Robin Van Persie njia panda
*Kuna hofu Kocha ‘wake’ Juventus atafungiwa
*Man U haielekei kufika dau, RVP haihusudu City
Nahodha wa Arsenal, Robin van Persie anaelekea katika hatari ya kutopata chaguo alilotaka.
Laiti Arsenal wakamilishe mipango ya kumsajili Santi Cazorla kutoka Malaga, RVP ataishia kama mpenzi aliyekataliwa kwa bezo.
Mholanzi huyu ana klabu tatu zinazomuwania: Juventus, Manchester City na Manchester United, huku Arsenal wakitaka abaki nao, lakini ameshasema haongezi mkataba.
Juventus wanaelekea wanachoka kusubiri. Walitoa dau la awali lililokataliwa haraka. Wamekuwa wanataka kuingia mkataba wa miaka mitano na RVP wenye thamani ya Pauni 190,000 kwa wiki baada ya kukatwa kodi.
Lakini pia, wakati Kocha Antonio Conte wa mabingwa hao wa Italia akiwa katika hatihati za kufungiwa baada ya kudaiwa kuhusika na kashfa ya kupanga matokeo, RVP anaanza kupata ufufutende wa kuhamia klabu hiyo aliyoihusudu.
Dau la kwanza la Juventus ni dhahiri lilikuwa dogo, na likakataliwa kihalali. Wamerejea tena kwa mazungumzo, lakini inaelekea hawajakaribia bei ya Arsenal kwa nahodha wao huyu wa msimu uliopita.
Nyuma ya pazia, Manchester United wanaonekana kujiamini kumnasa. Hata hivyo, kuna hisia kwamba hawataongeza kitita, licha ya kukataliwa kwa dau la chini kidogo ya Pauni milioni 15 walilotoa.
United wanazingatia kwamba Van Persie anatimiza miaka 29 mwezi huu, amekuwa na rekodi mbaya ya kuumia, hivyo uwezekano wa kuja kumuuza kwa faida baadaye ni mdogo sana.
Mazingira yake hayaendani na falsafa ya klabu hiyo katika uhamisho wa wachezaji.
Pengine Mashetani Wekundu hawa wanavizia Arsenal ifikie mahali pa kulazimika kupunguza dau lao kadiri mwezi wa mwisho wa usajili – Agosti unavyosonga mbele.
Fikara za wanunuzi hao watarajiwa ni kwamba Arsenal wataona afadhali wamuuze kwa bei pungufu ya Pauni milioni 20 badala ya kuja kumpoteza bila kupata senti tano mwaka mmoja tangu sasa, mkataba wake Emirates utakapomalizika.
Kwa upande mwingine, inaaminika kwamba RVP hawapendi Manchester City – licha ya kuwa wamewasilisha dau la kumsajili. Matajiri hao wa Manchester wanatambua hali hiyo ya RVP, ndiyo maana wanatafuta mbadala kama Gonzalo Higuain.
Lakini City lazima wauze kabla ya kununua.
Viongozi wa mabingwa hao wa Uingereza wanataka kupunguza washambuliaji watatu kati ya Carlos Tevez, Emmanuel Adebayor, Roque Santa Cruz na Edin Dzeko kabla ya kusaini nyota mwingine.
Yote haya yanamwacha Van Persie njia panda.
Baada ya awali kulilia kwenda Juventus, sasa suala la klabu kupoteza kocha aliyewapa ubingwa si habari nzuri hata kidogo, ndipo anapata mpasuko wa moyo.
Dalili zote sasa zinaonesha safari yake ni kuelekea Old Trafford, lakini ukweli ni kwamba bado Man U wapo mbali katika mazungumzo ya kibiashara na Washika Bunduki hao wa London.
Itakuwa ajabu, hata hivyo, ikiwa Arsenal hawatamuuza mchezaji huyu msimu huu wa kiangazi.
Ni kweli Kocha Arsenal Wenger kung’ang’ania msimamo wake wa kumwacha Arsenal jambo zuri linaloeleweka, habari ni kwamba lazima wamuuze RVP. Jingine lolote katika mazingira ya sasa halitapatiwa maelezo ya kukubalika.
Ingawa hivyo, haya yanamweka Van Persie katika wakati mgumu mno. Je, aende Manchester City kinyume cha matakwa ya dhamiri yake?
Au labda abaki akiomba United wabadili msimamo wa dau, jambo ambalo si la kawaida katika utamaduni wa klabu hiyo.
Labda aende tu Juventus, lakini je, itawezekana kwenda kwenye klabu iliyo katikati ya mawimbi mazito hivyo?
Walichokuwa wanafanya Juventus ni kujaribu kwa nguvu kumshawishi aende Italia, lakini sasa mambo yanakuwa magumu.
Kutokana na kauli ya RVP kwamba hangeongea mkataba Arsenal na aliyoandika kwenye tovuti yake kukosoa falsafa ya klabu, inaelekea hawezi tena kula matapishi yake.
Kwanza washabiki si rahisi wamkubali tena, hasa baada ya kumpata Cazorla anayepewa mkataba wa miaka minne.
Huyu anaonekana kuwa mchezaji muhimu katika kuongoza mashambulizi na kuwapanga wenzake, tena akicheza namba 10 katika mfumo mpya wa klabu hiyo msimu ujao.
Hata hivyo, Arsenal inakabiliwa na vigingi katika kukamilisha usajili wa Cazorla, na kazi si rahisi.
Hii ni kwa sababu Malaga ipo kwenye mtikisiko wa uchumi, mikataba ya wachezaji imekuwa tatizo kubwa linalouumiza uongozi na wamiliki.
Ikiwa Arsenal watafanikiwa kumnasa Cazorla ambaye tayari amefanyiwa vipimo kuthibitisha uimara wa afya yake, huenda wasihangaike tena na nyota wa Real Madrid, Nuri Sahim.
Wanaweza kuwasajili wote hata hivyo, Sahim kwa mkopo labda, lakini baada ya kukataa madau mengi kupita kiasi msimu uliopita wa usajili, na hii sio kawaida yaWenger.
Arsenal wamekuwa wakijadiliana na Alex Song juu ya mkataba mpya. Lakini huyu bado ana miaka mitatu Emirates, huku Barcelona wakiwa wameonesha nia ya kumchukua. Mambo yakienda namna hiyo, basi tutajua kwa nini Gunners wanapiga hesabu za Sahin.
Kilicho wazi ni kwamba Arsenal wanajipanga upya, wanajijenga kuwa imara, wanajiandaa kwa maisha bila Van Persie – hata kabla hajaondoka.
Mholanzi huyu ndio kwanza amemaliza msimu uliompandisha katika kilele cha soka yake, akifunga magoli ya kiwango cha kimataifa, lakini si ajabu akajikuta anajikunyata mwenyewe kwenye baridi kali.
Kulikoni hali ya ajabu kiasi hiki, na kweli msimu huu wa usajili wa kiangazi unaonesha umekuja na yake. Pengine ni msimu wa kawaida katika wazimu wa uhamisho kwa upande wa Arsenal.