*Ulaya watishwa na mataifa ya Amerika
*Brazil presha kubwa, kivumbi Ijumaa
Hatimaye fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil zimemaliza hatua zake mbili za awali.
Mchujo ulifanyika miongoni mwa timu 32 na kupata 16, zikiwamo mbili za Afrika, Algeria na Nigeria na sasa ni hatua ya robo fainali
.
Timu nane zimefanikiwa kuvuka, na karibu zote zimetoka jasho hasa kufika hatua hiyo, ikiwa ni pamoja na kucheza dakika 120 na nyingine kupigiana mikwaju ya penati.
Brazil walikuwa wa kwanza kuvuka kwa tabu, pale walipozuiwa na Chile hadi kwenye changamoto za penati, ambapo palikuwa na kosa kosa kadhaa.
Robo fainali zimepangwa kuanza kuchezwa Ijumaa hii, ambapo Ufaransa watashuka dimbani kupepetana na Ujerumani.
Ufaransa wanaonekana kuwa wazuri mwaka huu tofauti na 2010 walipotolewa katika hatua ya makundi bila kushinda hata mechi moja.
Ujerumani walikuwa wanapewa nafasi kubwa lakini hawakupata ushindi mnono sana kama walivyotarajiwa na walitolewa jasho hadi kufika hapo, wakipelekwa hadi dakika 120 na Algeria kupata ushindi mwembamba wa 2-1.
Brazil waliotishiwa kutupwa nje na Chile katika hatua ya 16 bora watapambana na Colombia wenye mchezo wa kasi na mkali, wote wakitoka bara la Amerika.
Jumamosi ni Argentina dhidi ya Ubelgiji. Argentina si wazuri sana na wametishiwa mara kadhaa kutupwa nje huku Ubelgiji wakijiamini sana na chipukizi wake wakifanya vyema.
Jumamosi hiyo hiyo Uholanzi waliopita baada ya kutolewa jasho sana pia watacheza na Costa Rica ambao wamewashangaza walimwengu kwa kiwango chao cha juu cha soka.
Nusu fainali ni Jumanne na Jumatano, mshindi wa tatu atatafutwa Jumamosi na fainali ni Jumapili ya Julai 13 ambapo pazia la fainali za Kombe la Dunia 2014 Brazil litashushwa.
Katika fainali saba zilizochezwa katika bara la Amerika, hakuna timu ya Ulaya iliyofanikiwa kutwaa Kombe la Dunia la Fifa. Ni Brazil pekee miongoni mwa mataifa nane haya waliofanikiwa kutwaa kombe katika ardhi ya Ulaya walipowafunga Uswisi 5-2 miaka 56 iliyopita.
Kwa hiyo sasa ni nyakati za majaribu kwa kocha wa Uholanzi, Louis van Gaal, wa Ufaransa, Didier Deschamps, Joachim Low wa Ujerumani na Marc Wilmots wa Ubelgiji.
Timu zote hizi za taifa zinafundishwa na makocha ambao ni raia wao, kama ambavyo Ghana na Nigeria pia walikuwa wakifundishwa na makocha raia wao.
Shinikizo lipo kwa Luiz Felipe Scolari kuhakikisha Brazil wanatwaa ubingwa kwenye ardhi yao huku
Alejandro Sabella wa Argentina naye akitaka kulibakisha kombe barani mwake na kuwarejesha Wazungu Ulaya mikono mitupu kwa mara nyingine.
Costa Rica na Colombia wanataka nao kuendelea kuuonesha ulimwengu wa soka kwamba nao wanaweza na watalibakisha kombe barani Amerika.
Bila shaka nyota mpya anayetamba duniani na anayetakiwa na Real Madrid, James Rodriguez atataka kuendelea kuibeba nchi yake ya Colombia akiwa ameshafunga mabao matano hadi sasa.