano Ronaldo au Lionel Messi ambavyo wengeweza kuzibeba timu zao kipindi kile kigumu.
Yani kama RealMadrid wangekuwa wamebanwa basi macho mengi yaligeuzwa kwa Cristiano Ronaldo kumtazama namna ambavyo angeisaidia timu.
Ndiyo hivo kwa Lionel Messi, wengi walimtazama sana Lionel Messi kipindi ambacho timu yake ilikuwa imebanwa katika mechi hii.
Kwa hiyo vipaji vyao vikubwa vilitazamwa na wengi kuwa kama ukombozi kwenye mechi hii. Hapa ndipo mvuto wa kwanza ulivyokuwa unakuja.
Cha pili ni ushindani mkubwa kati yao. Ushindani huu umeanza miaka 11 iliyopita, kuanzia kwenye tunzo za Ballon D’or.
Walipokezana tunzo hii kwa miaka kumi mfululizo na wakagawana katikati. Kila mmoja akichukua Mara tano tunzo hii.
Ushindani wao kwa wao ilikuwa chachu kubwa nyingine iliyokuwa inaongozeka kwenye mechi hii ya EL-CLASSICO.
Kila mmoja alikuwa anamtazama ni nani angeweza kumfunika mwenzake kwenye mechi husika ambayo iliwakutanisha wawili.
Ni nani angeng’ara sana kwenye mechi hii ?. Na mechi hii ilikuwa na asilimia kadhaa za kutoa mshindi wa ballon d’or.
Ambaye angeng’ara kwenye mechi hii alikuwa na asilimia fulani ambazo zingembeba kwenye tunzo za ballon d’or na hii ni kwa sababu moja tu, mechi hubeba hisia za wengi.
Leo hii Lionel Messi kabaki peke yake, hana mshindani tena, yani yupo kwenye ligi yake binafsi, yule mshindani wake halisi hayupo tena.
Ndiyo maana hata mvuto wa kuifuatilia hii mechi umepungua sana. Tumeshuhudia El Clásico mfululizo hivi karibuni lakini mvuto wake ni mdogo sana ukilinganisha na kipindi ambacho Cristiano Ronaldo alipokuwepo.